July 28, 2017Na Saleh Ally
AGOSTI 23 kutakuwa na mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba watakapokutana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hiyo ni mechi ya Ngao ya Jamii ambayo huwa ni maalum kwa ajili ya msimu mpya na inakuwa gumzo zaidi kwa kuwa inawakutanisha watani wa jadi, Yanga na Simba.

Inawakutanisha mabingwa wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wale wa Kombe la Shirikisho. Utaona mechi hiyo msimu huu imekuwa gumzo sana kwa kuwa inawakutanisha watani hao.

Miaka mitatu iliyopita, mara nyingi mechi hiyo huwakutanisha Yanga na Azam FC ambao walitawala katika nafasi ya kwanza na pili. Au nafasi ya kwanza ikawa Yanga katika Ligi Kuu Bara lakini ikabeba Kombe la Shirikisho lakini Azam FC akawa wa pili.

Gumzo la mechi hiyo ya watani, linajumuishwa na usajili mpya ambao umefanywa na timu zote mbili. Simba ikionekana kuwa imesajili wachezaji wengi wapya zaidi.

Kitu kibaya zaidi ambacho mimi nakiona, hasa kwa Simba kwamba mashabiki wao wanaona usajili wao umemaliza kila kitu na watakapokutana na Yanga watakachofanya wao itakuwa ni kutoa adhabu tu.

Lakini kwa Yanga nao wako ambao wanaona kikosi chao kimefanya usajili mzuri lakini hawa ni wachache na wengi wanaona kama Yanga haikufanya usajili mzuri kwa kuwa hakukuwa na mbwembe kama zile zilizozoeleka hapo awali.

Kama itatokea Simba ikapoteza mchezo huo wa Ngao ya Jamii, maana yake kitakachofuatia ni maneno mengi ya kejeli kutoka kwa watani wao. Kawaida mashabiki wa timu hizi hawataki kufungwa na wasingefurahia kuona upande mwingine unajigamba unavyotaka wenyewe.

Hivyo maneno mengi yanaweza kugeuka kuwa shida kwao na kuwapa wakati mgumu. Mwisho hasira zao watazimalizia kwa uongozi au wachezaji wa timu zao na mwisho watajivuruga.

Hali kama hiyo inaweza kutoa upande wa Simba pia ambao wanaona kuwa usajili wao ni safi sana na hawafungiki. Kama watapoteza mechi dhidi ya Yanga, basi kuanzia hapo inaweza ukaanza mgogoro ule wa kusema tumesajili wachezaji wa majina na hatujafanya kitu!Nasema haya kwa kuwa nimeanza kuona mapema hali ya mihemko inajitokeza katika kila upande hata kabla ya mechi yenyewe. Hali inayoashiria kuwa baada ya mechi hiyo hakutakuwa salama.

Mechi ya Ngao ya Jamii, haitakuwa na sare. Maana yake mmoja lazima apoteze. Hivyo ni mechi ambayo lazima itakuwa na maumivu kwenda kwa upande mmoja.

Atakayepata maumivu atakuwa na uvumilivu wa aina gani ili kuepuka kujivuruga. Maana kama Yanga watafungwa wanaweza wakaibeba hali ya kuamini hawakusajili vizuri, wakaanguka kabisa. Lakini Simba pia inaweza kuwatokea, mwisho wakaamini hawakusajili vizuri zaidi ya majina tu, wakaporomoka kabisa.

Kitu ambacho wanachotakiwa kufanya mashabiki na viongozi ni kuacha makocha na wachezaji wafanye kazi yao, yaani wawaamini. Baada ya mechi hiyo ya Ngao ya Jamii, waanze kutoa maoni yao kwa njia sahihi kama tathmini.

Itakuwa ni kabla ya ligi na baada ya hapo kutakuwa na wiki moja ya kurekebisha mambo kabla ya kuingia katika ligi yenyewe ambayo ndiyo kila kitu.

Hadi sasa Yanga na Simba zinajiandaa kwa ajili ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho halafu itafuatia michuano ya kimataifa. Hakuna timu inayojiandaa na mechi ya Ngano ya Jamii kama mashindano.


Hivyo kama Simba au Yanga, hawatafurahia kufungwa halafu watafanya mambo ambayo yanaweza kuwaangusha baadaye kwa kuwaingiza katika malumbano ya wenyewe kwa wenyewe. Mwisho watajiondoa relini, watashindwa kutulia na mwisho, watashindwa kufanya vizuri katika ligi na mafanikio yatakuwa hadithi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV