Na Saleh Ally, Ujerumani
BAADA ya kutoka Dortmund nimekuja katika eneo la Gelsenkirchen ambalo mbali sana na Dortmund pia mji wa Born ambao ni wa nne kwa ukubwa katika miji ya hapa Ujerumani.
Nilitembelea Uwanja wa Veltins Arena ambao unamilikiwa na klabu ya Schalke 04, moja ya klabu kubwa hapa Ujerumani na kubwa katika Bundesliga, ligi yao maarufu sana duniani.
Lengo langu ni ziara ya mambo mbalimbali yanayoihusu Bundesliga, ligi ambayo licha ya kutokuwa na watu wengi wanaoitazama lakini ni bora na inavutia sana kutazama kutokana na kuchezwa kwa aina zote, nguvu na ufundi.
Kwa nyumbani, StarTimes ndiyo wanaoonyesha ligi kupitia king’amuzi chao na idadi ya wale wanaoangalia imekuwa ikizidi kupanda mara moja baada ya nyingine ikionekana sasa wanaanza kuielewa.
Baada ya kufika Veltins Arena nikiwa nje na mataalamu wa uwanja huo pamoja na baadhi ya waandishi kutoka katika nchi nyingine nne za Afrika, China pia niliona uwanja pembeni mwa Veltins Arena.
Katika hali ya kawaida, niliamini uwanja huo ulikuwa ni kwa ajili ya mazoezi. Hivyo pembeni yake baada ya kuegesha basi letu, tulipanda ngazi na kuingia ndani ambako tulipata maelezo ya uwanja huo kama vyumba vya kubadilishia nguo, chumba cha waandishi, sehemu ya mgahawa wa ndani kama viwanja vingine vya Hispania na England, ambavyo nilikuelezea.
Kwa maana ya kuweka mambo kwa mpangilio, Wajerumani wako vizuri sana na mambo yao yamenyooka hasa. Lakini tulipotokea katika eneo la ndani la uwanja, yaani sehemu ya kuchezea, hakukuwa na majaji, yaani pitch.
Kawaida utaona kama uwanja umefunikwa chini hivi na saruji. Hapo ndipo nilipoanza kujifunza nami nawagawie wasomaji wa SALEHJEMBE na wale ambao wataangalia Bundesliga kupitia Startimes waweze kujionea.
Aliyekuwa anatutembeza, ameiambia SALEHJEMBE kwamba ule uwanja niliouona pale nje, ndiyo ulikuwa uwanja ambao huchezewa mechi hapo ndani tulipokuwa tumesimama.
Swali la kwanza ni kwanini uko nje, unafanya nini huko? Huku akitabasamu, akaniambia ulikuwa nje ukiota jua na kupata hewa na baada ya pale utarudishwa ndani kutumia teknolojia ya kisasa.
Lilikuwa jambo linalolazimisha kuinama, kuchungulia mara kadhaa kuhakikisha na hata kuomba kuingia pale kwenye ile saruji ngumu kujaribu kuhakikisha kwa kuusaka uwanja huo.
Baada ya kubaini ni kweli, ndipo alinipa maelezo kwanini wameamua kufanya hivyo. Kawaida uwanja wao umefunikwa na ukifunguliwa inakuwa sehemu ndogo sana kwa kuwa runinga nne za uwanja huo, huwa ziko juu katikati ukilinganisha na nyingine.
Viwanja vingi hulazimika kubadilishwa mara kwa mara kama hazipati jua la kutosha na kufanya hivyo ni gharama kubwa, hufikia hado euro 60,000 (zaidi ya Sh milioni 158) na klabu huweza kufanya hivyo mara nne hadi sita kwa mwaka.
Kurahisisha hilo ni kuhakikisha uwanja unapata hewa na mwanga wa jua wa kutosha. Hivyo uwanja huo kutolewa nje ni kuufanya uwe salama zaidi na klabu kwa msimu inaweza kuubadilisha mara moja tu au la.
Gharama ya kuutoa nje na kuurudisha mara moja ni euro 7,500 (Sh milioni 19.7), unaweza kusema takribani milioni 20. Hii ni kwa kuwa wakati unatolewa mitambo yake hutumia mafuta, oil au vilainishi pia umeme na nguvu kazi ya watu 10 kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa mpangilio na mabenchi kurejeshwa eneo lake sahihi.
Veltins Arena ni uwanja unaobeba idadi ya watu 62,271 na ni maarufu katika eneo hilo linalozungukwa na Dortmund na Koln na idadi ya ujumla ya miji ya eneo hilo ni watu milioni 5 na ushee.
Kitu ambacho wamekuwa wakisumbuka sana ni eneo la kufanya matamasha au mikutano mikubwa. Sasa Veltins Arena limekuwa ndiyo suluhisho na wanaingiza mamilioni ya euro kupitia kazi hiyo.
Hivyo uwanja unapotolewa nje, linabaki eneo la saruji ambalo limetengenezwa vizuri kabisa kwa kuwa mabenchi ya wachezaji, makocha na waamuzi husogea pembeni, basi nafasi inakuwa ya kutosha na kuingiza zaidi ya watu 79,612 kwa kuwa hata eneo hilo la kati hutumika pia.
Kivutio kingine ni kwamba idadi ya watu wanaoingia uwanjani wakati wa mechi za Bundesliga ni 62,271, lakini kunapokuwa na michuano ya kimataifa hasa Uefa au Europa League, mashabiki wanaoingia wanakuwa ni 54,740.
Hii ni kwa kuwa wakati wa Bundesliga kuna jukwaa moja kubwa na moja dogo ambalo linaingiza mashabiki wakiwa wamesimama. Lakini Shirikisho la Soka Ulaya )Uefa), limezuia mambo ya mashabiki kusimama sababu ya usalama katika michuano hiyo.
Hivyo kila kunapokuwa na michuano ya kimataifa, katika eneo hilo kunarejeshwa viti na baadhi ya vyuma kuondolewa na mambo kama kawa yanaendelea. Ikiisha michuano ya Ulaya, mambo yanarejeshwa kama kawaida, ni “Full kusimama” na kuimba.
Kumbuka Uwanja huu uliokamilika mwaka 200, ulitumika katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2006, pia kwenye Kombe la Dunia mwaka 2006. Umekuwa ukitumika katika michuano mingine mbalimbali.
Mechi ya kwanza kutumika ilikuwa ni Agosti 18, 2001, pale wenyeji Schalke 04 walipopata sare ya mabao 3-3 dhidi ya Bayer Leverkusen. Majani yake ni yale asilia hasa.
Kingine ambacho unaweza kujua ni kwamba uwanja huu una nyota 4, kawaida Uefa inapotoa nyota nne kwenye uwanja ni kiwango cha juu kabisa kama ilivyo katika hoteli zenye nyota 5.
Kwa wale wanaoshuhudia Bundesliga katika Startimes wanaweza kuendelea kujifunza na kufaidika kupitia uwanja huo kila watakapokuwa wakiangalia mechi za Schalke 04.
.
0 COMMENTS:
Post a Comment