Beki wa kati wa Kagera Sugar, Juma Nyosso, amemmwagia sifa mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu kutokana na kazi kubwa aliyoifanya uwanjani juzi Jumamosi.
Ajibu aliiongoza Yanga, kuibuka na ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Katika mechi hiyo Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ambayo yalifungwa na Ajibu pamoja na Mzambia, Obrey Chirwa.
Nyosso amesema kuwa walijitahidi sana kumzuia Ajibu asisababishe madhara katika lango lao lakini ilishindikana baada ya kuwazidi ujanja.
“Mechi ilikuwa nzuri na yenye upinzani mkubwa lakini mchezaji wa Yanga ambaye alitupatia shida sana kumkaba alikuwa ni Ajibu.
“Tulijitahidi kumzuia lakini mwisho wa siku akatuumiza lakini hivyo ndivyo soka lilivyo, tumekubaliana na matokeo na sasa tunajipanga kwa ajili ya mechi zetu zijazo,” alisema Nyosso ambaye katika mechi hiyo alionyesha uwezo mkubwa.
Alifanikiwa kuokoa hatari mbili langoni kwake lakini alikuwa ni kikwazo kikubwa kwa washambuliaji wa Yanga, Ajibu na Chirwa kupata nafasi za kufunga.
Lakini pia katika mchezo huo alimsababishia Chirwa kadi ya njano katika dakika 79 baada ya kumkanyaga wakati walipokuwa wakiwania mpira.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment