Baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mwadui FC wakiwa ugenini, benchi la ufundi la Azam chini ya kocha wake mkuu, Aristica Cioaba raia wa Romania, limeweka bayana kwamba ni ngumu kupata matokeo mazuri wakiwa mkoani kutokana na wapinzani wao wengi kukamia michezo yao.
Azam ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga, ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji wao Mwadui wanaonolewa na kocha Jumanne Ntambi, kwa matokeo hayo Azam sasa wamefikisha pointi 12 baada ya mechi sita.
Mromania huyo amesema kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu kwao licha ya kujiandaa vizuri kuibuka na ushindi lakini wapinzani wao waliwakomalia na kuambualia pointi moja pekee.
“Huku mikoani kugumu sana kupata pointi, nasema hivyo kwa sababu tunaocheza nao mara nyingi wanajitoa kupigania wasifungwe na kupoteza pointi kwenye kiwanja chao cha nyumbani, jambo ambalo huwafanya wacheze kwa ari ya juu sana.
“Lakini hata hivyo siyo mbaya kuambulia pointi hii moja tuliyoipata ambayo inatufanya tuendelee na mapambano yetu mengine kwenye ligi, na kuhusu mchezo huu tayari tumeshaumaliza, tunachokiangalia kwa sasa ni juu ya michezo yetu ijayo,” alisema kocha huyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment