September 29, 2017



Na Saleh Ally, aliyekuwa London
UKIFIKA katika eneo la mazoezi la Arsenal katika eneo la Colney, takribani kilomita 41 kutoka katika ya Jiji la London, hakika utasema kuwa Arsenal ni klabu kubwa na ina mipango madhubuti.


Eneo hilo kwa nje linaonekana utafikiri ni la kawaida, lakini kuna ulinzi mkali. Unapoingia ndani mambo ni tofauti kwa kuwa eneo ni kubwa sana. Viwanja kumi vya soka, pia kuna uwanja mmoja wa ndani, gym kubwa na sehemu maalum kwa ajili ya masuala ya afya.

Thamani ya eneo hilo ni zaidi ya pauni milioni 10 (zaidi ya shilingi bilioni 28) na imekuwa ikizidi kuongezeka thamani kadiri siku zinavyosonga mbele na sasa kuna sehemu bora ya mazoezi kwa ajili ya timu za watoto na vijana.

Arsenal ina hadhi ya Real Madrid au FC Barcelona hasa unapozungumzia sehemu ya mazoezi au uwanja kama ulivyo ule wao wa Emirates.




Kabla ya hapo, Arsenal ilikuwa inafanya mazoezi kwenye uwanja wa chuo ambao pia unatumiwa na timu ya Watford ambao unapakana na eneo la sasa la Arsenal ambalo ni mali yake.

Mtu wa kwanza kutia msisitizo kutaka Arsenal iwe na eneo lake na baadaye akatoa wazo la kusaidia kupatikana kwa uwanja ambao unamilikiwa na Arsenal ni Kocha Arsene Wenger, ambaye mwisho alisaidia kwa wazo la kumuuza Nicholas Anelka kwenda Real Madrid na baadaye fedha kuwa chanzo cha ununuzi wa mashamba ambayo sasa ndiyo eneo la mazoezi la Arsenal.



Wenger raia wa Ufaransa, ndiye alikuwa sehemu ya chanzo cha uamuzi wa Arsenal kuona wakati mwafaka wa kujenga uwanja mpya umewadia na mipango ya Emirates ikachagizwa na mwisho, leo Arsenal ni kati ya timu 10 za Ulaya zinazomiliki uwanja wa kisasa zaidi.

Arsenal imeendelea kuwa ndani ya 10 bora na mara nyingi 5 bora ya timu za Ulaya ambazo ni tajiri kifedha. Hii inaonekana ni mipango mizuri iliyoanzishwa na Wenger na inaonekana wazi, klabu imekuwa ikimtumia kama kocha, wakati mwingine kama mtaalamu wa masuala ya kiuchumi.

Kila klabu yenye viongozi wenye “akili timamu” za kibiashara duniani, lazima itaangalia suala la faida kwanza na mengine yatafuatia.

Klabu ipo kwa ajili ya kufanya biashara na biashara ni faida na si kutoa sadaka. Kama klabu inaingiza faida, hakika inakuwa inapanga kuingiza faida zaidi. Na kama kuna mtu anaisaidia kufikia inachokitaka, hakika lazima impe thamani kubwa.



Kuna mtazamo tofauti kati ya mashabiki wengi wa Arsenal na uongozi wa klabu hiyo ambayo imekuwa ikilaumiwa kwa kuendelea kumbakiza Wenger ambaye anaonekana ni kero kwa mashabiki wengi wa Arsenal wakiwemo wale kutoka Tanzania.

Tokeo Wenger ametua Arsenal mwaka 1996 akitokea Grampus Eight ya nchini Japan, amefanikiwa kubeba makombe matatu ya Ligi Kuu England, mataji saba ya Kombe la FA na Ngao za Jamii saba pia.

Kama ni makombe, ukiachana na ngao maana yake anayo kumi. Huyu si mtu ambaye unaweza kusema amefeli na huenda kizazi cha Arsenal kuanzia miaka mitano au sita kimekuwa na hamu kubwa ya kuona kombe la Ligi Kuu England linakwenda Emirates.



Kizazi hicho kinataka kuona kombe hilo, maana kama ni kombe, Wenger amebeba makombe ya FA matatu tokea mwaka 2013 hadi 2017 na kuifanya kuwa klabu ya England iliyobeba makombe mengi ya FA kwa kipindi hicho.

Hamu ya kuliona Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu England, imekuwa ni msukumo wa vijana au mashabiki wengi kutaka Wenger aondoke.

Mambo ni tofauti kabisa kwa uongozi wa Arsenal au wale Arsenal wenye uwezo wa upigaji wa mahesabu hasa kama wanaamini soka ni biashara kubwa na watu kama Wenger wanahitajika kuisaidia klabu kupata mafanikio makubwa kama kocha huyo Mfaransa alivyofanya.

Ukiachana na yale ya kikosi, Arsenal wanaonekana kuwa na manufaa makubwa na Wenger na huenda itakuwa kuna ugumu wa kumuondoa kama ambavyo mashabiki wengi wanataka.



Wenger anaendelea kuwa kiungo muhimu sana katika kikosi cha Arsenal na Klabu ya Arsenal. Viongozi na wamiliki wanamchukulia kama shujaa na ndiyo maana unaona wakati wengi wakipiga kelele aondoke, lakini uongozi wa klabu hiyo ulimuongezea miaka miwili ya kazi.



Hii inaonyesha, huenda wale wanaotamani au wanaotaka kumuona Wenger anaondoka, watasubiri kwa muda mrefu na wasio wavumilivu, wanaweza kuondoka Arsenal na kumuacha Wenger akiendelea “kudundadunda” ndani ya klabu huyo kutoka Kaskazini mwa jiji kubwa zaidi Uingereza la London.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic