September 16, 2017



 Na Saleh Ally aliyekuwa Manchester

ANAITWA Rutgerus Johannes Martinus van Nistelrooy, ingawa watu wengi au wapenda soka kwao Uholanzi, Tanzania, England na duniani kote wamemzoea kwa jina la Ruud van Nistelrooy.

Takwimu zinaonyesha Van Nisterlooy ni kati ya washambulizi bora kuwahi kutokea duniani hasa kama utazungumzia washambulizi namba tisa.

Mashabiki wengi hasa wale wasio wa Manchester United au Real Madrid alizozichezea kwa mafanikio makubwa, walikuwa wakisema hakuwa mshambulizi mzuri kwa kuwa kazi yake ilikuwa ni kuvizia tu langoni ili afunge.


SALEHJEMBE haichoki kupiga hatua huku na kule kuwasaka wachezaji nyota kabisa duniani ambao wengine huamini ni vigumu kuwapata.


Van Nistelrooy sasa ni kocha wa timu ya vijana ya PSV ya kwao Uholanzi, timu ambayo ilimfanya atambulike katika ulimwengu wa soka aliyojiunga nayo mwaka 1998 hadi 2001 alipoondoka na kujiunga na Manchester United baada ya Kocha Sir Alex Ferguson kuvutiwa naye.

Takwimu zinambeba kwa kuwa mmoja wa washambuliaji bora kabisa wa kati duniani kutokana na mechi alizocheza na mabao aliyofunga katika timu nyingi alizochezea.



Angalia wakati anaanza kujulikana akiwa na PSV, alicheza mechi 67 na kufunga mabao 62, hivyo kumfanya kuwa na asilimia 94 ya ufungaji wa mabao katika mechi alizocheza za timu hiyo hadi anaondoka kujiunga na Manchester United.

Alipojiunga na Manchester United, alicheza mechi 150, akafunga mabao 95 na kuchukua asilimia 78 za ufungaji ambazo ni moja ya zile zilizo juu zaidi kufanywa na washambulizi waliowahi kuitumikia timu hiyo na kumfanya Kocha Ferguson kujivunia ile kauli yake kwamba Van Nistelrooy ni kati ya washambuliaji bora zaidi waliowahi kusajiliwa na Manchester United, yeye akiwa mwalimu.


 Alipohamia Real Madrid mwaka 2006 hadi 2010, wengi waliamini asingeweza kutamba. Lakini katika mechi 68 alizocheza, alifunga mabao 46. Hii ilizidi kuonyesha yeye ni hatari zaidi na hata wakati anaishia alipoitumikia Hamburger SV ya Ujerumani, alicheza mechi 36 na kufunga mabao 12.

Akiwa timu ya taifa ya Uholanzi, Van Nistelrooy alicheza mechi 70 na kufunga mabao 50. Jambo ambalo linafanya kusiwe na mtu anayeweza kusema yeye si mshambuliaji bora zaidi.




Wengi wanahoji au kusisitiza kuwa hakuwa na ladha nzuri kisoka kwa kuwa alivizia zaidi. Kocha Ferguson aliwahi kulifafanua hilo kwa kusema Van Nistelrooy alikuwa na burudani zaidi kwa kuwa alifunga mabao mengi muhimu.


Lakini akasisitiza kuwa burudani ya soka ni mabao na Van Nistelrooy alikuwa akifunga mabao mengi. Sasa burudani ipi itolewe ili watu waseme ilikuwa burudani?

Katika mahojiano na SALEHJEMBE jijini Manchester, Van Nistelrooy anasema mshambuliaji anayetakiwa kufunga, atumie njia yoyote ili afunge.

Lakini kuhusu kuvizia, anasema ni swali aliloulizwa mara nyingi zaidi akiwa England, hasa waandishi.

“Wewe unatokea Tanzania lakini umeniulizia swali hilo hapa England, huenda ni swali limeundwa kutoka hapa England (anaangua kicheko).

“Waandishi wa England walianzisha huo mjadala, mimi niliamini wengi huwa na timu zao na huenda wasivutiwe na jambo fulani kwako mwisho wanaanzisha kitu fulani. Nimecheza nyumbani Uholanzi, Hispania na Ujerumani. Sijaulizwa hilo swali.


“Unajua kazi yangu ilikuwa kufunga, kama ingekuwa ni kwa kukimbia zaidi ili nifunge ndiyo jambo zuri, ingekuwa bora zaidi. Lakini kama ingekuwa ni kwa kuvizia ili nifunge, ni jambo bora zaidi.




“Kawaida sikuwa nikivizia, huenda ilibadilishwa maana. Ukweli nilikuwa najua namna ya kujipanga, namna ya kutoka haraka na kukutana na mpira. Huenda nilikuwa mjanja au mwenye akili nyingi ya ung’amuzi wapi pa
kukaa.


“Mimi nilijua sana nikae vipi kumpa wakati mgumu beki. Wakati mpira unanifikia hata yeye angeogopa kunigusa. Au wakati anageuka mimi namaliza kazi,” alisema.

“Jiulize, kama navizia sana vipi sikuwa naotea sana. Sasa navizia vipi huku nafunga mara nyingi bila ya kuwa offside.

"Nakumbuka mara nyingi katika mechi nyingi hasa za England na wakati mwingine mabeki wa timu za Hispania, waliwakumbusha waamuzi kuwa waniangalie huwa nafunga mabao ya kuotea. Nia yao ilikuwa ni kujiweka sawa kuwalaghai waamuzi lakini mimi nilibaki kimya na kufunga mabao.”



Alipoulizwa katika matukio anayoyakumbuka zaidi katika Premier League kwa miaka yake sita aliyocheza Manchester United, akasema ni lile dhidi ya Arsenal.


Tukio hilo ni takriban miaka 13 iliyopita, ilikuwa ni mechi ambayo baada ya Manchester United kupewa penalti, wachezaji wa Arsenal walipinga lakini hawakuwa na namna. Van Nistelrooy alikabidhiwa jukumu la kupiga na bahati mbaya kwake akakosa.


Yeye ndiye alikuwa ameangushwa, jambo ambalo wachezaji wa Arsenal walisema alijiangusha. Baada ya kukosa, beki Martin Keown aliwaongoza wenzake wachache kumzonga Van Nistelrooy na yeye alikuwa akimrukia
Mholanzi huyo kama anayetaka kumgonga na kifua.


“Watu wamekuwa wakisema sijasamehe, lakini ni tofauti. Nalichukulia kama tukio la kukumbukwa zaidi ndiyo maana nalizungumzia zaidi. Nikilikumbuka linaniumiza, halikuwa la kiuanamichezo,” anasema.


Mechi hiyo ilibandikwa jina la “Battle of Old Trafford” na baada ya mechi kwisha kwa sare ya 0-0, Arsenal iliendelea kucheza bila ya kufungwa mfululizo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic