September 18, 2017


Baada ya Yanga kuanza Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kusuasua, Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja ameibuka na kufunguka juu ya hatma ya kikosi hicho pamoja na chao katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo.

Juzi Jumamosi, Yanga iliilazimisha Majimaji sare ya bao 1-1 katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea na kujikusanyia pointi tano katika mechi tatu za mwanzo zenye jumla ya pointi tisa.

Katika msimu uliopita ambao Yanga ilikuwa bingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Simba huku zote zikiwa na pointi sawa 68, timu hiyo ndani ya mechi tatu za mwanzo ilikuwa tayari imejikusanyia pointi saba.

Akizungumza kuhusiana na matokeo mabaya wanayoyapata wapinzani wao wa jadi Yanga, Mayanja alisema hiyo haiwezi kumaanisha moja kwa moja kwamba Simba inaweza kuwa bingwa msimu huu kwani Yanga inaweza kuamka na kufanya vizuri siku za mbele.

Utakumbuka kuwa kuelekea mechi tatu za mwisho za mzunguko wa kwanza msimu uliopita, Yanga iliibuka na kuipiku Simba kileleni, iliyokuwa ikiongoza kwa tofauti ya pointi nane.

“Kikubwa ambacho sisi Simba tunaomba kwa sasa ni kushinda mechi zote za mbele mpaka tukae kileleni kwa sababu hivi sasa Mtibwa ndiyo inaongoza ligi.

“Siku zote nimekuwa nikisema kwamba, ligi ni kama mbio za marathoni, unaweza kuongoza mwanzoni, lakini baadaye mambo yakabadilika na yule aliyeanza vibaya akaamka na kufanya vizuri zaidi yako.

“Hivyo basi, matokeo ambayo wapinzani wetu Yanga wameyapata hivi karibuni, haimaanishi kwamba Simba moja kwa moja itakuwa bingwa msimu huu, kama ujuavyo ligi ina timu 16 na siyo mbili za Simba na Yanga.


“Ukiangalia kwa sasa Mtibwa ndiyo wapo juu, hivyo Mungu anaweza kufanya miujiza yake ukashangaa kuona wamekuwa mabingwa, tunachoomba kwanza sisi tukae kileleni, kisha tuanze kuona mustakabali utakuwaje siku za mbele kwa kuwa ligi bado ni mbichi na hakuna timu inayopenda kuukosa ubingwa,” alisema Mayanja.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic