August 5, 2017




Na Saleh Ally
KAMA utafuatilia kikubwa kinachoendelea katika mchezo wa soka kama mjadala basi ni suala la usajili wa mchezaji Neymar dos Santos kutoka Barcelona kwenda PSG ya Ufaransa.

Neymar ameamua kuondoka Barcelona kwa kuwaaga wenzake, baadhi akiwemo Lionel Messi wamemtakia kila la kheri katika maisha yake aendako.

Gumzo kuu ni usajili wa Neymar ni kitita cha pauni milioni 198 ambazo Barcelona watalipwa kutoka kwa PSG. Unaweza kuona ni kama jambo la kawaida ukizungumzia kwa maana ya hesabu ya kawaida ni Sh bilioni 580.

Nafikiri itakuwa rahisi kama nikikueleza kwa mfano mzuri. Kampuni ya SportPesa inatoa takribani Sh bilioni 1 kwa mwaka kwa klabu ya Simba na Yanga.

Hivyo kila mwaka inatumia Sh bilioni 2 kwa kila mwaka kwa klabu hizo kubwa. Hii ni mikataba mikubwa zaidi kwa klabu za Afrika Mashariki na SportPesa ndiye mdhamini anayetoa fedha nyingi zaidi kwa klabu moja pekee kwa kuwa anafikisha Sh bilioni 1 kwa mwaka kwa klabu moja.

Simba na Yanga, sasa zimeingia katika rekodi mpya kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kupata mdhamini anayetoa Sh bilioni kwa mwaka mmoja pekee.



Sasa unaweza kujiuliza, kama hiyo Sh bilioni 1 wakipewa Yanga na moja nyingine kwa Simba inaonekana ni rekodi. Maana yake wangepewa fedha anazonunuliwa Neymar kwa klabu zote mbili ingekuwa ni mkataba wa takribani miaka 24 kwa kila klabu. Nafikiri kidogo utakuwa umenielewa.

Lengo la kukumbusha hivyo ni kutaka kukuonyesha namna ambavyo hatua zimekuwa zikipigwa na wenzetu na walipofikia katika mpira kwa kuwa fedha zinaingia ni nyingi sana ndiyo maana wanaweza kufanya manunuzi makubwa kama hayo.

Mipango ya kufanya mambo kwa mpangilio, kuwaaminisha wadhamini kwamba mambo ni mazuri na watajitangaza, basi wanakuwa tayari kutoa fedha nyingi kujitangaza na klabu zinafanya kazi kwa kupata faida.

Usajili wa mchezaji mkubwa kama Neymar, utakaribisha wadhamini zaidi. Klabu itauza jezi zaidi, itaongeza uaminifu kwa wadhamini zaidi na pia mashabiki watataka kuona mechi zao kwa wingi. Hii ni fedha, hii ni mipango ya fedha, hii ndiyo akili.

Hapa nyumbani gumzo kuu ni Bi Hindu, mwanachama wa Simba ambaye anapambana kwa kushirikiana na wadhamini wa klabu ambao wanaelezwa kikatiba wao ndiyo wamiliki wa mali za Simba.

Wadhamini wa klabu, ndiyo wenye mali, jambo ambalo naona ni kosa. Wenye mali za klabu ni wanachama wote wa Simba, si wadhamini tu kama ambavyo imekuwa ikielezwa. Hao wadhamini wameteuliwa tu, vipi wawe wenye mali. Unaweza kuwa mwenye mali kwa kuteuliwa? Hiki ni kichekesho.
Unajaribu kujiuliza, kwa nini Bi Hindu anatumia nguvu kubwa yeye na wenzake? Jibu wana uchungu sana, “wameitoa Simba mbali!” Swali langu sasa baada ya kuitoa mbali, wameona hapa ndiyo mwisho, hawataki iende mbali zaidi?

Nimeona barua ya wadhamini kuzuia mkutano wa Simba, hiki ni kitu cha ajabu kabisa na huenda watu wanaogopa kuzungumzia kisa wataambiwa unazungumza kwa kuwa “umepozwa”, siwezi kuhofia upuuzi mdogo kama huo kwa kuwa nimepambana na kila aina ya “upuuzi” mkubwa na kushinda.

Mdhamini anaweza vipi kuwazuia wanachama kufanya mkutano ulio kwa mujibu wa katiba. Yeye anazungumzia katiba itumike ya Sunderland. Ajabu amesahau hii ni Simba, tena ajabu yeye mdhamini Hamisi Kilomoni anatambulika kuwa mdhamini kwa katiba ya Simba na si ile ya Sunderland! Kama ni katiba ya Sunderland maana yake hata yeye hayupo!

Wanaokataa mabadiliko ambao kigezo chao ni kuitoa Simba mbali, sasa wanataka Simba iendelee kuwa mbali au ilipo sasa? Kama wanaokutana ni wanachama, kwa nini wasiende kwenye mkutano na kuweka hoja zao mezani na zijadiliwe na kama zina mashiko ziwe njia ya kupita katika mabadiliko sahihi.

Naungana na Bi Hindu na wenzake katika nafasi hii. Kuwa kama ni mabadiliko, lazima watu waelimishwe, haraka ya nini. Sasa akina Bi Hindu na wenzake mbona wanapinga tena hayo mabadiliko kwa kuzuia mkutano ambao wangeweza kuzungumza kuwa kwanza elimu na watu waridhike ili kwenda kwenye mabadiliko.

Nani ambaye ana hofu na mabadiliko? Kuna kiongozi wa zamani wa Simba anafanya figisu? Anaona wenzake watafanya jambo kubwa au Simba ikibadilika anaona siku moja atarudi halafu hataambulia kitu?

Nani anakataa Simba inataka mabadiliko? Kama ndiyo njia sahihi ni wanachama kujadili na si watu kulalama kila siku katika vyombo vya habari. Mimi siamini Bi Hindu, mzee Kilomoni na wenzao waliojificha nyuma yao ndiyo wana ‘nundu’ za uchungu wa Simba.

Wanachotakiwa ni kutoa nafasi watu wayajadili mabadiliko hayo ili watu wapite njia sahihi na ikiwezekana siku moja, Simba nayo iuze mchezaji na kuwa gumzo kuu katika biashara na inachokiingiza na si wazee na wenzao wamegoma. Tumechoka.



1 COMMENTS:

  1. Umeongea facts tupu mkuu. Hao wazee wameshatoa kiasi gani kwa ajili ya usajili na maandalizi ya team???

    Wapeleke hizo hoja zao kwenye mkutano ili wana Msimbazi wakaamue huko

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic