Na Saleh Ally
NIKISEMA Klabu ya Yanga imemshindwa mshambuliaji wake, Donald Ngoma na sasa anataka kuwa mkubwa kuliko klabu yenyewe, ninaamini sitakuwa mbali na mawazo ya wengi sana.
Miezi kadhaa iliyopita kabla ya kuanza kwa usajili wa msimu huu unaoendelea sasa, nilieleza wazi kwamba sikuwa nikifurahishwa na wachezaji wa kigeni ambao walitaka kuwa wakubwa kuliko klabu yao na hasa wale wanaoichezea Yanga.
Nilieleza nilivyoshangazwa na wachezaji kadhaa kama Vicent Bossou ambaye ni mchezaji wa kimataifa ambaye alifikia na kukaa benchi, hakuwa fiti na Yanga ilifanya kazi ya ziada kuhakikisha anarejea katika kiwango.
Baada ya Bossou kukaa sawa, pale mshahara ulipocheleweshwa kidogo, alikuwa katika kundi la wachezaji ambao walitangulia kugoma. Nikaeleza kwamba niliamini hata yeye alikuwa akilipwa mapema mshahara wake na Yanga huku akiwa benchi. Sasa vipi angeshindwa kuonyesha uvumilivu pia kuwa sehemu ya ushawishi kwa wenzake kuhakikisha wanakuwa wavumilivu!
Niliporejea kwa Ngoma, nilikubali ni mchezaji mzuri lakini mwenye mbwembwe nyingi na Yanga inaonekana viongozi wamekuwa na hofu ya mashabiki.
Timu za Tanzania viongozi wake wengi ni waoga na wanahofia mashabiki. Hivyo mchezaji akijua kwamba anapendwa na mashabiki basi anaweza kufanya lolote dhidi ya viongozi kwa kuwa anajua hawatamgusa.
Ngoma amekuwa majeruhi, amekuwa akisafiri mara kadhaa kwenda kwao kutibiwa na wakati mwingine klabu ikalalamika kwamba uondokaji wake haukuwa sahihi.
Vituko kadhaa alifanya Ngoma msimu uliopita na mara kadhaa alilazimisha mambo na ikafikia Yanga kulalamika kwamba alikuwa nje muda mwingi na hakuonyesha kwamba kweli kuna juhudi anafanya kurejea uwanjani.
Ngoma akaingia kwenye mzozo na daktari akionyesha wazi kuwa hakuwa muungwana hasa kumshambulia daktari wa timu akimuonyesha hajui lolote na uongozi ukakaa kimya.
Kumbuka wakati kocha akiwa Hans van der Pluijm. Ngoma aliwahi kutuhumiwa kumpiga mchezaji mwenzake. Hakuna hatua zilizochukuliwa na jambo likawa siri na Yanga hawapendi kulizungumzia na kama hili lilikuwa ni kweli, basi ni sehemu kubwa ya udhaifu wa uongozi kwa kuwa unaweza kuwaficha mashabiki lakini wachezaji nao ni sehemu ya Yanga na hawatacheza Yanga milele lakini wakati wapo, mioyo yao inajua maana ya sahihi na si sahihi.
Sasa Yanga imekuwa ikilalamika pia kuhusiana na Ngoma ambaye baada ya mechi chache za mwanzo wa msimu, aliumia. Baada ya hapo vimeanza vituko vya kuondoka nchini na ondoka yake inaonekana ina walakini.
Ni kama uongozi haukuona sahihi naye amelazimisha. Ndiyo maana Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema akirejea atakutana na adhabu kwa kutofuata utaratibu sahihi.
Taarifa nyingine zinasema alimuaga kocha ingawa si sahihi mchezaji kuondoka kwa ruhusa ya kocha pekee kwa kuwa uongozi ndiyo unamuongoza hadi kocha mwenyewe.
Yanga ni klabu kubwa na inapaswa kuheshimiwa na anachofanya sasa Mkwasa ndicho sahihi na kama itafikia suala la kuadhibiwa bora lifanyike na umma ujue ameadhibiwa vipi.
Haipendezi kuwa na mtu asiyefuata utaratibu ndani ya klabu chini ya uongozi huku wengine wakifanya hivyo.
Si sahihi kutengeneza matabaka ya ubora na madaraja ndani ya timu moja. Yanga wanapaswa kuliangalia hili kwa jicho la mbali, la sivyo baadaye litawaletea shida.
Yanga haijawahi kucheza kwa Ngoma ikaonekana, lakini Ngoma anaichezea Yanga ndiyo maana anaonekana. Hivyo lazima kuwe na mtiririko wa heshima na utambuzi wa nani yuko wapi kwa kuwa Yanga ni kubwa kuliko Ngoma.
Viongozi wa klabu hizi nao wanapaswa kuwa na maamuzi sahihi bila ya woga. Lazima tukubaliane, kiongozi bora ni yule aliye tayari kuchukua uamuzi mgumu kwa ajili ya mabadiliko yanayokwenda katika maendeleo.
Kuogopa mashabiki watachukia huku vitu vinaharibika, nalo si jambo sahihi. Jambo la msingi ni kushikilia kilicho sahihi na kusisitiza utaratibu halali kufuatwa bila ya kujali ukubwa wa jina la mtu.
Hakuna timu yenye mafanikio bila ya upendo. Dharau huwa haikai pamoja na upendo. Kiongozi anayedharauliwa hawezi kuwa rafiki wa mchezaji, katika hali hii maana yake upendo umepotea na unapopotea maana yake hakuna amani na bila ya amani hakuna timu yenye mafanikio kwa kuwa inaua ushirikiano.







Peleka ngoma kwa mkopo fc platinum. Hana faida kwetu. Bora hats Per Sherman
ReplyDelete