UKITAKA uishi huku unapiga hatua zenye mwendo mzuri au ulio
sahihi, ni vizuri kama utakubali kila siku unayopata nafasi ya kuishi lazima
ujifunze kitu. Nasema kila siku unayopata nafasi kwa kuwa mimi na wewe ni
wanadamu, kila siku moja au dakika tunayoishi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi
Mungu kwa kuwa yeye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho katika kila kitu. Hivyo, ni
vizuri kuipa thamani kubwa siku au muda unaopewa kuendelea kuwepo duniani.
Kujifunza ni moja ya thamani hiyo kuliko kutaka kuonekana unajua kitu. Huenda
huo ukawa ni ujumbe niliopenda nianze nao katika Metodo ingawa nilicholenga
kuzungumzia ni suala hilohilo la kujifunza. Natamani sana kuona Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Mako cha Tanzania (Tafca) wanaamka na kukumbuka kwa kuwa kuna
jambo huwa wanalisahau kwa kiasi kikubwa na wameendelea kulisahau kwa siku
nyingi. Suala la kuwafundisha walimu wa makipa kwa ajili ya maendeleo ya soka
nchini. Kila kukicha wenzetu ambao kwao mpira umeendelea wanazipa thamani siku
wanazoishi kwa kujifunza na kujiimarisha. Katika kozi nyingi za mchezo wa soka
zinazotolewa hasa nyumbani Tanzania, makocha wamekuwa wakipewa kozi za pamoja bila
ya kuangalia wao watafundisha upande upi.
Lakini nchi nyingi za Ulaya, Amerika
Kusini, Asia na kwingineko ambako mpira umepiga hatua, kuna kozi maalum tena
hatua kwa hatua kwa ajili ya makocha wa makipa. Kuwafundisha makochawa makipa, maana yake ni kuwaandaa kwa ajili ya kuzalisha
makipa bora ambao watakuwa na kiwango sahihi kwa ajili ya kuzitumikia timu zao.
Kuwafundisha makocha “jenero”, si jambo baya. Lakini kocha ambaye anaweza kuwa
na faida kidogo kwa makipa ni yule aliyekuwa golikipa halafu akafundishwa kozi
ya ukocha wa kawaida. Lakini bado anaweza asiwe msaada sana kwa makipa wake kwa
kuwa naye atakuwa hayajui mambo mengi mapya ambayo yanatokea katika mpira kwa
sasa. Kadiri siku zinavyosonga mbele, mchezo wa soka unazidi kupiga hatua ya
maendeleo. Wafungaji au washambulizi na viungo washambulizi wamekuwa
wakifundishwa kila namna ya mbinu kuhakikisha wanakuwa bora kuzisaidia timu
zao.
Kuzisaidia timu zao ni kufunga mabao, kufunga ni lazima
wategue mtego wa safu za ulinzi za timu pinzani na kufunga. Ili wafanye hivyo
ni lazima mpira umpite kipa ambaye ndiye mchezaji wa mwisho. Kama ni hivyo,
kipa ameandaliwa vipi? Kwa nyumbani Tanzania, makipa wanaendelea kubaki na
mbinu za mwaka 47 kutokana na kutokuwa na mafunzo yanayoendana na wakati ili
kuwafanya wawe washindani na kwenda na muda sahihi. Kama mshambuliaji na kiungo
mshambuliaji wanapewa mbinu mpya za kumshinda kipa. Tujiulize, kipa anapewa
mbinu gani za kisasa kupambana na zile za kisasa za wapinzani wake? Hakuna
anayeweza kukataa kuwa makipa wengi sasa wanadaka kwa kutumia vipaji vyao kwa
kuwa hata walimu wanaowafundisha
nao wanatumia vipaji vyao pia! Hatuwezi kusema wana mbinu
mpya wakati hatujaona mafunzo wanayopewa kuboresha mbinu hizo!
Kama ni hivyo,
vipi tunaweza kuufanya mpira wetu kukamilika kimafunzo na kuwa na ushindani
uliokamilika timu zetu zinapocheza tukianzia kwa kipa namba moja, mabeki,
viungo hadi washambulizi? Makipa wana mafunzo yao, wanaanza kufundishwa walimu
nao wanawafundisha makipa. TFF inapaswa kuliangalia hili ili kuwawezesha makipa
tulionao kwenda na wakati na kuachana na kutegemea vipaji. Inawezekana sasa
tukaliona halina umuhimu, ushauri wangu vizuri
kushituka mapema kabla hatujaachwa katika kiwango cha kutisha, siku
tunashituka, tutajikuta tupo katika dunia ya peke yetu!
MSIMU wa Ligi Kuu Bara tayari umeanza kwa timu 16 katika
kampeni ya kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa msimu huu mbele ya mabingwa watetezi
Yanga ambao wamefanikiwa kuchukua ubingwa huo mara tatu mfululizo. Tangu msimu
wa 2014/15, 2015/16 na 2016/17, Yanga wamekuwa mabingwa kitu ambacho ni cha
kupongezwa kutokana na nguvu kubwa waliyoitumia mpaka kuweza kutimiza suala
hilo. Hii sasa inaonyesha kuwa, msimu huu Yanga watakuwa na wakati mgumu katika
mechi zake kwa kuwa ni bingwa mtetezi ambaye kila timu itakayokuwa inakutana
nayo itataka kuhakikisha inafanikiwa kuifunga sasa lazima wajipange kwa kukabiliana na hali zote. Tayari tumeshuhudia
katika mechi za kwanza ambazo timu zote zimecheza matokeo yao tumeyaona na inaonyesha
wazi jinsi timu zilivyoweza kujipanga kufanya vizuri kwa kuwa kila moja
inaonekana kuwa moto hakuna ambayo inadharaulika. Licha ya ligi kusimama
kupisha mchezo wa timu ya taifa lakini tumeshuhudia kwenye mechi zilizopigwa
juzi Jumamosi na jana Jumapili namna zilivyokuwa ngumu kutokana na matokeo
yaliyopatikana kupitia michezo hiyo licha ya kwamba baadhi yao wana vikosi bora
walivyovisajili kwa gharama kubwa. Tumeshuhudia Simba ikianza vizuri katika
ligi ya msimu huu kwa ushindi mkubwa wa
mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting hii ilikuwa kwenye mchezo wao wa kwanza kabisa
uliopigwa wiki mbili zilizopita na juzi Jumamosi wakatoa suluhu na Azam FC
kwenye Dimba la Chamazi Complex.
Ukiangalia hapo unapata picha halisi ya jinsi ushindani
ulivyo mkubwa kwa kila timu kuwa na kiu ya kutaka kufanya vizuri kutokana na
maandalizi waliyofanya kwenye pre-seasons. Timu kama Singida United imesajili
wachezaji wengi wapya na wenye uzoefu na ligi lakini yenyewe ilianza kwa
kupoteza ugenini dhidi ya Mwadui FC, hivyo utaona namna ambavyo ligi ilivyo
ngumu haijalishi umesajili kwa fedha kiasi gani lakini uwanjani kila mtu
anaona. Azam FC hawakupewa kufanya vizuri hasa kwenye mchezo dhidi ya Simba na
Lipuli ilipocheza na Yanga lakini funzo ni kwamba matokeo ya mechi hizo
yalikuwaje na kwa nini yawe hivyo?
Jibu lake litakuwa ni kwamba kila timu
ilifanya maandalizi ya maana kabla ya kuanza kwa ligi hivyo lolote linaweza
kutokea kwa kuwa hakuna mwenye uhakika wa kuanza na kumaliza vyema ligi. Ukweli
ligi ni ngumu lazima kila timu ijitume ili kuweza kufikia malengo ingawa bado
mapema lakini picha halisi ya ushindani inaonekana kwa timu zote kuonyesha
zimejipanga vizuri kwani hakuna mwenye uhakika wa kubaki. Mwisho niwaombe
waamuzi kuzingatia kanuni 17 za mchezo wa soka ili bingwa apatikane kwa uhalali
maana zimeshaanza kelele kwa baadhi yao kuonekana tatizo kutokana na maamuzi
ambayo wamekuwa wakitoa katika baadhi ya mechi. Tusingependa kusikia tena
kelele mara kwa mara kwa kitu ambacho mlikaa darasani na mkakisomea wenyewe,
chezesheni kwa haki na msitishwe na makelele ya makocha na wachezaji bali
fuateni kanuni zilizowekwa.
JUZI Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es
Salaam, tulishuhudia mchezo wa Ligi Kuu Bara uliozikutanisha wenyeji Azam dhidi
ya Simba. Matokeo ya mchezo huo yalikuwa suluhu. Awali kabla ya mchezo huo,
hofu ilikuwa kubwa kwa mashabiki juu ya usalama wao, lakini Jeshi la Polisi
Tanzania likawahakikisha kutakuwa na usalama huku likitoa angalizo kwa
mashabiki kwamba wawe wastaarabu. Mashabiki walitahadharishwa mapema kwamba
wanatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa, lakini pia kwa wale watakaofika
uwanjani na kukuta uwanja umejaa, basi warudi nyumbani na kushuhudia mechi
kupitia luninga. Kikubwa ambacho naweza kuwapongeza mashabiki, walifuata kile
ambacho walitahadharishwa mapema, lakini pia jeshi la polisi lilikuwa
limejipanga tayari kuweka ulinzi wa kutosha kuhakikisha hakuna uvunjifu wa
amani. Mwanzo mpaka mwisho wa mchezo, hakukuwa na vurugu zile ambazo wengi
walikuwa na hofu nazo jambo ambalo linadhihirisha kwamba mashabiki wa soka hapa
nyumbani wamestaarabika na kuondoa ile dhana inayoonyesha kwamba mchezo wa soka
ni wa wahuni. Kumekuwa na dhana hiyo kutokana na kwamba, mara kadhaa kumekuwa
na vurugu viwanjani ambazo chanzo chake ni mashabiki, lakini kilichotokea juzi
pale Azam Complex, imeondoa dhana hiyo mbaya. Rai yangu ni kwamba, amani kama
hiyo iendelee kutokea viwanjani kote ili kuepusha uharibifu wa mali viwanjani
kama ilivyotokea Uwanja wa Taifa katika mechi kadhaa kama ile ya Yanga dhidi ya
TP Mazembe na ya msimu uliopita iliyowakutanisha Simba na Yanga ambayo
ilisababisha uwanja huo kufungwa kutokana na mashabiki kung’oa viti. Kutokana
na vurugu kutawala sana viwanjani, siku za nyuma Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), lilishindwa kutoa ruhusa kwa Azam FC kuutumia uwanja
wao huo kwa mechi za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga. TFF ilikuwa haina imani
na usalama wa uwanja huo kwa jinsi ulivyo, kwanza unaingiza idadi ndogo ya
mashabiki ambayo ni 7000 tofauti na Uhuru unaoingia zaidi ya mashabiki 23,000
na ule wa Taifa unaochukua watazamaji 60,000.
Mashabiki wa Simba na Yanga
wanapocheza na Azam wanakuwa wengi, hivyo TFF ilikuwa ikihofia kuzuka kwa
vurugu kama itatokea mashabiki watakuwa wengi tofauti na uwezo wa uwanja huo.
Lakini baada ya jeshi la polisi kujiridhisha juu ya kujipanga kwao kulinda
usalama na kuwadhibiti mashabiki, tukaona TFF ikiruhusu kwa mara ya kwanza
kutumika na mpaka dakika tisini zinamalizika, Azam ikashindwa kufungana na
Simba. Baada ya mchezo huo kumalizika kwa amani, tunatarajia kuona tena Yanga
wakienda hapo na mambo yakiwa sawa katika suala zima la usalama kama ilivyo kwa
wenzao wa Simba.
Mwisho kabisa niwaambie Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar na Mwadui
FC ambao nao walikuwa wanataka kuona mechi zao dhidi ya Simba na Yanga
zinachezwa kwenye viwanja vyao, kuvifanyia marekebisho ili kuipata haki yao.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred, viwanja vya timu hizo
ambavyo ni Mabatini, Manungu Complex na Mwadui Complex havina hadhi ya
kuchezewa mechi hizo kutokana na kutokuwa na majukwaa ya kutosha. Kama kweli
viwanja hivyo vinataka kupata haki kama waliyoipata Azam FC, hawana budi
kufuata kile TFF inavyotaka kwani tayari wameambiwa juu ya kuweka majukwaa
kwenye viwanja vyao ili hata zile mechi zingine wanazocheza hapo ziweze
kuchezwa kwani wasipofanya hivyo, kuna hatari ya kufungiwa viwanja vyao.
0 COMMENTS:
Post a Comment