August 26, 2017


Na Saleh Ally
KUISHI ndiyo shule namba moja, kila unavyozidi kuishi ndiyo unavyojifunza zaidi.  Ukitaka uondoke duniani katika siku yako ya mwisho ukiwa bora, basi kubali kujifunza badala ya kujiona unajua sana au unajua kila kitu.

Kiungo mpya wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi amejiunga na Yanga akiwa amechelewa baada ya suala lake la usajili kutokuwa limekamilika vizuri.

Hata wakati akiwa kambini Pemba, Tshishimbi alifanikiwa kucheza mechi moja tu ya kirafiki huku akiwa bado hajapata leseni ya kuanza kuitumikia Yanga katika michuano ambayo inatambulika.

Kibali chake kilipatikana hatua za mwisho kabisa Yanga haijaingia uwanjani kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, juzi. Katika mechi hiyo, Yanga ilipoteza kwa kufungwa mabao 5-4 ya mikwaju ya penalti baada ya dakika 90 za bila bao.

Wakati mechi hiyo inaisha hivyo, gumzo kubwa kwa mashabiki wa soka alikuwa Tshishimbi ambaye ndiye alikuwa anacheza katika mechi ya kwanza na kuonyesha kiwango cha juu na ikiwezekana kuwa kati ya wachezaji watatu walioonyesha kiwango cha juu zaidi katika mchezo huo.

Tshishimbi amefanya vizuri na mashabiki wote wa soka wanakubali. Wako ambao wanakataa kishabiki au kutokana na ushabiki wao dhidi ya Simba, hao ni watani unaweza ukawaachia wakaendelea na mambo yao.

Kama utakwenda katika uhalisia, Tshishimbi anaweza akawa somo, akakufunza kujua kwamba kuna mambo mengi wachezaji wetu wa Tanzania wamekuwa wakiyaacha yawaamulie badala ya wao kuamua wanataka nini.

Mfano, Tshishimbi angekuwa na kila sababu ya kusema ni mechi yake ya kwanza, hajazoeana na wenzake, hajawahi kucheza mechi kama ya Simba na Yanga na kadhalika.

Bado angeweza kusema hakuwa na uhakika na kibali chake hivyo akili yake yote hakuwekeza katika mechi na mengine mengi. Haikuwa hivyo, anacheza mechi ya kwanza na anakuwa staa wa mchezo.

Wako wachezaji kadhaa wamewahi kufanya kama yeye na wakawa nyota siku ya kwanza, baadaye wakaanguka. Asilimia 90 wamekuwa ni washambulizi ambao kazi yao inakuwa ni kuwapita mabeki na wanalishwa mipira na wachezaji wa viungo.

Tshishimbi ni kiungo, ushirikiano wake uwanjani unakuwa na watu wengi zaidi kuliko mshambulizi. Analazimika kukaba kuisaidia timu inapokuwa inashambuliwa na kila mmoja amekubali kuhusiana na uwezo wake ulivyo katika ukabaji na kutibua pasi za hatari.

Kama hivyo haitoshi, alikuwa sehemu ya mzunguko mpya wa timu, Waingereza wanaita ‘hub’. Mashambulizi ya Simba yaliishia kwake, mashambulizi ya Yanga yakaanzia kwake. Hakuna anayeweza kubisha katika hilo.

Kikubwa nilichojifunza kwa Tshishimbi, linapofikia suala la kazi hakuna suala la visingizio kwamba huyu ilikuwa vile au huyu iko vile, badala yake kinachotakiwa ni kazi kweli.

Tshishimbi ameonyesha kuwa mtu makini anapopewa nafasi, haifanyii utani anaitumia vizuri na kujenga imani. Jiulize kama Kocha George Lwandamina anaweza kutamani kumuweka benchi Tshishimbi katika mechi ijayo. Hata kama akitaka, utasikia kelele kwa kuwa watu wameona kazi.

Nataka nikuulize wewe unajua Juma Mahadhi kapewa nafasi ngapi Yanga hakuwahi kuzitumia vizuri? Au wachezaji wangapi unawajua walipewa nafasi Yanga na timu nyingine za Tanzania na hawakuwahi kufanya vizuri tena zaidi ya mara tatu, nne, tano au sita?

Nimezungumza mara nyingi kuhusiana na wachezaji wa Kitanzania kushindwa kujaribu nje kwa hofu ya ushindani au kuamua kubaki hapa nyumbani kwa kuwa wanashangiliwa sana au wakiamini maisha na kila kitu ni mazuri hapa zaidi.

Tshishimbi alijua Yanga kuna ushindani, amekuja. Tena utaona DR Congo inatoa wachezaji wengi zaidi kwa kuwa wanataka kufanikiwa na wanajua wanapofanya vizuri ndiyo mafanikio yenyewe.

Tshishimbi hawezi kuwa mchezaji mwenye kiwango cha juu kuliko wote uliowahi kuwaona, lakini inatosha wewe kujifunza kuwa kwa mtu makini anaweza kufanya yale ambayo wengi hawajatarajiwa na uliomuona alivyokuwa akitaka Yanga ishinde au akizuia isifungwe kwa kuwa anajua pale ndiyo kuna ‘unga’ wake, alifanya juu chini kuulinda.

Ninaamini kuna wachezaji wengi Watanzania wenye kiwango bora kama Tshishimbi. Bila ya kujali atakionyesha tena au la, lazima kujifunza kuweka mambo sawa au kuhakikisha kila nafasi unayopewa unaitumia na kuifanyia kazi kwa juhudi badala ya kuacha visingizio viwe nguzo yako ya baadaye. Kataa kabisa visingizio.




2 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic