July 22, 2017




Na Saleh Ally
ROGER Lukaku alikuwa ni kati ya wachezaji wa Zaire walioshiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 1994 nchini Tunisia lakini hawakufika mbali.

Zaire ndiyo DR Congo kwa sasa. Huyu aliamua kuhamishia maisha yake nchini Ubelgiji ambako baadaye alianzisha familia na mmoja wa watoto wake ni Romelu Menama Lukaku Bolingoli. Sasa ni mshambuliaji mpya wa Manchester United.

Lukaku alijua baba yake aliwahi kucheza hadi timu ya taifa ya Zaire. Lakini alichochagua kwake ni jina la Lukaku, hakupenda kutumia lile la Bolingoli kama ndugu zake wengine Wacongo.

Mfano, binadamu yake Bolingoli-Mbombo anayekipiga Club Brugge ya Ubelgiji. Aliamini jina la Lukaku kwa kuwa baba yake alishaanza kulitangaza, angependa liendelee kufanya vizuri.

Kwake alimueleza baba yake kwamba angependa kuwa mchezaji bora kama ilivyo kwa Didier Drogba ndiyo maana alivutiwa siku moja angecheza Chelsea. Kweli ndoto yake ilitimia lakini hakuna ambaye aliamini angekuwa bora na gumzo siku moja.

Lukaku sasa ni gumzo akiwa ametua Man United kwa uhamisho wa zaidi ya pauni milioni 75 na kumfanya kuwa mmoja wa wachezaji ghali duniani.

Amejiunga na Man United akitokea Everton huku wengi wakiwa wanaamini huenda angejiunga na Chelsea timu ambayo alikuwa akiipenda. Inaonekana ushawsishi wa Kocha Jose Mourinho ulimfanya abadili mawazo.

Kinachovutia ni kwamba, Lukaku anaaminika kuwa mchezaji mwenye mafanikio aliyekatishwa tamaa mara nyingi zaidi kabla ya kuanza kufikia mafanikio.

Katika timu nyingi alizocheza akiwa mtoto au kijana, ilionekana kuwa ni mzito na yuko taratibu sana asingeweza kucheza na kufunga mabao kama yeye alivyotamani kuwa Drogba, gwiji kutoka Chelsea na Ivory Coast.

Huenda alikosea kutangaza mapema alitaka kuwa nani na waliokuwa wakimpa maoni, waliangalia zaidi Drogba yukoje na kumkatisha tamaa yeye kwa kuona anapoteza muda wake.

Kwa umbile lake, Lukaku alikuwa akiongezeka kilo kwa haraka sana. Daktari alisema ilitokana na mifupa mikubwa aliyo nayo aliyoieleza ni mizito na imara zaidi.

Hali hii ilifanya makocha kadhaa kumshawishi kucheza kama beki wa kati au namba sita kwa kuwa ana sifa ya kumiliki mpira kwa ustadi mkubwa. Aliendelea kukataa na kushikilia msimamo wake wa kutaka kucheza kama mshambulizi kwa kuwa ndoto yake alitaka kuwa Drogba.



Wakati anatua Everton akitokea Chelsea, msimu huo katikati alifikisha kilo 100 na kumfanya kuwa mchezaji mzito zaidi katika Ligi Kuu England. Alipata ushauri wa kupambana na kilo na daktari alimtaka kufanya hivyo kuongeza usalama wa viungo vya mwili wake wakati akiwa uwanjani. Aliufuata ushauri huo kwa kuufanyia kazi.

Hadi anaondoka Everton kwenda Manchester United, Lukaku alikuwa na kilo 91, kabla ya hapo alifikia hadi kilo 94 akitokea 100. Akiwa ni hatari kwa kufunga, msumbufu kwa mabeki na gumzo sasa duniani kote huku Chelsea nao wakionyesha walimtaka lakini ujanja wa Mourinho ukawatoa relini.

Waliokuwa wakimshauri hawakuwa na nia mbaya kwa kuwa mabeki wengi au walinda mlango ndiyo wanakuwa na kilo nyingi kutokana na maumbo yao lakini bado si shida kwa nafasi zao.

Ni aghalabu, kukuta mshambuliaji ana kilo 100 kama ilivyo kwa Lukaku au Adebayo Akinfenwa ambaye sasa anayekipiga Wycombe Wanderers ambaye anafikisha kilo 103 na umbo lake linaonyesha wazi kuwa ana kilo nyingi na haipingiki. Huenda kwa Lukaku ikawa vigumu kugundua.

Nilichokilenga hapa ni alipofikia Lukaku ambaye anatokea nchi jirani na Tanzania ya DR Congo na kwamba ni mtu ambaye alishikilia na kusimamia kile alichokuwa akitaka kukitimiza licha ya ushauri mwingi.



Kama nilivyosema waliomshauri hawakuwa na nia mbaya, lakini wakati mwingine ushauri unaweza kukatisha ndoto zako kama utakuwa mwoga. Leo walioamini Lukaku asingeweza, watakuwa wanashangazwa naye.

Kwani anaendelea kuwa mmoja wa wachezaji wenye miili mikubwa lakini washambuliaji hatari na sasa ni mmoja wa wachezaji ghali kabisa. Sasa jiulize wewe, ulikopita mara ngapi ulipinda njia ya kuziacha ndoto zako kwamba ulikuwa ukitamani kuwa fulani lakini ukaogopa baada ya kupewa ushauri kuwa hutaweza.

Kama Lukaku angeogopa, leo angekuwa anacheza nafasi ya ulinzi au kipa. Asingefanikiwa kupata mafanikio na kujifananisha na Drogba lakini asingeibuka mchezaji bora kwa misimu miwili mfululizo akiwa Everton na huenda leo asingekuwa mchezaji ghali kama alivyo.


Kumbuka, kupokea ushauri ni jambo jema lakini kuuchambua kwa kuufanyia kazi kwanza ni jambo muhimu zaidi. Pia nakukumbusha, kujiamini kuwa unaweza wakati wengine wanaamini hauwezi, ni dawa sahihi ya kukufikisha ambako wengi wanaamini hautaweza kufika.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic