October 21, 2017


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.
MAJUKUMU ya kusimamia utendaji bora katika nchi haliwezi kuwa jambo rahisi au dogo, lakini ningependa kutumia nafasi hii kufikisha ujumbe wangu kwako kwa kuwa ninaamini ndiyo kipindi mwafaka kabisa kufanya hivi.

 Nilikuwa naangalia baadhi ya picha zako, huenda niliona vibaya lakini nimeona kama unazeeka haraka na akili yangu imenieleza “huyu mzee” ana mambo mengi na anapambana kwa ajili ya nchi, hii maana yake unapambana kwa ajili yangu mimi na Watanzania wengine.

Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally (kushoto) akiongea jambo katika ofisi yake na Kaimu Katibu Mkuu wa Shrikisho Soka nchini (TFF) Wilfred Kidao (kulia).
 Kwa hali inavyokwenda siwezi kuamini unapatia kila jambo kama mwanadamu lakini ninaamini unajifunza mengi kila unapopita na huenda kuna njia ya kurejea na kuyafanya yale ambayo ulijifunza.

 Kilichonivutia kukuandikia barua hii ni kwa kuwa upatikanaji wako huenda ningefikisha maneno yangu kwa mdomo tukiwa ana kwa ana unaonekana kuwa ni mgumu. Bado nina imani kubwa, kuna siku nitakutana nawe na kuzungumza mambo kadhaa na nitapata nafasi ya kutoa maoni yangu na mawazo niliyonayo.

 Kwa kuwa ninajua ni kati ya wasomaji wa Gazeti la Championi, nikaamua kukuandikia barua hii nikiwa na uhakika ujumbe wangu utafika kwako.
Nina mambo mawili tu; kwanza itakuwa pongezi na pili litakuwa ni suala la kukumbusha jambo ambalo serikali ya awamu ya tatu, na ya nne hawakulifanyia kazi. Hivyo ninaamini kwa mwendo wako, linaweza kufanyiwa kazi kwa kuwa imeonekana ukiamua jambo; halishindikani.
 Kwanza nianze na kukupongeza kuhusiana na ule mzozo unaohusisha jambo la Makinikia ambalo liliwagawa Watanzania, wakawa katika makundi mawili, linalokuunga mkono na lile lisilokuunga mkono.

 Wakati mwingine watu walishindwa kukaa katika kundi moja wakiwa wanahamahama. Maana ilionekana uko sahihi, wakati mwingine ikaonekana unatuingiza katika matatizo, basi ikawa hofu tu.
 Kilinichonifurahisha ni kwa kuwa ulishikilia msimamo wako hadi mwisho wa jambo. Sasa majibu yametoka kuwa katika makubaliano na Barrick, Serikali nayo itapata hisa ya asilimia 16.

 Ukiachana na hilo kuna mambo mengi mazuri ambayo yatakuwa mapinduzi katika mikataba mingi ambayo Serikali yetu itaingia kama vile ofisi za wahusika kuwa hapa nchini, fedha kuwekwa hapa nchini, mgawo wa faida kuwa hamsini kwa hamsini, huduma za migodini kufanywa na Kampuni za Tanzania, kuimarishwa kwa huduma za jamii, kuajiri Watanzania katika nafasi muhimu za uongozi, kutengwa bajeti ya kiwanda cha kuchakata makinikia hapa nchini, muwekezaji kuchukua dhahabu wakati serikali itachukua shaba na fedha.

 Yako mengi na wakati yakiendelea, Barrick wamekubali kulipa Sh bilioni 700 kama fidia. Hili ni jambo la kupongezwa bila ya woga wala kuzunguka.
 Huenda wako wanaoweza kujisikia vibaya kutoa pongezi kwa kuwa awali hawakufanya hivyo kutokana na mawazo tofauti. Nawashauri kuwa watu chanya na kuonyesha kuwa walifikiri tofauti na sasa wanaweza kusema ukweli.

 Siamini kama nikiamua kusema ukweli utakasirika kama watu wanavyosema. Mfano, kuna baadhi ya watendaji wamekuwa wakikuangusha kwa utendaji mbovu na mwisho wananchi wakakulaumu wewe kwamba Serikali yako inawaonea. Siamini kama kila jambo huwa unaagiza. Badala yake wako waoga au si wabunifu basi hufanya mambo ili mradi.

 Bado narudia kukupongeza kutokana na msimamo uliouonyesha katika sakata hili la Makinikia na ninajiuliza namna ambavyo Tanzania ilivyopoteza vitu vingi sana kabla ya wewe kufikia kuchukua msimamo huu na kuushikilia. Natoa pongezi katika hili na ninasema nitakuunga mkono katika mambo kama haya kwa kuwa unaonyesha umelenga kuwasaidia Watanzania kujikwamua na kufaidika na nchi yao.

 Wakati namalizia pongezi, suala la pili kama nilivyosema awali, kukuomba. Kama kweli umekomaa na Makinikia ambayo watu waliamini haiwezekani, nakukaribisha huku katika michezo. Karibu tafadhali uwakomalie hasa katika viwanja.

 Bahati nzuri wewe ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinamiliki viwanja vingi zaidi vinavyotumika katika michezo ukiwemo wa soka.

 Vibaya zaidi, vimechakaa sana, wanaoongoza si wabunifu, vyoo ni vichakavu na sehemu za kuchezea au huduma kwa jumla ndani ya viwanja hivyo ni dunia kabisa.
 Viwanja hivyo vinaipaka matope CCM na inaonekana wahusika wameotesha mizizi na wako tayari kupokea fedha lakini hawajali kuhusu huduma. Wakumbuke wanaowahudumia ni wananchi walewale unaowapigania.

 Ninaamini wapenda michezo nao wana haki ya kupata huduma bora. Michezo inaweza kulitangaza taifa, michezo ni ajira inaweza kuisadia Serikali kuiboresha ajira lakini michezo ni furaha na faraja.
 Tafadhali, dude la Makinikia lishushe huku michezoni, wabane vijana wako wa CCM wavikarabati viwanja ili wanacholipwa kiendane na malipo wanayopokea.

 Sijui kama fedha wanazolipwa timu zinapocheza au kunapokuwa na sherehe huwa zina mahesabu au zinapita katika utaratibu sahihi au zinaingia mifukoni mwa wahusika! Lakini huku wanatutesa sana, hawasikii, hawaogopi na wanaendelea wanavyotaka.
 Sipendi kuandika barua ndefu sana, lakini baada ya kuisoma, naomba utusaidie wapenda michezo ili tukusaidie kuzalisha ajira zaidi, upendo na ushirikiano lakini furaha na ukakamavu.
Nikutakie Jumamosi njema.
Ndimi Mtanzania mpenda nchi yake.

Mhariri Mtendani wa Global Publishers, Saleh Ally

2 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic