October 23, 2017



NA SALEH ALLY
INAWEZEKANA ukaona naendelea kulirudia hili suala mara kwa mara na utajiuliza ni kwa nini nimekuwa nikifanya hivi. Kawaida kama kuna jambo unalichukulia kama kero basi lazima ukubali kwamba vizuri hadi hapo litakapopatiwa ufumbuzi.

Suala la viwanja vya kuchezea mpira vimekuwa ni tatizo sana na tunakubaliana hadhi ya Ligi Kuu Bara imekuwa si ile hasa unapoangalia katika runinga.

Huenda runinga ya Azam TV ambayo huonyesha mubashara mechi za Ligi Kuu Bara imechangia kwa kiasi kikubwa Watanzania kuanza kuona kasoro ya viwanja vyetu kwamba kweli ni vibaya sana.

Viwanja vina hadhi duni na kitu kinachoshangaza ni kuona sehemu ambazo zinakuwa mbaya zaidi ni katikati ya uwanja ambako mechi itachezwa, hiyo ndiyo sehemu ambayo timu hucheza mechi na timu ndizo zinazowavuta mashabiki kufika hapo.

Kinachonifanya nirudie kusisitiza kuhusiana na viwanja ni kwa kuwa mara nyingine tena nimeona mechi zinachezwa, hivyo ninaamini tatizo bado lipo na linawezekana kupatiwa ufumbuzi.

Miaka mitatu kabla nilipiga kelele kuhusiana na viwanja kuwa na kiwango duni hadi ufumbuzi ulipopatikana. Nashukuru tatizo lilionekana na wahusika wakakubaliana na mimi na uwanja niliokuwa nikiupigia kelele sana ni Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Ufumbuzi ulipatikana, nafuu inaonekana na mambo yanawezekana. Lakini nashangazwa kuanza kuona viwanja vilivyokuwa na nafuu ndiyo vimekuwa tishio kwa ubovu na mmoja wapo ni Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga.

Kama uliangalia mechi kati ya wenyeji Stand United dhidi ya Yanga, utakubaliana nami. Hakika ni aibu na jambo la kushangaza kabisa nimekuwa nikijiuliza, wahusika wa uwanja huo hawaoni aibu kukaa jukwaani na kuangalia mpira?

Kama hawaoni aibu wao ni watu wa aina gani asioumizwa na utendaji wao duni na kipi kinaweza kuwa kisingizio kwa kuwa maji yapo, majani yapo na fedha wanazo kufanya angalau ukarabati unaoweza kuufanya uwanja utumike kwa matumizi ya mchezo wa soka.

Kama Uwanja wa Kambarage ulikuwa kati ya vile vinavyosifiwa kwa ubora misimu miwili iliyopita, vipi sasa kiwango kimeporomoka hadi uwanja huo kufikia kati ya vile vinavyotisha kabisa?

Wako wapi wahusika na kwa nini hawashughulikii? Hawashughulikii kwa kuwa hawana hofu ya kuwajibishwa? Hawashughulikii tatizo kwa kuwa hakuna aliyewahi kuwajibishwa?

Kama sivyo, basi tuamini wahusika wa viwanja hivyo ambao ni viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala, hawana hofu yoyote na yeyote kwa kuwa wanatokea chama tawala?

Lakini najiuliza pia kwamba wahusika hawana hofu hata kidogo ya kuona kuna mabadiliko ya utendaji katika serikali ya awamu ya tano na wanaweza kuwajibishwa?

Kwa nini watu hadi wawe na hofu ndiyo wafanye utendaji bora na kwa nini watu hadi waadhibiwe ndiyo wafanye jambo sahihi?
Tunakubaliana kwamba serikali ni ya wananchi. Kama haisikilizi malalamiko ya wananchi itawezaje kuwa na utendaji bora ambao unaonyesha kwamba kweli ni chama kinachowajali wananchi?

Ushauri wangu kwa viongozi hasa wenyeviti wa mikoa kulishughulikia hili tatizo la viwanja na kama haiwezekani au wameshindwa kuwawajibisha wahusika, basi wao wanapaswa kuwajibika na wakiendelea kulala, basi wawajibishwe.

CCM imepata nafasi ya kumiliki viwanja, lazima ikubali viwanja hivyo ni kwa matumizi ya wananchi na kama ni hivyo lazima iboreshe huduma kwa kuwa inachukua fedha viwanja hivyo kutumika.

Mimi sitaacha kuwakumbusha, sitaacha kusema kuhusiana na viwanja vibovu na siku nikipata nafasi ya kukutana na Mwenyekiti wa CCM, Dk John Pombe Magufuli nitamkumbusha kwamba kuna wazembe ambao wanaangusha juhudi zake za utendaji bora unaojali wananchi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic