MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi,
juzi Jumamosi alimshuhudia mshambuliaji mwenzake wa klabu hiyo, Mghana,
Nicholas Gyan katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC na akasisitiza
jamaa huyo ni bonge la straika, sema tu watu hawajamshtukia.
Okwi alikuwa
jukwaani katika mchezo huo na alishuhudia kila kitu kilichotokea.
Mganda huyo
aliyetokea katika kikosi cha Ebusua Dwarfs, alishawahi kucheza na Gyan katika
mchezo wa kirafiki kwenye Simba Day mwezi uliopita dhidi ya Rayon Sports ya
Rwanda ambayo Simba ilishinda bao 1-0, halafu Mghana huyo akaondoka kumalizana
na timu yake, tangu hapo hawakuwahi kukutana tena na Okwi, mpaka Mganda huyo alipomuona juzi,
yeye akiwa jukwaani.
Okwi ambaye
hakuitumikia Simba katika mchezo huo kutokana na kuchelewa kurudi nchini
akitokea kwao Uganda alipokuwa ameenda kAwa ajili ya kuitumikia timu yake ya
taifa katika mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2018
dhidi ya Misri, alisema anaamini akipangwa pamoja na Mghana huyo, safu ya
ushambuliaji ya Wekundu haitakamatika.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Okwi
alisema kuwa Gyan alionyesha uwezo mkubwa katika mchezo huo pamoja na John
Bocco lakini walishindwa kufanya vizuri kutokana na kukamiwa na mabeki wa Azam.
“Gyan ni mchezaji mzuri, kuna vitu anavyo ambavyo naamini kuwa siku tukipangwa
naye pamoja basi tutafanya makubwa kama yale tuliyofanya dhidi ya Ruvu Shooting
tulipokuwa na Juma Liuzio.
“Lakini pia washambuliaji wengine katika kikosi
chetu ni wazuri sana,” alisema Okwi. Akizungumzia kuhusiana na kuchelewa kwake
kurudi nchini kwa ajili ya kuitumikia
timu hiyo katika mchezo huo uliomalizika bila ya kufungana,
Okwi alisema: “Kilichonichelewesha kujiunga na timu yangu mapema ni kutokana na
matatizo ya kifamilia lakini pia hali ya usafiri.
“Baada mechi yetu na Misri
nilitakiwa kuja moja kwa moja Dar es Salaam lakini nilipata matatizo ya kifamilia
ikanibidi niende kwanza nyumbani Uganda kisha ndiyo nije Dar.
“Hata hivyo,
baada ya kuyatatua nilitakiwa nifike jana alfajiri (juzi) lakini kutokana na
kubadilishwa kwa ratiba ya ndege niliyokuwa nije nayo, (Kenya Airways),
nilijikuta nikichelewa kufika Dar jambo ambalo lilimfanya kocha pia ashindwe
kunitumia katika mechi hiyo.
“Lakini pamoja na hali hiyo napenda kuwapongeza
wachezaji wenzangu wote wa Simba kwa kazi kubwa waliyoifanya kwani mechi hiyo
ilikuwa ni ngumu sana kwani Azam walipania sana,” alisema Okwi. Okwi kwa sasa
ndiye anayeongoza kwa kufumania nyavu katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu
msimu huu akiwa na mabao manne ambayo yote kwa pamoja waliyafunga dhidi ya Ruvu
Shooting ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 7-0.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment