Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon, amesema kuwa, kutokana na kila timu zitakazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao kufanya usajili wa uhakika, kilichobaki ni kukutana uwanjani kuthibitisha hilo.
Omog ameyasema hayo huku Yanga ikiwa kwenye hatua za mwisho za kukamilisha dili la kiungo mkabaji, Papy Kabamba Tshishimbi raia wa DR Congo, pia ikiwa tayari imewasajili Ramadhan Kabwili, Baruan Akilimali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Ibrahim Ajibu na Mcameroon Rostand Youthe.
Wakati Yanga ikiwanasa wachezaji hao, Simba yenyewe imewasajili Emmanuel Mseja, Ally Shomary, Jamal Mwambeleko, Yusuph Mlipili, Emmanuel Okwi, Nicolaus Gyan, Said Mohammed, Shomari Kapombe, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, John Bocco, Aishi Manula na Haruna Niyonzima.
Omog amesema kila timu imefanya usajili na kwa kuwaangalia tu ni wachezaji wazuri, hivyo anasubiri kuona uwanjani kama kweli watathibitisha ubora wao.
“Sisi tumesajili na timu nyingine zimesajili, najua katika kipindi hiki kila timu inajipanga kuhakikisha inafanya vizuri msimu ukianza.
“Wachezaji waliosajiliwa wote ni wazuri kwa kuwaangalia tu hivi, lakini nasubiri kuwaona uwanjani kama kweli ubora wao utakuwa kama vile wengi wanavyotarajia. Nasubiri ligi ianze kuthibitisha hilo,” alisema Omog.
0 COMMENTS:
Post a Comment