July 31, 2017


Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog ametamba kuwa hataki utani kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara huku akiahidi kuja na mbinu mpya zitakazofanikisha malengo yake ya ubingwa.

Simba kwenye msimu uliopita iliukosa ubingwa dakika za mwisho baada ya kuongoza kwenye ligi hiyo kwa muda mrefu kabla ya Yanga kuwapita na kuchukua taji hilo.

Timu hiyo, hivi sasa ipo kambini nchini Afrika Kusini ikijiandaa na msimu mpya wa ligi unaotarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu.

Omog alisema kikubwa atakachokifanya kwenye msimu ujao ni kutoidharau timu yoyote watakayokutana nayo katika ligi kuu.

Amesema anataka katika msimu ujao kushinda kila mechi ili wajiwekee mazingira mazuri ya ubingwa huo baada ya kuukosa kwa miaka mitano.

Aliongeza kuwa, dharau ndiyo zimechangia kwa kiasi kikubwa wao kuukosa ubingwa huo na kwenda kwa watani wao wa jadi Yanga.

"Niseme tu kuwa, dharau ndiyo zimesababisha sisi tuukosa ubingwa wa msimu uliopita wa ligi kuu, hivyo hilo nimeliona nimepanga kulimaliza tatizo hilo kwa kuwatengeneza kisaikolojia wachezaji wangu.

"Katika msimu uliopita wachezaji wangu walikuwa wakikutana na timu ndogo wanadharau na kusababisha kupata matokeo mabaya ambayo yalikuwa yanatuweka katika nafasi mbaya ya kuuchukua ubingwa sitaki hilo litokee tena msimu ujao," alisema Omog. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV