October 4, 2017



Na Saleh Ally
UMEWAHI kuwasikia mashabiki wa Simba wakilalamika kuhusiana na kocha wao Joseph Omog? Kama haujawahi, nakuombea isitokee ukasikia maana kama unaelewa mambo, basi ni jambo linaloweza kukupa kichefuchefu!

Wako wanaoamini kulalamika ni haki yao na huenda wanaamini ni timu yao hivyo kulalamika ni haki yao, jambo ambalo binafsi naona ni umbumbu uliopitiliza kuhusu mambo na kutotaka kujifunza, kunazidi kuwafumba macho waendelee kuwa walalamikaji wanaotaka kuichanganya timu yao itoke ilipo na kuingia kwenye “mwendo wa kuyumba”.

Mashabiki wa Simba, wameingia kwenye kundi la ubora wa lawama. Tena ni lawama ambazo hazina sababu za msingi na wao wanazikweza wakiona Omog anakosea sana kukipanga kikosi lakini hawana ushauri mbadala wanaoutoa na wengine ni bendera fuata upepo tu, hakika wanakera zaidi ya kuudhi.

Nani kasema ukiwa shabiki basi uropoke tu? Nani anasema shabiki kusema anavyojisikia, basi aseme tu hata kama hajui? Huenda huu ni wakati mwafaka wa kuliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuipa Simba nafasi ya kutumia wachezaji 13 badala ya 11 ili kuwaridhisha mashabiki wao.

Angalia, baada ya sare ya mabao 2-2 ya Simba dhidi ya Mbao FC. Shabiki mmoja wa Simba alinipigia simu kulalamika, kocha alikosea kupanga kikosi akisema angekuwepo Salim Mbonde wao wasingefungwa. Nikamuuliza kama kuna beki kati ya Juuko Murshid au Method Mwanjale alikosea. Akasema hapana, akakubali kuwa mashuti yote yalitokea nje ya 18, bao moja ikionekana ni krosi lakini ikajaa wavuni. Sasa kosa la Juuko na Mwanjale lilikuwa lipi na angekuwepo Mbonde angezuiaje? Akakata simu!


Mbonde Vs Juuko
Kwa sasa Simba ina kikosi kikubwa na inalazimika kuwa na wakati mgumu wa kupanga kikosi. Kama unakumbuka kuna mashabiki walilalamika kukosekana kwa Juuko Murshid, uongozi ukafanya juhudi na kumleta. Leo akicheza inaonekana Mbonde angekuwa bora zaidi. Lakini kumbuka, wako waliolalamika Mbonde aliposajiliwa Simba, wako waliolalamika pia kwamba si beki bora. Sasa Omog awapange namba moja wote?


Juuko Vs Mwanjale
Amecheza Mwanjale, wako wanaosema angecheza Juuko. Lakini unakumbuka Mwanjale aliituliza kwa uhakika safu ya ulinzi ya Simba na alipokuwa hachezi baada ya kuumia kwake msimu uliopita, wakasema kumkosa ndiyo maana wameyumba. Sasa amecheza, tena vizuri kabisa, wako wanaoona angecheza Juuko ndiyo vizuri zaidi!



Mkude Vs Kotei

Huu umekuwa mjadala mwingine ambao umejaa lawama za kijinga kutoka kwa mashabiki ambao wanaangalia ushabiki zaidi kuliko ufundi. Hata mimi kwa ushabiki ningechagua, Jonas Mkude acheze badala ya James Kotei, ukiniuliza nitakuambia kwa kuwa ni Mtanzania.
Lakini kiuchezaji, kocha ana mfumo wake na huenda Omog anavutiwa na ukabaji wa Kotei na upigaji wake pasi za kuhamisha uwanja, haraka na nyingi ndefu zinazotengeneza “tempo” ya timu kushambulia kwa kasi kuliko Mkude anayepiga fupifupi.
Lakini watu wanalalamika, ukiwauliza Mkude na Kotei nani ana kiwango kizuri zaidi, wanasema Kotei. Lakini wanataka Mkude aanze, sasa jiulize acheze kipa? Au Simba wacheze 13?


Bocco Vs Mavugo
Karibu kila shabiki wa Simba alilalamika kuwa Laudit Mavugo hafai, Mrundi huyo ambaye mimi bado ninaamini ni mshambulizi mzuri sema anapaswa kupunguza papara, alionekana hafai kwao.
Leo yupo John Bocco, mashabiki wamegeuka wanamtaka acheze Mavugo kwa kuwa Bocco anakosa sana! Sasa Bocco akae nje? Kama hapana Simba wacheze 12 au 13?
Angalia wako waliotaka Bocco atolewe wakati Mavugo anaingia Vs Mwadui FC, hakutolewa akabaki na kufunga, wakakaa kimya.
Juzi Bocco ametoa pasi ya kifua kwa Kichuya akafunga bao dhidi ya Stand United. Kuna fowadi hakosi? Nani asiyejua ubora wa Bocco? Lakini Mavugo bado anapewa nafasi na anafanya vizuri na huo ndiyo ubora wa kikosi kupitia upana.



Ndemla Vs Niyonzima

Bado wako wanaojadili Said Ndemla aanze, hata mimi kwa ushabiki ningewashauri hivyo Simba. Lakini kiufundi, kama anaanza Ndemla, basi Haruna Niyonzima analazimika kubaki nje, nani kati yenu anaona sawa?
Nafikiri si vizuri kulalamika kwa kuwa unamsikia fulani analalamika tu, wakati mwingine kabla ya kutoa malalamiko yako, yafanyie uchunguzi kwanza.

FIN.





















2 COMMENTS:

  1. Katika vitu vinavyo nikera Mimi ni mashabiki kupanga kikosi chao, ifike wakati tumwachie kocha afanye kazi yake.

    ReplyDelete
  2. Dah!! Mkuu kweli mashabiki wakibongo umewapatia hasa. Simba sasa hivi inaenda vizuri tena sana na wana kikosi kipana sana. Wamwache kocha na wachezaji watimize wajibu wao. Mambo ya kupanga vikosi haya bado utasikia kapanga kikosi cha mashabiki. Ole timu ifungwe balaaa. Hongera kwa uchambuzi mzuri. Bigup

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic