August 29, 2017




Na Saleh Ally
TANGU Simba imeanza maandalizi ya msimu mpya wa 2017-18, nimekuwa nikisikia kauli moja ya kushangaza sana ikitolewa na mashabiki wanaoonyesha wao kazi yao ni kufuata upepo wa kila wanachosikia.

“Omog aondoke, atuachie timu yetu”. Kauli hii imekuwa ikitolewa mara kwa mara kwa mashabiki wanaohojiwa redioni au vyombo vingine vya habari.

Lakini kauli hiyo imetumika sana katika sehemu mashabiki wa soka wamekutana mitandaoni wakijadili mambo mbalimbali kuhusiana na mchezo wa soka hasa ikifikia suala la maandalizi ya msimu mpya.

Mashabiki walianza kuibuka na kauli hiyo wakiamini Kocha Joseph Omog wa Simba hana uwezo wa kuwa na kikosi kama cha Simba ya sasa, yaani hatakiweza.

Yaani inaonekana kikosi hicho kina wachezaji wengi sana nyota, hivyo hana uwezo badala yake angetafutwa kocha mwingine ambaye atakuwa na uwezo wa kukisaidia kufanya vema zaidi na ikiwezekana kutwaa mataji yote.

Walioanzisha mada hiyo siwajui, lakini mwanzo niliamini ni lile kundi la watu fulani ambao hupenda “kuonekana” wanajua mambo mbele ya jamii fulani, wakaamua kukizungumzia kitu fulani hata kisicho na msingi kwa wakati huo wakilazimisha kionekane ni cha msingi sana au wanapaswa kusikilizwa au kinatakiwa kujadiliwa.

Huenda ujuzi wa mambo, unatakiwa pia kujifunza jambo kama haulijui na inawezekana kukusaidia kufanya jambo jema zaidi kwa upande wako na ukilishadadia kama litafanikiwa basi mwisho likawa na msaada.

Jiulize wanaotaka Omog aondoke wakati wa mechi za kirafiki, kipindi ambacho anatengeneza timu akisubiri ligi. Wao walitaka kikosi chake kishinde mabao saba au nane wakati wa pre season, ikifika ligi iweje?

Wakati wa pre season ndiyo kipindi kocha anajaribu kila anachoweza. Suala la matokeo yalikuwaje linaweza kufuatia baada ya mambo matatu hadi manne kutoka kwa kocha na benchi lake la ufundi.

Unaweza ukaona kocha akapanga kikosi cha wachezaji 11, ndani yake wakawemo watano ambao anataka kuwajaribu au wale anaoamini watakuwa wakitokea benchi. Anaweza kupanga kikosi anaowategemea asilimia 60 akawaweka benchi kwa kuwa amewaamini.

Anaweza kumjaribu mchezaji anayecheza pembeni kucheza katikati kwa kuwa anataka kuona itakuwaje na anajua kipindi cha ligi hakuna nafasi ya kufanya hayo.

Sasa angalia mchezaji anayejaribiwa katika namba fulani wakati shabiki anayelazimisha matokeo ya kuvutia wakati wa maandalizi ili akamtambie mwenzake wa timu nyingine bila ya kujua plani ya kocha ni ipi!

Inawezekana kabisa Omog akawa si kocha mzuri sana na siku moja akafeli kama makocha wengine ambalo si jambo geni.


Lakini angalia ndiye kocha aliyechukua ubingwa akiwa na timu si Yanga au Simba alipoiongoza Azam FC kufanya hivyo ukiwa ni msimu wake wa kwanza kuja Tanzania.

Aliporejea kuinoa Simba, amekuwa kocha wa kwanza kuirejesha kwenye enzi za kubeba makombe ilipokuwa bingwa wa Kombe la Shirikisho, lakini ikawa imerejea katika michuano ya kimataifa baada ya misimu minne ya mambo ‘halijojo’.

Kigezo cha kusema Simba hii ni kubwa kuliko yeye inatokea wapi? Kwa nini au sababu zipi? Hawa mashabiki wanaoanzisha hilo wana nia ipi?

Simba haijasajili malaika, kuna siku itapata sare au kufungwa. Au ndiyo mada ya aondoke itaibuka tena? Na sasa baada ya Simba kuanza ligi kwa kuitwanga Ruvu Shooting kwa mabao 7-0 mada imekufa.

Kazi ya Omog ni kutengeneza mifumo na kulinda nidhamu ya kikosi chake kuwa na mwenendo sahihi kupitia umoja. Wanaocheza uwanjani ni wachezaji na kama wanafuata vizuri anachowafundisha, maana yake watafanya vizuri.

Sasa mjadala ni hivi? Kama Emmanuel Okwi kafunga mabao manne mechi moja, wengine pia wamefunga na sifa zinawaendea wao, siku wakishindwa kufunga ni kosa la Omog?


Nafanya hivi makusudi kuufufua huu mjadala wa wale waliouanzisha na kupotea baada ya ushindi huo wa kikosi cha Omog wa mabao saba, wataibuka ikitokea sare au Simba kupoteza mechi moja? 

2 COMMENTS:

  1. Mkuu wewe ulimpa siku 29..tupe mrejesho

    ReplyDelete
  2. Ukinyonga huo.Wewe pia ulikuwa mkumbo huo huo.Sasa umekuwa bendera mfuata upepo. Kocha hafundishi kufunga ball anafundisha mfumo.Kazi ya kufunga ni ya wachezaji.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic