September 22, 2017

RAIS WA TFF, WALLACE KARIA


Na Saleh Ally
LIGI KUU Bara inaendelea kuchanua na kadiri siku zinavyosonga mbele burudani yake inazidi kuwa ya kukata na shoka kwa kuwa ni burudani.

Umeona namna ambavyo Simba ilianza kwa kasi lakini bado kuna timu ambazo hazikutarajiwa zilionyesha soka safi na kuwashangaza wengi.

Lipuli FC kuituliza Yanga ikaishia kupata sare au ushindi finyu wa Yanga dhidi ya Njombe Mji. Lakini uliona kiwango cha Majimaji ilipokutana na Yanga na kupata sare ya bao 1-1, wakongwe wakilazimika kusawazisha.

Pia angalia, namna Azam FC iliyokuwa inadharauliwa ilivyoituliza Simba ambayo ilionekana ina uwezo wa kushinda kila mechi mabao sita na kuendelea!

Achana na hivyo, kuna mengi yanaonekana kushitua wengi kwa kuwa hawakuyatarajia kabisa. Kwa muda unavyozidi kusonga, inaonekana kiwango cha ung’amuzi kwamba timu dhaifu ni ipi kimeshuka na kiwango cha ushindani na ubora wa timu nyingi kimepanda.

Kila timu moja inaihofia nyingine kwa kuwa karibu kila timu imetoa sare au kufungwa. Huu ndiyo ushindani unaotakiwa na kama ukiendelea, basi inawezekana tukaanza kuwa na ligi bora.

Hii inaonyesha pia katika uchezeshaji kuna haki na ndiyo maana ushindani unapaa kwa kuwa kila anayeshinda analazimika kufanya kazi ya ziada.

Wakati Ligi Kuu Bara hii hali inaendelea, kinachonishangaza mimi ni kuona Ligi Daraja la Kwanza inaendelea kuwa ligi ya vituko.

Inakuwa ligi ya vituko kwa kuwa kila kukicha unasikia malalamiko kuhusiana na kampeni za makusudi za mikoa kadhaa kutaka timu zao zipande ligi kuu.

Hamu ya kupanda ligi kuu imegeuka kuwa adhabu ya “kuua kwa upanga”, maana timu zinataka kupanda hata kama hazina uwezo. Timu zinataka kupanda kupitia kampeni za kisiasa au za mikoa na kadhalika.

Maana yake, timu zinalazimishwa kushindwa hata kama zina uwezo. Kinachoonekana kila timu inayocheza nyumbani ni lazima ishinde na huenda inafanya hivyo kwa kuwa inajua itakapoenda kucheza ugenini italazimishwa kushindwa.

Malalamiko katika Ligi Daraja la Kwanza si ya leo au juzi na yamekuwa katika kiwango cha juu zaidi, jambo ambalo hakika limepitiliza.

Kama mnakumbuka, misimu miwili iliyopita kulikuwa na kashfa kubwa ya upangwaji wa matokeo na hayo yalikuwa ni matokeo ya uozo wa ligi kuu kwa muda mrefu.

TFF iliyopita ilikuwa vululu, mambo yalienda kirafiki na baadhi ya wapambe wa viongozi walifanya kazi ya kuzunguka mikoani wakisaidiana na timu ambazo waliamini zina fedha ili zipande ligi kuu.

Sasa tunaamini kuna uongozi makini wa TFF chini ya Wallace Karia. Tunajua kuwa uko madarakani kwa muda mfupi, lakini unaona tafrani za uonevu, ugomvi, mechi kumalizika kwa ugomvi mkubwa na waamuzi kuwa na maamuzi yao mfukoni kwa ajili ya manufaa ya wenyeji kwa kuwa nao wanakuwa ni ‘wenyeji’.

Wakati TFF ya Karia ilipoingia madarakani, imeingia na kuzungumzia suala la kutaka kuongeza timu katika ligi kuu kwa madai ya kutaka wachezaji wa Tanzania wawe na nafasi ya kucheza mechi nyingi.

Kwangu niliona ni haraka au kukurupuka, nimeshauri uboreshwaji kwanza wa mambo kadhaa kwa kuwa kigezo cha mchezaji bora si kucheza mechi nyingi pekee.

Ligi daraja la kwanza ikiwa bora inaweza kuwa mchango wa kujenga wachezaji bora. Wachezaji ambao wataingia Ligi Kuu Bara wakiwa washindani hasa kutokana na ushindani wanaoupata katika ligi husika.

Kiwango bora katika nchi, hakiwezi kupimwa na ligi kuu pekee. Hivyo kuna haja ya TFF kuinua macho yake haraka katika ligi daraja la kwanza na kurekebisha mambo la sivyo itakuwa ni ligi ya vituko inayozalisha vituko na kupandisha vituko katika ligi kuu.

SOURCE: CHAMPIONI




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic