July 7, 2017



Kama umesikia, kipa namba moja wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ alidai kuwa kuna uwezekano mkubwa msimu ujao asiwe na kikosi cha klabu hiyo kutokana na kupata ofa katika timu tatu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Kutokana hali hiyo, hivi sasa anajiandaa kwa ajili ya kwenda kujiunga na moja kati ya timu hizo baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Yanga ambayo ameitumikia kwa mafanikio makubwa tangu alipojiunga nayo akitokea Azam FC.

Hata hivyo, imebainika kuwa timu hizo za Afrika Kusini ambazo Dida anadai kuwa zinamuhitaji ni danganya toto na badala yake anatarajia kujiunga na Singida United ambayo inafundishwa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm ambaye mwanzoni mwa msimu uliopita alikuwa akiifundisha Yanga.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Singida United ambazo Championi Ijumaa limezipata zimedai kuwa, wapo katika mazungumzo na Dida na endapo mambo yatakuwa sawa basi anaweza kujiunga na timu hiyo.

“Tupo katika mazungumzo na Dida ya kutaka kumsajili baada ya kocha kutuambia kuwa kwa sasa ni mchezaji huru, hana tena mkataba na Yanga na mambo yakiwa sawa tunaweza kumsajili.

“Hata hivyo, viongozi wetu wanafanya siri kubwa sana kwani inavyoonekana Yanga pia bado wanamhitaji, kwa hiyo hataki wajue, lakini kuhusiana na ishu ya Afrika Kusini anakosema kuwa anataka kwenda ni geresha tu anawapoteza maboya Yanga,” kilisema chanzo hicho cha habari.


Alipotafutwa Dida ili aweze kuzungumzia suala hilo, hakupatika kutokana na simu yake ya mkononi kutokuwa hewani lakini alipoulizwa kuhusiana na hilo, Mtendaji Mkuu wa Singida United, Festo Sanga, alisema: “Dida ni kipa mzuri lakini siwezi kusema chochote kwa sasa kama tunamuhitaji au la ila ni kweli kabisa tunatafuta kipa.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV