August 2, 2017Na Saleh Ally
UTAKUWA umesikia mengi kuhusiana na Raphael Daud ingawa niliwahi kumuita kwa jina la Raphael Alpha kwa kipindi kirefu kabisa.

Baadaye niliambiwa jina lake sahihi ni Raphael Alpha. Jina lake lilibadilishwa baada ya kutokea makosa wakati wa usajili wa leseni katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Raphael Alpha hadi leo ni mchezaji kinda katika kikosi cha vijana cha Mbeya City. Raphael John yeye alikuwa katika kikosi cha wakubwa lakini majina yao yakachanganywa naye akalazimika kutumia jina hilo ili acheze ligi hadi liliporekebishwa.

Leo ninamzungumzia Raphael Daud kamili, kiungo ambaye alianza kuichezea Mbeya City katika msimu wa 2014-15. Hata hivyo, haikuwa rahisi kwake rahisi kwake baada ya kukaa benchi mzunguko wote wa kwanza, kocha akiwa ni Juma Mwambusi.

Mechi ya kirafiki dhidi ya Majimaji ikiivaa Mbeya City, Raphael alikuwa katika benchi tena. Bahati mbaya mkongwe Steven Mazanda aliumia, akaenda benchi na bahati nzuri kwa Raphael akaingia kuchukua namba.

Baada ya mechi hiyo kwisha, kocha Mwambusi alichukua uamuzi wa kumrudisha Mazanda kucheza namba sita na moja kwa moja akamkabidhi Raphael dimba la juu.

Mzunguko wa pili wa ligi, alicheza mechi zote 15 za mzunguko wa pili na kufanikiwa kufunga mabao manne.

Msimu uliofuata yaani wa 2015/16 alicheza mechi zote 25 akiwa fiti na kufunga mabao sita. Kama hiyo haitoshi, msimu uliofuata au uliopita, Raphael akaichezea Mbeya City mechi 27, akikosa tatu tu na kufunga mabao nane.

Kwa taarifa yako, ingawa ni kiungo mchezeshaji hadi sasa tokea Mbeya City imeingia Ligi Kuu Bara ndiye mfungaji bora, akiwa amefunga mabao 18 na kufuatiwa na Patrick Mangungulu mwenye bao 17.

Kwa rekodi chache nilizokupa, nataka kukuthibitishia kuwa kati ya usajili bora kabisa walioufanya Yanga msimu huu, basi Raphael ni mmoja wao na kama ni moja ya chaguo sahihi amelifanya kiungo huyo basi ni kujiunga na Yanga, nitakuambia kwa nini.

Yanga imeondokewa na Niyonzima ambaye ilimtegemea kama kiungo mchezeshaji. Huenda ilipanga kumtumia Thabani Kamusoko, kama ikimalizana na Papy Tshishimbi raia wa DR Congo kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland.

Bado naona itakuwa kosa kubwa kama Kocha George Lwandamina hatamuamini kiungo huyo kinda ambaye kwa misimu mitatu mfululizo hajakosa hata mechi sita.

Lwandamina ni kocha mtaalamu sote tunajua, lakini nimeona makocha wengi wangependa kuchagua wachezaji wa nje zaidi kwa ile imani mchezaji wa kimataifa hapaswi kukaa benchi.

Vizuri ampe nafasi na asimbeze au kuona umri wake bado ni mdogo. Ninaamini atakuwa na msaada ingawa Raphael atakuwa na kazi ya kumshawishi kocha kama kweli atakuwa msaada kwake.Kama Lwandamina angeniambia nimpangie kikosi, basi ningempa hiki kifuatacho. 1. Youthe Rostand 2. Juma Abdul 3. Haji Mwinyi 3. Kelvin Yondani 5. Nadir Haroub 6. Papy Kambamba 7. Obrey Chirwa 8. Raphael Daud 9. Donald Ngoma 10. Ibrahim Ajibu 11. Thabani Kamusoko.

Mchezaji ambaye amekuwa na kiwango cha juu, nidhamu ya kuvutia na mshindani sahihi ambaye lazima kukubali kumpa muda hata kidogo kwa kuwa anakwenda katika timu kubwa yenye presha ya juu zaidi.

Huenda akawa ana nafasi ya kujifunza na kupata nafasi kwa kuwa Mbeya City kwa kuwa ni timu ya mashabiki wengi na wanachama, presha yake inaweza kuwa imemsaidia kidogo kwenda kuungana na presha ya Yanga.

Kwake Raphael nataka kumpa moyo kwa kuwa namuona ni hazina kubwa ya taifa letu baadaye. Namuona ana sura ya wachezaji wenye nafasi ya kucheza nje ya Tanzania na kuitangaza Yanga na nchi yetu pia kuwa msaada katika timu yetu ya taifa.

Huenda anaweza kushindwa kidogo wakati akijifunza kadhaa, lakini ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi na zaidi kutokana na mwenendo wake. Huenda jambo jema zaidi itakuwa ni kujilinda na “madudu” ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa tumeona wengi wakitokea timu za mikoani na nidhamu zao, lakini wakifika Dar es Salaam na kujiunga na timu kubwa au maarufu, tunaanza kuona wanabadilika na hawashikiki tena kwa muonekano wa usiku katika kumbi za starehe.


Kama kweli Raphael anataka mpira, basi ninaamini ataweza na hakuna wa kumzuia kufika mbali. Kama anataka mengine, Dar es Salaam yanapatikana kirahisi zaidi na suala la kuchagua linaendelea kubaki ndani ya moyo na ubongo wake.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV