August 2, 2017
Na Saleh Ally
KIUNGO Athumani Iddi Athumani amerejea tena katika soka la ushindani kwa maana ya kucheza kwa mara nyingine Ligi Kuu Bara.

Iddi maarufu kama Chuji amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Ndanda FC ya Mtwara, timu ambayo msimu uliopita iliponea chupuchupu kuteremka daraja baada ya uongozi kuyumba katika mambo mengi hasa ya kuihudumia timu hiyo.

Katika hali ya kawaida unaweza kusema Chuji amerejea kazini na kuwakuta wachezaji wengi aliowaacha wakiwa wamepiga hatua kubwa kabisa.

Mfano, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani au Mnyarwanda, Haruna Niyonzima aliyekuwa pacha wake kama kiungo mchezeshaji yeye akicheza kiungo mkabaji bado wanaendelea kucheza na wanashikilia njia yao sahihi.
Chuji alipotea njia, alikwenda katika mpito usio sahihi na mwisho akaishia kuyumba. Kwani utaona hata baada ya kuondoka Yanga, alipotua Mwadui FC alishindwa kuonyesha kilicho sahihi na mwisho akapotea kabisa.

Kuondoka kwa Chuji Yanga, kumeacha rekodi moja kwa zaidi ya misimu mitano sasa. Hakuna namba sita aliyeishika namba hiyo na kuitumikia akijihakikishia kwamba anaweza.
Hii ni rekodi kwani kwa misimu yote hiyo, Yanga imekuwa ikisumbuka kupata kiungo mkabaji ndani na nje ya Tanzania na wengi wameonekana kushindwa au kuonekana si “Natural defensive Midfielders.”

Kawaida mpira namba na watu wa asili ambao hawajatengenezwa. Lakini wakati mwingine hulazimika kutengenezwa. Kwa Chuji mambo yalikuwa rahisi zaidi kwa kuwa wakati akiwa Polisi Dodoma ambako Simba walimtoa, alikuwa akicheza kama namba nne au tano tegemeo.
Hata alipoamua kusogea juu, kwake ilikuwa rahisi zaidi kutokana na kipaji chake cha unyumbulifu wa mwili kinachozaa kontroo murua inayomfanya kujiamini na kufanya vitu vingi sahihi.

Sasa amerejea baada ya utulivu na mwenyewe kuamua kujirekebisha. Huenda michuano ya Ndondo Cup imemsaidia kujenga imani upya kwa baadhi ya wadau ambao walimuona akiitumikia timu ya Faru Jeuri.

 Chuji atakuwa na mtihani mkubwa kwa kuwa safari hii atakuwa anajaribu kwa mara ya pili kuuonyesha umma wa wapenda mpira kuwa amerejea na anaweza kukipa nafasi kipaji chake kikamrejesha katika njia sahihi. Kazi kubwa itakuwa kwake hata kama Ndanda FC kupitia uongozi wake itafeli tena. Bado Ndanda FC haijafanya usajili wa uhakika kubadilisha mambo wakati siku za kufunga dirisha zikiwa zinakwenda ukingoni. Lakini bado Ndanda FC haijaonyesha kwamba ina mpango madhubuti wa kubadilisha mambo na kuwa timu mpya yenye malengo tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

Chuji atakuwa na mzigo mkubwa kwa kuwa kwanza aliwahi kufeli baada ya kutoka Yanga, alipokwenda Mwadui FC akaonyesha hawezi na kukawa na maneno mengi ya kuendekeza starehe kuliko kazi jambo ambalo alishindwa kulipangua kwa kuwa, kweli hakuwa katika kiwango chake.

Mzigo wa kwanza wa kuonyesha kwamba amebadilika na anaweza kucheza katika kiwango kilichowatesa Yanga kumpata mbadala ndiyo huu. Lakini bado atakuwa na mtihani wa kuibeba Ndanda FC kama mzoefu na lazima awe mvumilivu kwa kuwa maisha ya Ndanda FC  hayawezi kuwa kama ya Yanga au ikiwezekana kama Mwadui FC ya wakati ule inaanza.

Mbaya zaidi, hata kama mambo si mazuri sana ndani ya kikosi cha Ndanda FC, bado Chuji atatakiwa kufanya kazi yake kwa ufasaha, kazi yake kwa weledi na kuonyesha utumishi bora ili kuepuka kufeli kwa mara nyingine.

Lazima kabla ya kwenda Ndanda FC, Chuji alitafakari mengi. Kwamba ni sehemu ya namna gani na kwamba kama yakitokea matatizo lazima awe mvumilivu na kama Ndanda FC watakuwa wamejirekebisha pia itakuwa ulaini wa mambo kwake kwa kuwa itampunguzia presha.

Katika hali ya kawaida, Chuji ni kama amerejea kuchagua mwisho wake kisoka kama utakuwa mzuri au ataupaka matope na kumaliza kwa sifa mbaya ya kufeli.

 Huenda Chuji atakuwa na wakati mgumu zaidi kipindi hiki kwa kuwa wapo watakaomvika uzee au kumkumbushia alivyowahi kufeli hapo nyuma kwa kila kosa moja atakalofanya. Kikubwa anachotakiwa kufanya ni kuwa na moyo wa chuma lakini ubongo wenye jicho la tai kwa kuwa anatakiwa kuona mbali kuliko alipo sasa pia kuamua ya kesho kabla ya jua kuzama.


 Hata akicheza kwa kiwango bora vipi. Misimu miwili hadi minne ijayo itamlazimu Chuji kupumzika na hasa kama atakuwa fiti na moyo wake unaitaka kazi hiyo. Hivyo, acha tumpe nafasi lakini nasi tufungue mioyo yetu tukisubiri kuona ameamua kumalizaje mpira wake. Karibu tena baba Sabry.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV