December 29, 2017




NA SALEH ALLY
SOTE tunajua kwamba kumekuwa na upungufu wa mashabiki wanaojitokeza uwanjani kushuhudia mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara tofauti na miaka minne mitano iliyopita.

Kumekuwa na sababu mbalimbali ambazo zinaainishwa kwamba ndiyo chanzo kikubwa cha mashabiki wengi kutokwenda uwanjani kwa wingi timu zinapocheza.

Katika mkutano na wahariri wa habari za michezo nchini, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, naye aliligusia suala hilo na kuahidi kulishughulikia.

Lakini wakati analizungumzia, Karia naye alionekana ana mitazamo miwili kuhusiana na suala la watu kupungua viwanjani na kusababisha kupunguza kipato kwa timu nyingi.


Karia anaamini nusu watu hawaendi uwanjani lakini kwa alivyozungumza, pia anaonekana kuamini kwamba watu wanakwenda uwanjani na halina tatizo. Ingawa pia anasema wameliona wanalishughulikia.

Kwa kifupi tatizo lipo, tunaliona na halihitaji darubini kuliona na kama ukiniambia nimpe ushauri Karia na timu nzima ya TFF, basi nitasema wawe positive au chanya kwa maana ya kuamini lipo na linatakiwa kushughulikiwa.

Kama watakubali, basi kushughulikiwa kwake kunatakiwa kuwe si kwa muda mrefu sana ili kuweza kulipatia ufumbuzi kwa kuwa viiingilio vya mlangoni ni moja ya chanzo kikubwa cha mapato na chanzo za uhai wa klabu ambayo inakuwa inategemewa na timu.
Tunajua hapa nyumbani Tanzania, mapato ya mlangoni ndiyo 

kipato mama halafu kinafuatiwa na wadhamini halafu runinga. Kwa kipindi hiki imebadilika lakini bado kuna adhari kubwa katika kipato hasa kwa klabu kubwa ambazo zina mtaji mkubwa wa mashabiki.



Chanzo ambazo kinazungumzwa sana ni suala la Azam TV kurusha mubashara mechi za Ligi Kuu Bara kwamba kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo.


Jambo hili linapaswa kujadiliwa kwa uwazi na kulipatia ufumbuzi nini cha kufanya kwa kuwa tunajifunza kwa kuona sehemu ambako mpira umeendelea, mpira bado unaonyeshwa katika runinga na bado watu wamejaa kwa wingi uwanjani.

Sote tunajua, Azam TV wapo katika mpira kwa mazuri, biashara kwao lakini kutoa mchango wao kimaendeleo na tunakubali sote kwamba wanatoa msaada mkubwa na sote hatuwezi kukubali kuwakosa tena.

Lakini kwa kuwa wapo, tunawahitaji na uwepo wao unaonekana umesababisha jambo fulani tunaona limezaa kasoro, kipi kifanyike kutengeneza mambo yawe sawa huku tukiendelea kuwa na Azam TV.

Nimeona kumekuwa na kosa kubwa; kwamba wahusika wakiona kulijadili suala hilo ni kama kutaka kuishambulia Azam TV. Kuwa wazi na kujadili chanya kwa lengo la kusaidia kupata ufumbuzi nafikiri ni vizuri zaidi kuliko kufunika kombe.

Niliwahi kuwaelezea wasomaji wa gazeti hili kuhusiana na namna watu wanavyokwenda uwanjani katika viwanja mbalimbali vya soka kama vile Uwanja wa Camp Nou unaomilikiwa na FC Barcelona au Santiago Bernabeu mali ya Klabu ya Real Madrid.


Uwanjani ni sehemu ambayo mnaweza kwenda familia nzima, mazingira mazuri, watu wanaangalia mpira kwa raha na furaha kuu. Lakini kuna utaratibu mzuri na mnakaribishwa uwanjani kama ambavyo ukienda sinema au sehemu yoyote ya kistaarabu hapa nyumbani.


Lakini hapa nyumbani kila sehemu baunsa aliyenuna, anayesema kwa lugha kali na maneno machafu ili mradi kaambiwa alinde. Mlinzi kajisahau yuko pale uwanjani kwa kiingilio cha yule anayembugudhi ambaye anaweza kuchagua kuangalia kwenye runinga ya Azam badala ya kwenda kubugudhiwa uwanjani.

Uwanjani bado hakuna mazingira rafiki yanayoweza kumvutia mtazamaji ambaye anaweza kuona kwenda uwanjani ni starehe zaidi kuliko kuangalia katika runinga.

Hii ni sehemu tu ya sababu lakini ziko nyingi sana ambazo TFF na klabu zenyewe wanaweza kuzishughulikia na mwisho, watu wakaanza kwenda tena uwanjani na Azam TV ikiendelea kuonyesha mubasharaa.




1 COMMENTS:

  1. Siamini kuw kurusha mpira mbashara ndicho chanzo cha washabiki kupungua uwanjani, si kweli! Tatizo ni ushindani wa ligi na matokeo ya vilabu vinavyoshiriki. Mfano mzuri fuatilia msimu uliopita na huu (hasa mechi tano za mwanzo) kwa klabu ya Simba jinsi washabiki walivyokuwa wakijaa sana uwanjani halafu linganisha na miaka miwili nyuma. Jibu unalo!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic