September 9, 2017


VIPIGO viwili kutoka kwa Stoke City na Liverpool vinaiweka Arsenal mahali pagumu ambako zipo sababu kibao zinazowafanya wasiweze kutwaa taji la Ligi Kuu England.

Huu ni mwaka wa 13 sasa Arsenal haijatwaa tena taji la Ligi ya England ambayo ni maarufu kama Premier Leauge, na mbaya zaidi msimu huu wa 2017/18, tayari imepoteza mechi mbili kati ya tatu za kwanza.

Arsenal chini ya Kocha Arsene Wenger ilianza msimu huu kwa kuifunga Leicester City mabao 4-3, ushindi ambao ulipondwa kutokana na udhaifu wa timu kuruhusu mabao mengi katika mechi moja.

Ikaja kufungwa bao 1-0 na Stoke City kabla ya kubugizwa mabao 4-0 na Liverpool, hadi hapo tayari picha ya Arsenal kwa msimu huu imeshaonekana.

Premier League ni ligi inayotoa kiasi kikubwa cha fedha za zawadi kuliko zote England, lakini inaonekana kama Wenger hana mpango na fedha hizo badala yake zile zinazoingia kwa mauzo ya wachezaji.

Miaka 13 ni mingi na bado mashabiki wanaamini muda wowote watatwaa tena ubingwa lakini kwa hadi sasa kuna dalili za Arsenal kushindwa tena kutwaa ubingwa kutokana na sababu hizi hapa chini;

TATIZO LA BEKI WA KATI
Kutokana na kutokuwa na chaguo, Arsenal ilianza mechi mbili za kwanza ikimtumia beki wa kushoto kama beki wa kati tena kwa kutumia mfumo wa mabeki watatu nyuma. Wachezaji wawili walichezeshwa katika nafasi isiyo yao kiuhalisia na Wenger hakuliona hilo. Matokeo yake timu ikaruhusu mabao manne katika mechi mbili tu.
Ni kiburi tu, lakini Wenger alijua kabisa Laurent Koscielny ana adhabu, anajua Mustafi atakuwa amerejea kutoka timu ya taifa na anajua Rob Holding hayupo tayari kuanza mechi za ushindani.

Badala yake, akadharau vyote hivyo na kukaidi kusajili beki mpya wa kati. Hata kama mabeki wote hao watakuwa vizuri yaani kina Koscielny, bado Arsenal ilihitaji beki mpya wa kati. Usisahau kwamba Koscielny ana miaka 31, huyu nguvu zake zinaelekea ukingoni.

Soka ni mchezo wa ajabu sana, kwani hakuna muda wa kusubiri uwezo wa mchezaji anayeanza kikosi cha kwanza, Shkodran Mustafi haonekani kama mtu anayekidhi matakwa ya mashabiki, yupo taratibu mno uwanjani na anacheza rafu za hovyo. Arsenal imekosa beki wa kati wa nguvu ambaye anaweza kupambana timu isifungwe kirahisi.

KIBURI
Wenger kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita alibadili mfumo na kucheza 3-4-3, lakini katika mechi zake kimebaki kuwa kilekile na hajabadilika. Kwa taarifa yako tu, Arsenal imewahi kushinda mechi mbili za kwanza za ligi miaka saba iliyopita, sababu ni kwamba Wenger huwa anashindwa kufanya maandalizi mazuri katika ‘pre season’.

Mbinu zake zote zimekuwa zilezile na ni nyepesi kusomwa na timu pinzani kiasi kwamba hata timu ya kuokoteza ikiamua inaweza kutoka sare na Arsenal, Wenger amekuwa mzito kubadilika kwa miaka 10 sasa.

Tazama katika kipigo cha Stoke, Wenger alibaki akilaumu waamuzi badala ya wachezaji wake kushindwa kujituma. Mara nyingi Wenger amekuwa hatazami kuhusu upungufu wa kikosi chake, badala yake amekuwa akitazama shutuma dhidi yake na jinsi ya kuzijibu.

Sasa Wenger mwenye umri wa miaka 67 ameongeza mkataba wa miaka miwili, hii ina maana kwamba mashabiki wa Arsenal wategemee miaka mingine miwili ya kulikosa taji la Premier League.

BORA LIENDE, TIMU HAINA KIONGOZI
Huko nyuma Arsenal ilikuwa na wachezaji viongozi ambao waliweza kutoa tamko ndani ya uwanja na wakaogopeka, lakini sasa hakuna mtu huyo na kila mchezaji anajiona ‘faza’ uwanjani anafanya atakalo.

Fikiria mchezaji kama Mesut Ozil au Alexis Sanchez kama wangethubutu kuleta kiburi, dharau na kutojituma mbele ya viongozi kama Patrick Vieira au Tony Adams, hapana wangejua nini kingewapata.

Sasa uwezo wa kujituma wa wachezaji upo chini na ndani ya uwanja inaonekana hakuna mtu anayesikilizwa kwa tamko la karipio na wote wapo wa aina moja, na hili lilithibitika katika mchezo dhidi ya Stoke City.

Kila timu sasa inajua kwamba, kama unataka ushindi dhidi ya Arsenal we wachezee kindava tena kwa nguvu kwelikweli mabeki wa Arsenal na watalegea wenyewe na ushindi utapatikana, yaani ni wepesi wa kukata tamaa. Ndicho walichofanya Stoke City.

Mchezaji kiongozi anapokuwepo uwanjani, anakuwa mwepesi wa kuamuru aina ya uchezaji kutoka busara iliyopitiliza hadi nguvu kubwa hapa kocha hawezi kutoa uamuzi kwani muda wake ni wakati wa mapumziko.

SANTI CAZORLA YUPO NJE, INACHUKULIWA POA TU
Katika misimu mitatu sasa, Santi Cazorla amekosa mechi 79 kutokana na majeraha. Arsenal imekosa kitu fulani muhimu kutoka kwa kiungo huyu raia wa Hispania na kikosini hakuna mtu wa kuziba nafasi yake.

Cazorla ni kiungo mbunifu anayeweza kuitoa timu katika hali ya kuzidiwa akatuliza mambo na kuanzisha upya mashambulizi, au kutafuta namna nyingine ya kuipenya ngome ya adui.

Huyu ni mtaalamu wa kutengeneza nafasi kuanzia katikati ya uwanja, anawaunga viungo na washambuliaji pia anawaunga viungo na mabeki, lakini sasa Arsenal haina mtu wa aina yake na timu haitengenezi nafasi.
Wenger bado anabahatisha kuhusu afya ya Cazorla, na bado anaamini ipo siku kiungo huyo atakuwa vizuri na atafanya naye kazi ipasavyo, ingekuwa kocha mwingine tayari angekuwa ametafuta mbadala wake na kumsajili.

FEDHA ZA MAN CITY, UNITED
Msimu uliopita Arsenal ilimaliza ligi ikiwa nafasi mbovu chini ya Wenger na wengi wakadhani hilo lingekuwa fundisho kwa kocha huyo kuelekea msimu huu wa ligi. Badala yake, Arsenal imefanya kinyume kwani imesajili wachezaji wawili tu, Sead Kolasinac kutoka Schalke 04 na Alexandre Lacazette kutoka Lyon, tena hapo zimetumika pauni milioni 47.7 tu kwa Lacazette kwani Kolasinac amesajiliwa kama mchezaji huru.

Wapinzani wa Arsenal, Manchester City wao wametumia jumla ya pauni milioni 219.87 kusajili wachezaji saba huku Manchester United wakitumia pauni milioni 147.96 kusajili wachezaji watatu.

Klabu iliyomaliza nafasi ya tano msimu uliopita ilipaswa kujitathimini na kutumia fedha zaidi katika kujenga kikosi chake badala ya kubania fedha na kusajili wachezaji wa bei rahisi.
Matokeo ya kutumia fedha nyingi yameanza kuonekana kwa Man United kwani katika mechi tatu za kwanza ina pointi tisa na mabao kumi, haijafungwa hata bao moja.

OZIL, SANCHEZ
Kuendelea kulazimisha kuwatumia Alexis Sanchez na Mesut Ozil katika kikosi cha kwanza na kuwategemea kwa asilimia 100 ni kosa lingine linalotumiwa na Wenger kwani wachezaji hao hawana moyo wa kupambana sasa.
Wenger lazima aelewe kuwa, mioyo ya Sanchez na Ozil haipo Emirates, wanawaza nje ya Arsenal na bila shaka wote wanasubiri miezi minne tu ufike muda wa usajili mwingine ili waanzishe chokochoko za kuondoka tena.
Taratibu Wenger anapaswa kuwaamini wachezaji wengine na kuhesabu kama Sanchez na Ozil wameshaondoka ili kutuliza kichwa chake kwa kuwaamini watu wasioaminika.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic