September 11, 2017

Na Saleh Ally, aliyekuwa Manchester
JUHUDI za kumfanyia mahojiano Dwight Yorke zilikwama jijini Manchester baada ya mchezaji huyo kuhofia kuulizwa maswali ambayo yamekuwa yakimkwaza mara kwa mara.

Yorke alikataa kuzungumza hata na runinga ya Man United, lakini baadaye akafanya mazungumzo nayo.
 Kwa kuwa gazeti hili lilikuwa kati ya vyombo vitatu vilivyokuwa ndani ya eneo ambalo walikuwa wanapatikana wachezaji, baadaye Yorke raia wa Trinidad and Tobago, alikuja mwenyewe na kusema amekubaliana na suala la mahojiano lakini angependa kupata maswali yanayohusu uwanjani zaidi.

Baada ya awali kuwa amekataa mahojiano, nilijaribu kufuatilia kwa baadhi ya maofisa wa Manchester United ambao walinieleza mambo kadhaa yakiwemo mawili ambayo kamwe hapendi kuyasikia.

Moja ni ile ishu ya mtoto aliyewahi kumkataa baada ya kuzaa na mwanamitindo Katie Price, nilielezwa mtoto wao ni mpofu wa macho.

Lakini kuna taarifa, Yorke aliwahi kuzuiwa kuingia Marekani baada ya kuonekana katika pasi yake ya kusafiria kuna mhuri wa Iran, yaani aliwahi kusafiri kwenda nchini Iran.

Nami sikuthubutu kumuuliza kwa kuwa sikuwa kati ya niliyokuwa nimelenga kutaka kupata kitu kutoka kwake, badala yake nilitaka kujua alicholenga baada ya maisha yake nje ya Manchester United na kile anachokikumbuka zaidi ndani ya klabu hiyo.

 “Kikubwa ni kikosi cha Manchester United ambacho kwa muda niliocheza tangu 1998 hadi 2002, ninaweza kusema yalikuwa ni mafanikio ya juu kabisa kuliko sehemu nyingine yoyote.

 “Mwaka 1999, ndio ambao hautasahaulika katika maisha yangu tulipotwaa makombe matatu ya Kombe la FA, Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kikosi chetu kilikuwa bora kila idara na wachezaji wote walikuwa ni wale wanaotaka kushinda na si vinginevyo. 

“Tulikuwa tunasikilizana sana na hii ilinipa hamu ya kuwa kocha baadaye. Maana nilicheza Aston Villa kwa miaka mingi zaidi, takriban kumi. Lakini sikufikia robo ya mafanikio niliyopata Manchester United na unaona leo wapo waliosahau kama nilicheza Aston Villa,” anasema Yorke aliyekuwa pacha wa Andy Cole wakati huo wakiitikisa dunia kwa kufunga mabao muhimu kwa Manchester United.

 “Nilishaanza mafunzo ya ukocha, ninaendelea kujifunza zaidi. Unajua siwezi kuishi nje ya ukocha kwa kuwa hata sasa naona akili yangu inafanya kazi vizuri na ninaweza kucheza hata ligi lakini shida ni mwili sababu ya umri.

“Naupenda sana mpira, siwezi kuishi nje yake. Hivyo nafasi yangu ya kubaki ndani ya mpira ni kuwa kocha,” anasisitiza.

Katika wachezaji walio katika kikosi cha wakongwe wa Manchester United, Yorke ndiye anaonekana kuwa fiti zaidi na tayari katika umri wa zaidi ya miaka 40, maana sasa ana miaka 45, aliweka rekodi ya kumaliza London Marathon ambayo ni zaidi ya Kilomita 40 na alitumia muda wa saa 3:32, hii ilikuwa mwaka 2011.

 Kwao Trinidad and Tobago, wamejenga uwanja na kuupa jina lake ingawa unatumika kwa mchezo wa kriketi ambao yeye pia ni shabiki mkubwa wa mchezo huo na kaka yake ni mmoja wa wachezaji nyota wa timu ya taifa ya mchezo huo.

Yorke anasema anaamini alijitahidi kufanya makubwa akiwa Man United, anajua amesaidia katika nchi yake lakini bado anataka kufanya zaidi akiwa nje ya uwanja.

“Baada ya kumaliza kucheza, haina maana nikae kando tu. Nataka kusaidia mpira nchini kwangu na kote nilikopita.”

Yorke anasema pamoja na kufanya vizuri Manchester United, lakini ana mapenzi makubwa na Aston Villa kwa kuwa ilimlea kisoka na kumfanya atafutwe na timu kubwa.

Wakati Manchester United inabeba makombe matatu katika mwaka wake wa kihistoria wa 1999, yeye ndiye alikuwa mfungaji bora wa kikosi hicho akifunga mabao zaidi ya 25.



Hali hiyo imefanya Klabu ya Manchester United kuhifadhi viatu vyake jozi moja aliyovaa mwaka huo kama sehemu ya kumbukumbu ya mchango wake katika klabu hiyo.

Kiatu hicho kimehifadhiwa kwenye makumbusho ya Manchester United yaliyo katika Uwanja wa Old Trafford na watu hulipa kuingia uwanjani hapo kushuhudia vitu mbalimbali vikiwemo viatu vya nyota huyo wa zamani wa Mashetani hao Wekundu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic