October 27, 2017




Utakuwa unakumbuka lile sakata kiungo Pius Buswita kufungiwa baada ya kusaini Simba na Yanga hadi pale alipokombolewa.

Sasa siku imewadia, siku ya Buswita kuonyesha alichonacho dhidi ya Simba.

Buswita amesema atautumia mchezo kuwaonyeshea mashabiki wa timu hiyo kuwa hajakosea kurudisha fedha za usajili za Simba ili atue Jangwani.

Kiungo huyo, hivi karibuni aliwekewa pingamizi na Simba katika usajili wake baada ya kusaini Yanga kwa kile kilichoelezwa kusaini klabu mbili tofauti kabla ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumfungia hadi atakaporejesha shilingi milioni 10 alizozichukua kutoka Simba.

Nyota huyo, baadaye alirudisha fedha hizo na kurejea kuanza kucheza mechi dhidi ya Mtibwa Sugar. 

Buswita alisema mechi ngumu ndizo anazozipenda kwa ajili ya kudhihirisha ubora wake alionao, hivyo amejiandaa vema kuhakikisha anaonyesha kiwango kikubwa katika mchezo huo.

Buswita alisema, ana vitu vya kuifanyia klabu yake ya Yanga ikiwemo kuifungia na kutengeneza nafasi za mabao kama shukrani baada ya kutua kuichezea timu hiyo katika msimu huu.

“Niliumia kuikosa mechi iliyopita dhidi ya Simba, kocha alinipanga katika kikosi cha kwanza alichokipanga kianze, lakini dakika za mwishoni niliondolewa baada ya viongozi wa Simba kuniwekea pingamizi TFF baada ya kuchukua fedha zao za usajili na kunitaka nirudishe ndiyo nicheze.

“Hivyo, basi baada ya kuikosa mechi hiyo ya Ngao ya Jamii, mechi hii ya ligi kuu ninaamini nitakuwepo kwenye kikosi kitakachocheza na Simba, hivyo ni mechi kubwa kwangu kucheza ambayo nimepanga kuonyesha kiwango kikubwa.

“Nitacheza mechi hii kwa lengo la kuwaonyeshea Wanayanga kwa nini nilirudisha fedha za Simba ili niichezee Yanga katika msimu huu nikitokea Mbao FC,” alisema Buswita ambaye ameifungia Yanga bao moja katika mechi mbili alizozicheza.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic