November 13, 2017




Na Saleh Ally
MOJA ya picha Simba wakiwa kambini huko Sumbawanga, wachezaji wanaonekana wakimsikiliza mwalimu wao, Joseph Omog lakini kiungo Mohamed Ibrahim, yeye anaangalia upande mwingine na ukiangalia vizuri ni sawa na mtu asiyehusika na kundi hilo.

Mo Ibrahim lazima atakuwa ni mtu ambaye kama mimi au wewe, hawezi kuwa anafurahia kukaa benchi kwa kuwa msimu uliopita alipambana kwelikweli na akaonyesha uwezo. Matarajio yake, msimu huu ilikuwa ni kupata nafasi ya kucheza.

Picha ile inaonyesha ni mtu ambaye hayuko vizuri kwa maana angependa kucheza na hali haipo hivyo na huenda ameendelea kuwa kimya mwenye maumivu ndani ambayo sasa yameanza kutoka nje na yataonekana kupitia vitendo vyake huenda hata bila ya mwenyewe kujua.

Kuna wakati una jambo linakukera, unakaa kimya bila kusema au kutumia njia sahihi kulitatua. Utaanza kufanya mambo ambayo hata yanaweza kuwakwaza wengine na wakikueleza unaweza kushangazwa kwa kuwa si tabia yako. Lakini ukimya wako hutengeneza hasira za ndani kwa ndani na zinapoanza kutafuta njia ya kutoka, njia sahihi inakuwa ni matendo.

Mo Ibrahim ni kati ya wachezaji vijana wa Kitanzania wanaochipukia na hakuna ubishi ana nafasi ya kung’ara na kufanya vizuri kama ataendelea kujituma kwa lengo la kufanya vizuri.

Binafsi nafurahishwa sana na Mo Ibrahim kwa kuwa mara nyingi alipopewa nafasi ya kucheza na Kocha Omog, aliitumia vizuri na kama unakumbuka msimu uliopita mwishoni aligeuka kuwa shujaa wa Simba katika mechi mfululizo mwisho mwa Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo Simba walifanikiwa kubeba ubingwa.



Nafurahishwa zaidi na Mo Ibrahim kwa kuwa anaonyesha ni kijana mwenye hamu kubwa ya kuisaidia timu yake. Ana hamu kuu ya kutaka kufanikiwa na anaonyesha anajiamini ndiyo maana anataka kucheza na tunakubali alipowahi kupewa nafasi alijitahidi.

Kamwe asiache kusema analichukia benchi, asione aibu kuwaeleza watu asingefurahia kukaa benchi na badala yake anataka kucheza. Hapohapo namshauri hana sababu ya kuonyesha anaonewa kwa kuwa hata aliyempa nafasi za msimu uliopita ni kocha huyo huyo ambaye hampi nafasi kwa sasa.
Bado ninaamini Mo Ibrahim ana nafasi kubwa ya kuitumikia Simba na kama ataendelea kuwa mvumilivu kidogo, siku itafikia naye atakuwa tegemeo la Simba na si mchezaji wa benchi tena.

Wakati anasajiliwa na Simba akitokea Mtibwa Sugar, hakuna aliyejua kuhusiana na uwezo alionao. Sote tunaweza kukubaliana kwamba ni mchezaji mzuri na anahitaji nafasi zaidi ya kucheza.



Tunaweza kukubaliana nafasi inatafutwa. Kama unamuona Haruna Niyonzima utaweza kukubaliana nasi ni mzoefu, kuna vitu anajua zaidi yako na vizuri ukajifunza zaidi na kuendelea kujituma zaidi.

Kulichukia benchi wala si kukimbilia timu nyingine. Sijajua kama umewaza kuondoka, lakini najaribu kuiangalia hali ilivyo na kama kweli utakuwa umewaza labda kuhamia Yanga, Azam FC, Singida United au kwingineko kwa sababu ya benchi, lazima ujue hata huko pia kuna benchi na lazima utagombea namba.

Unaona wakati Ibrahim Ajibu anatua Yanga, amekuta Donald Ngoma na Amissi Tambwe wakiwa majeruhi. Kama wangekuwa fiti hata kwake kusingekuwa na urahisi alioupata.
Jiulize Azam FC ingekuwa ile ya Kipre Tchetche na John Bocco, kama Mbaraka Yusuf asingepata nafasi aliyopata. Simba iliyopo inamchanganya kocha yeyote kwa kuwa wachezaji wengi ni wazuri lakini mwisho ambao huwa hawachoki kupambana mwisho huwa wanafanikiwa.

Bado Mo Ibrahim ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na lazima akubali kwamba kama mtu wa kwanza kuhama angekuwa Jonas Mkude lakini wako naye, amevumilia na sasa yuko Simba na anacheza.

Wakati mwingine vizuri kuchagua mfano wa karibu kuliko kusikiliza miluzi mingi ambayo mwisho itakupoteza. Watu wengi wanaozungumza kuhusiana na ishu ya Mo Ibrahim inaonekana kama anaonewa jambo analopaswa kuwa nalo makini sana hata akiamua kuondoka.





3 COMMENTS:

  1. Mwandishi huyu alimshaur Haji Mwinyi...kuangalia anavyowekwa benchi. Wewe tens unamshaur No abaki hapo kwa kuwa ni kijana.
    Nilipata shda sana kwenye ushauri wa Mwinyi. Hakuna timu inayosajil wachezaji 11 maana wote wangekuwa na namba za kudumu. Timu kama Simba au Yanga na zingne zinahtaj kikosi imara. Ukipata fursa shawishi benchi.
    Mo ni mzuri ila kikosi in kipana. Yanga kikosi si kipana. Ajib angepata tu mamba hats Tambwe na Ngoma wangekuwa fit

    ReplyDelete
  2. Maisha ni mzunguko Mwache aende akajaribu kwingine hakuna anejua ya kesho!mpira ndo kaz kwake.

    ReplyDelete
  3. No way out, find another team my young Mohamed, Manyika is now playing, Ajibu is now playing and other players from Simba are playing to their teams. Why not you? Bench is going to kill your talent, SHTUKA MDOGO WANGU! Dirisha dogo lisikupite.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic