October 6, 2017




NA SALEH ALLY
KUNA wakati kuna shabiki mmoja wa Yanga aliwahi kunitumia ujumbe mfupi kupitia mtandao wa kijamii, akaniambia kwamba angependa kuona namuacha kiungo kinda wa Yanga, Juma Mahadhi.

Nikamuuliza, angependa nimuache kwa maana ipi kwa kuwa sipo karibu naye, sikuwa nimefanya lolote linaloonyesha kumzuia au kumfanya asifanye jambo fulani, hasa lile unaloweza kuliita jambo zuri.

Akaniambia nimekuwa nikimsakama sana hadi anachanganyikiwa na kushindwa kucheza. Nilisikitika sana kutokana na maneno ya shabiki huyo wa Yanga.

Nilisikitika si kwamba nilijisikia vibaya, badala yake nilimuonea huruma na kumuona ni mtu mgumu sana kuelewa na huenda hata maandishi niliyokuwa nayaandika kuhusiana na Mahadhi hakuwahi kuyasoma au aliyasoma hakuelewa nilikuwa ninamaanisha nini.

Mbaya zaidi, niliwahi kuandika mara moja kuhusiana na Mahadhi hivyo hakuna sababu ya kusema kwamba ninamsakama au namfanya asifanye mambo yake kwa kuwa nilichoandika kilikuwa ni msisitizo wa kumkumbusha kwamba anakwenda katika njia ambayo si sahihi.

Leo bila ya kujali nani hapendi kwa kuwa najua ninachofanya ni sahihi na nia yangu ni sahihi kwa kuwa nimelenga kuona Mahadhi anafika mbali kutokana na ninavyoamini, basi ninamuandikia tena na akiendelea kulala nitamuandikia tena na tena.

Naendelea kujiuliza, kwa mchezaji kama Mahadhi ambaye nilimuona anapaa akiwa Coastal Union miezi kadhaa iliyopita, vipi anaweza kutua haraka hivyo baada ya miezi kadhaa akiwa na timu kubwa kama Yanga.

Wapo ambao wamekuwa wakilalamikia nafasi; lakini mimi napishana nao na niliwahi kutoa mfano wa msimu uliopita kuwa mwishoni baada ya Yanga kuandamwa na majeraha mfululizo, Kocha George Lwandamina alimpa nafasi ya kuwa kiongozi wa mashambulizi, akashindwa.

Bado Lwandamina amempa nafasi ya kukaa benchi na pia kuingia katika baadhi ya mechi ambazo ni muhimu sana. Lakini Mahadhi ameshindwa kuonyesha lolote ambalo linaweza likamfanya apewe nafasi tena na tena.
Najiuliza kasi ya Mahadhi ambayo alikuwa nayo wakati Coastal Union inapambana na Simba au Yanga iko wapi? Nani kaichukua? Kaipeleka wapi na kwa sababu zipi?
Angekuwa hachezi angalau, anacheza na bado anashindwa! Shida ni nini kwake? Na kama ipo azungumze na kocha wake na kumueleza kinachomsibu ili aweze kumsaidia na kukifanyia kazi.

Mfano kwa mategemeo ya kawaida kabisa, baada ya kuondoka kwa Simon Msuva, mchezaji ambaye alitakiwa aibebe Yanga kutokea pembeni kwa kasi, krosi za uhakika na nguvu, alipaswa kuwa ni Mahadhi. Sasa kwa nini wakati yupo Msuva tuliamini ni vigumu kwake kupata nafasi na kutamba pembeni na sasa ameondoka bado mambo ni yaleyale na ikiwezekana ni nafuu ya msimu uliopita!

Kwangu naona kuna mambo mawili matatu kuhusiana na Mahadhi na inawezekana ameyakubali yanaendelea kumuangusha na atalazimika kubadilika ili kutoka alipo.

Huenda ameridhika na kufika Yanga kwake ilikuwa ndoto anaona inatosha na kama ni hivyo ni kosa kubwa kwa kuwa safari yake ya mpira ndiyo inaanza na anapaswa aonyeshe uwezo wa juu ili apate nafasi ya kuondoka Yanga akiwa hitaji kubwa na kusajiliwa na timu za juu ya Yanga hasa nje ya Tanzania.

Inawezekana Mahadhi amekubali zile imani za kishirikina, baada ya kushindwa kufanya vizuri, ameanza kuamini “kapigwa misumari” na alio karibu nao wanaendelea kumuaminisha hivyo. Hivyo kisaikolojia, anazidi kupotea kabisa. Kinachotakiwa lazima amuamini Mungu na aelewe mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na si ushirikina na hakuna anayeweza kuzuia “Juhudi na Maarifa”.

Pia anaweza akawa anaamini kocha hampendi, au hapewi nafasi ya kutosha hivyo akakaa pembeni na kazi yake ikawa ni kulaumu tu, jambo ambalo litazidi kumdidimiza tu.

Nafasi anapata na nafasi inayotumika huwa ni nafasi ndogo tu. Huhitaji dakika 90 kumuonyesha kocha unafaa au unahitajika. Dakika tano au 10 zinaweza kutosha kabisa kumbadili kocha mawazo kwamba ninamhitaji huyu mtu si kuingia badala yake kuanza kabisa.

Sijachoka bado, nina matumaini makubwa na Mahadhi kwamba pamoja na kuwa msaada kwa Yanga anaweza kuwa msaada kwa taifa letu. Hivyo ninaendelea kumsubiri tu hadi siku atakapoamka, nami nitachukua njia yangu kuendelea na safari zangu.




1 COMMENTS:

  1. Kwahili la Mahadhi upo sahihi yaani dogo amepotea na kipaji anacho mimi nahisi kuna ulimbukeni anahisi amefika na pia utoto maana ana mambo mengi sana akiwa karibu na goal. Mwengine wa kumkumbusha ni Juma Abdul Jafar naye mafanikio nahisi yashamlevya. Endelea kutumia kalamu kwa maendeleo ya Taifa ipo siku utakumbukwa kama gwiji wa habari za michezo kama kina Charles Hillary na wengine

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic