August 4, 2017


Ombi la aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji la kutaka apewe dhamana katika kesi inayomkabili ya uhujumu uchumi, linaonekana ni bado kitendawili baada ya leo kushindwa kutolewa uamuzi kutokana na Jaji Isaya Arufani wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutokuwepo mahakamani hapo kusikiliza ombi hilo.

Manji alipeleka maombi hayo katika mahakama hiyo kupinga hati iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuzuia dhamana dhidi yake.


Kutokana na jaji huyo kutokuwepo, ombi hilo limesogezwa mbele na linatarajiwa kusikilizwa Agosti 7, mwaka huu.

Ikumbukwe kuwa, Manji na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya uhujumu uchumi, kukutwa na mihuri miwili ya JWTZ, ukiwemo wa Mkuu wa Kikosi cha 21 JWTZ, wa Mkuu wa Kikosi Makutupora Dodoma (JWTZ) na wa Commanding Officer Korogwe, plate number mbili za magari ya serikali jambo ambalo ni kinyume cha sheria. 

Katika kesi hiyo ambayo inaendeshwa na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Huruma Shaidi, leo asubuhi ilitajwa katika mahakama hiyo na kuahirishwa hadi Agosti 9, mwaka huu kutokana na Manji kutofika mahakamani hapo.


Manji alishindwa kufika mahakamani Kisutu kutokana na kuwa na kesi katika Mahakama Kuu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV