August 11, 2017





Mnigeria Eisa Mfowoshe akiwa mazoezini.
KATIKA kuiimarisha safu yao ya ulinzi, Yanga imemshusha nchini beki Mnigeria, Eisa Mfowoshe aliyemaliza mkataba wa kuichezea Klabu ya Itihad ya Oman. Ujio wa beki huyo unakamilisha idadi ya wachezaji watatu waliokuwepo kwenye majaribio ya timu hiyo wengine ni beki Mnigeria, Henry Okoh na kiungo Fernando Bongyang na Mfowoshe.

Kati ya wachezaji hao mmoja pekee ndiye anatakiwa asajiliwe ili akamilishe idadi ya wachezaji saba wa kimataifa kati ya sita ambao tayari wamesajiliwa na Yanga. Championi Ijumaa lilikuwepo kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kumshuhudia beki huyo akionyesha uzoefu wa kupambana na washambuliaji wenye uwezo wa juu.

Katika mazoezi hayo, beki huyo mwenye umbile kubwa alionekana akifanya program zote kwa makini huku akionyesha uhodari wake wa kupiga pasi zilizonyooka ndefu na fupi kwa wenzake. Wakati mazoezi hayo yakiendelea, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina alimpangia washambuliaji wawili, Donald Ngoma na Amissi Tambwe kwa ajili ya kumpima.

Mnigeria huyo alionyesha uhodari wa kuwadhibiti huku akitumia vema umbile lake kubwa kuokoa mipira ya juu kwa vichwa na kupanga mabeki wenzake aliocheza nao akiwemo Kelvin Yondani kama vile wameshacheza pamoja muda mrefu.

Mara baada ya mazoezi hayo kumalizika, Championi Ijumaa lilizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Husseni Nyika kuhusu suala hilo, alisema:

“Mfowoshe amekuja jana (juzi) na kuanza majaribio na Yanga ili kocha amuangalie na kama akimshawishi, basi tutamsajili. “Beki huyo ni mchezaji huru aliyemaliza mkataba wa kuichezea Itihad hivi karibuni kwa mujibu wa wakala wake.

“Hivyo, wakati akiwa kwenye majaribio, nimezungumza na kocha amjaribu kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting tutakayocheza Jumamosi (kesho),” alisema Nyika. Usajili wa wachezaji wa kigeni utafungwa rasmi Agosti 15, mwaka huu.

NA: WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA| CHAMPIONI IJUMAA

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic