November 1, 2017



Na Saleh Ally
MECHI ya watani wa jadi Simba na Yanga imepita huku ikiacha gumzo la kila aina na watu wakiendelea kuzungumzia mambo mbalimbali kama mfano au hadithi fulani.

Kama ilivyo kawaida ya mechi hiyo, watu baadhi hufurahi na wengine huingia kwenye majonzi au kama kawaida ya mashabiki wengi hulaumu hapa na pale kuonyeshwa kutoridhishwa kwao na wengine wakiendelea kufurahia.

Mfano baada ya mechi iliyopita, asilimia kubwa ya mashabiki wa Yanga wameonekana kuwa na furaha kubwa ikiwa ni pamoja na kurudisha imani kwa kikosi chao ambacho wengi wamekuwa hawakiamini.

Kwa kuwa kila gumzo limeingizwa kuwa gumzo na kujadiliwa, mimi nimeamua kulihamisha kidogo ingawa bado nitazungumzia kuhusiana na mechi hiyo ya watani.

Nataka kuzungumzia suala ambalo tumelisahau, suala la idadi ya watu waliojitokeza uwanjani siku hiyo wakati Simba na Yanga zikicheza kwenye Uwanja wa Uhuru ambao una uwezo wa kuingiza watu 23,000.

Kabla ya mechi watu wengi walikuwa na hofu kwamba ingekuwa vipi na watu wangeingia namna gani uwanjani hapo kwa kuwa idadi ilionekana isingetosha kwa vile watu wangependa kuiona mechi hiyo moja kwa moja.

Kawaida, mashabiki wa Simba na Yanga wameuzoea Uwanja wa Taifa ambao unachukua hadi mashabiki 50,000. Hivyo ilionekana upungufu wa zaidi ya watu 25,000 kwenye Uwanja wa Uhuru ni kama tatizo. Hilo likawa ni sehemu ya gumzo kabla ya mechi na wengi matarajio yakawa ni kuwepo kwa vurugu kwa kuwa watu wangelazimisha kuingia hata baada ya tiketi kuuzwa.

Wengine wakafikiri kuwa tiketi zingeuzwa zaidi na kusababisha tafrani ndani ya uwanja au nje siku hiyo. Lakini siku ya mechi mambo yakawa tofauti kabisa baada ya watu waliojitokeza kuwa wachache kuliko ilivyotarajiwa na kushangaza wengi.



Wakati mechi inachezwa, majukwaa yalikuwa yakionekana mapengo mengi tu. Hii haikuwa kawaida kwa kuwa kwenye Uwanja wa Taifa unaoingiza watu 60,000 ukiona mapengo, basi mara nyingi kama watu ni wachache maana yake wako angalau 35,000 uwanjani pale. Vipi Simba na Yanga katika kipindi hiki ushindwe kujaza watu 23,000 tu?

Hapa kuna mambo ya kujifunza na ndiyo maana nikaamua kulizungumzia suala hili ili kuzishauri Yanga na Simba kuacha kuishi na hisia za zamani kwamba zina nguvu na zikabaki kuamini hivyo katika kila jambo badala ya kubadili mambo kulingana na wakati.

Nitakupa mfano mzuri, wakati fulani nilishuhudia mechi kati ya FC Barcelona dhidi ya Celtic ya Scotland. Mechi hiyo ilikuwa inapigwa kwenye Uwanja wa Camp Nou jijini Barcelona, Hispania. Wakati naingia uwanjani, nilipokelewa na warembo waliokuwa wamevalia sare nzuri ambao walinipeleka hadi sehemu ambayo nilipokelewa na wahudumu wengine kwenda kunionyesha sehemu sahihi niliyotakiwa kukaa.

Niliona na watu wengine wakifanyiwa kama mimi kuhakikisha tunakaa katika sehemu zetu lakini wahudumu hao wakiwa ni wenye tabasamu la bashasha kama unapokolewa katika mkutano wa kiserikali na wewe ni kiongozi!

Hili lilinishangaza sana lakini kwa kunifurahisha. Lakini kabla sijaingia uwanjani hapo, tayari siku mbili kabla nikiwa jijini Barcelona niliona matangazo kwenye runinga, kwenye mabango ya barabarani na wakati mmoja niligawiwa kipeperushi kinachoonyesha mechi hiyo.


Nafikiri niliwahi kueleza hili; kwamba unakwenda kuwaona Lionel Messi, Luis Suarez, Neymar (wakati huo) lakini bado unakutana na matangazo ya kukushawishi kwenda uwanjani na kununua tiketi. Pia matangazo hayo yanaendelea mitandaoni.

Nilipofika Uwanja wa Emirates jijini London ambako nilishuhudia mechi ya Ligi Kuu England msimu huu kati ya wenyeji Arsenal dhidi ya Bournemouth ambayo walishinda kwa mabao 3-0. Pia niliona mambo yaleyale niliyoyaona Barcelona ambayo pia nimekutana nayo katika viwanja kadhaa.

Nimeendelea kujiuliza kwani Simba na Yanga wao ni nani hasa kwamba hawawezi kujitangaza au kufanya jambo la matangazo?

Jiulize, baada ya kuwa hakuna kiingilio cha Sh 3,000 au 5,000 na wakaanzia Sh 10,000, vipi hawakufanya matangazo angalau kuwaeleza mashabiki hali ilivyo, nini cha kufanya ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia watu usalama kuwa mambo yatakuwa safi au kuwaondoa hofu kuhusiana na zile hisia za kukosa tiketi au kuwepo vurugu?


Uongozi wa Yanga zaidi ndiyo ulihusika katika hili kwa kuwa walikuwa wenyeji wa mechi hiyo. Hawakupaswa kukaa kimya pekee badala ya kutembeza uhamasishaji wa mashabiki wao kujitokeza. Mkutano mmoja wa waandishi wa habari hautoshi.

Watu wanaona bora kukaa nyumbani kutokana na hofu ya mambo wanayosikia. Lakini wanapenda zaidi kwenda uwanjani kuliko kuangalia kwenye runinga lakini wanakuwa hawana uhakika kutokana na kutopata uhakika.



Mechi hiyo inapaswa kuwa funzo kwa Simba na Yanga na timu nyingine za ligi kuu. Lazima wajue wanafanyabiashara na biashara ni matangazo si ujanjauanja tu wa kutaka kupitia njia za mkato.

3 COMMENTS:

  1. SALEH KUWA NA KUMBUKUMBU KUWA YANGA WALIOMBA UTUMIKE UWANJA WA CCM KIRUMBA ILI KUWEZESHA WATU WENGI WAINGIE UWANJAN NA KUZIPATIA TIMU MAPATO,TFF KWA KUSHIRIKIANA NA SIMBA(HAPA NAMNUKUU HAJJ MANARA ALIYESEMA KWANINI MPIRA UKACHEZWE MWANZA NA SI DAR,TENA KWA KEBEHI KABISA AKIONA KUWA DAR SIMBA NI WAZURI ZAIDI KULIKO CCM KIRUMBA).
    KWA KUGUNDUA ILO LA TFF NA SIMBA,YANGA WAKAONA KAMA MBWAI NA IWE MBWAI HIVYO TULISHAJICHANGISHA ZAIDI YA 100,000,000/-TZS NA KUACHA MECHI ICHEZWE KAMA WANAVYOTAKA WAKUBWA(KIFUPI TULISUSA NA TUKAANDAA 500/-KWENDA KUANGALIA VIBANDANI).SASA WEWE SALEH USILAUMU SANA JAPO NAWE NI WALEWALE ILA KUNA WAKATI UNAKUWA NA MSIMAMO THABITI.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Mambo ya kama mbwai mbwai ni ya kizamani na mpira hauwezi kuendelea kwa sababu hiyo. Na sioni ni kwa jinsi gani wapenzi wa Yanga kwenda mpirani kwa uchache ingewasaidia Yanga uwanajani na hata kimapato. Vile vile kwa Simba. Sasa labda ni washabiki wenye mtazamo kama wako ni dhahiri hawana mtazamo wa kibiashara kuwa timu yao ingepata mapato kwa hivyo. Lakini mbaya Zaidi ni kuwa timu inakosa washabiki wa kuwatia moyo uwanjani. Hili ni muhimu na hata nchi zilizoendelea, wanaelewa kuwa mshabiki ni mchezaji wa 12. Upande wa biashara kama nilivyosema inajieleza wazi na kususa hakuwezi kuisaidia timu

      Delete
  2. Waishazoea kuishi kwny zama za giza so hawataki kubadilika hvo vlabu vyenu..

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic