September 15, 2017


Na Saleh Ally
MASHABIKI wengi ninaoamini watakuwa ni wa Yanga walionyesha kukerwa moja kwa moja na Msemaji wa Simba Haji Sunday Manara alipoandika maneno kwenye mtandao wa kijamii akiwadhihaki Yanga.

Inaonekana Manara alilenga kufanya utani, kwamba baada ya Serikali ya Tanzania kulitwaa shamba lenye heka 714 lililokuwa linamilikiwa na Mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji.

Shamba hilo katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, limechukuliwa na serikali kwa madai halikuwa likiendelezwa.

Wakati linachukuliwa, Manji alikuwa mahabusu kwenye gereza la Keko ambako alikuwa kutokana na kukabiriwa na kesi ya uhaini ambayo jana ilifutwa baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuwasilisha mahakamani kuwa hakuwa na nia ya kutaka kuendelea kumshitaki.
Wakati Manji akiwa ndani, shamba lake limetaifishwa. Nataka kwanza kukumbusha kuwa Manji ni mwanamichezo, kuwa katika matatizo hakumvui uanamichezo wake.

Manji ni mwanadamu, kuwa katika matatizo hakumvui uanadamu wake. Hivyo ni jambo jema kwa wanamichezo na wanadamu kuyachukulia yanayomtokea ni kama matatizo na wala si jambo la kufanyia dhihaka wala utrani hata kidogo.

Hasira za mashabiki hao ambao ninaamini ni wa Yanga kwa Manara ni baada yay eye kuanza kuwadhihaki kwamba baada ya shamba kupokonywa basi ndiyo zile mwisho za kuwa na uwanja wa kisasa kama ambavyo ilikuwa inaelezwa.

Kukumbusha msomaji, shamba hilo la Manji, ndiyo alilolitoa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wakati akiwa katika mchakato wa kuwekeza kwa miaka 10 ndani ya Yanga kupitia kampuni yake ya Yanga Yetu Ltd.

Zoezi la uwekezaji lilionekana kukwama ikiwa ni tayari alikuwa ametoa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi. Hapo nafikiri Manara aliona ni sehemu ya utani.
Ingekuwa kawaida, sidhani kama kungekuwa kuna jambo la ajabu kwa kuwa tunajua Yanga na Simba ni watani na wana haki ya kutaniana. Lakini kwa kipindi ambacho Yanga wanaona wamepoteza tena mwenyekiti wao wa zamani akipoteza na yuko katika matatizo, Manara hakuwa sahihi hata kidogo.

Huenda akaona yuko sahihi, akaona alichokifanya hakikuwa na shida lakini ukweli halisi lilikuwa ni jambo linaloonyesha kuuweka pembeni uungwana na hasa kwa mwanadamu asiyeumizwa na matatizo ya wenzake.

Wakati Manara akisumbuliwa na matatizo ya macho, unakumbuka Wana Yanga hawakufanya utani kumuambia maneno mabaya ambayo wangeweza kusingizia ulikuwa ni utani. Badala yake walijichangisha wakiongozwa na Jerry Muro na wote wakaenda kumjulia hali na kumpa mchango huo umsaidia kwa ajili ya matibabu.

Ninaamini wakiwa pale nyumbani kwake, utani uliendelea kama kawaida lakini tunajua sote kilichowapeleka ilikuwa ni kwenda kumsaidia na kuhakikisha anaondokana na tatizo lililokuwa likimkabiri katika kipindi hicho.

Uungwana waliouonyesha Wanayanga hao, huenda ni nafasi nzuri ya kumkumbusha Manara kwamba utani sawa lakini ni vizuri kuingia katika maumivu ya walio karibu yako kupima kinachowakabiri badala ya kuwasakama kwa maneno ambayo yanaweza kuwaumiza.

Siku chache zilizopita nilimpa moyo Manara kutokana na maneno ya hovyo kutoka kwa mashabiki wa Yanga wasiojitambua ambao walizungumza maneno ya kushusha na kuudhalilisha uanadamu wa Manara. Nilipinga na kusema huo haukuwa utani badala yake ni ghadhabu na chuki na kamwe si sahihi kumfanyia vile Manara.

Leo kweupe, nampinga MAnara, pia ninamkumbusha kwamba sisi ni wanadamu, kesho yako wala kitakachotokea hauikijui. Hivyo si sahihi kuchanganya matatizo na ukweli hasa katika jambo ambalo unaona linahusisha maumivu ya kiuanadamu.

Wale ambao walikasirishwa na Mara, pia nawashauri kwamba vizuri kumueleza kwa kufuata misingi ya utu. Kutukana pekee, hakuwezi kuwa njia ya kuwasilisha hoja sahihi. Wako waliomfikishia hoja kwa maneno makali lakini yaliyofuata misingi. Hivyo ni vizuri kumfikishia ujumbe bila ya kutukana na itawezekana. Waungwana, sisi ni wanadamu, tusipooneana huruma, tunapoteza sifa ya utu.








0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic