December 25, 2017




NA SALEH ALLY
WAKATI fulani niliwahi kuzungumzia namna ambavyo nimekuwa navutiwa na wachezaji wa Yanga namna wanavyojituma uwanjani.

Sijawahi kupata jibu sahihi kwa nini hii imekuwa hivyo miaka nenda rudi na imeshakuwa kama utamaduni kabisa kuona wachezaji wa Yanga wakijituma sana hata kama wakati huo kuna njaa.

Wachezaji wa Yanga wana kasumba ya kutaka mafanikio halafu wakafikisha madai yao baadaye. Kwa wale wanaokumbuka, Yanga iliyotwaa ubingwa wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza kule Uganda, kikosi kiliondoka nchini kwa basi.

Wachezaji wa Yanga waliishi maisha ya kuunga na mechi ya kwanza wakakutana na SC Villa na kuchapwa mabao matatu. Lakini mwisho walipokutana na SC Villa wakati wa fainali, wakabeba kombe na kuwashangaza wengi.

Huko inaweza kuwa mbali sana, msimu uliopita, Yanga imebeba ubingwa ikiwa katika hali ngumu sana. Pamoja na presha ya Simba ambayo ilikuwa inautaka ubingwa kwa hali na mali, wachezaji wa Yanga waliendelea kupambana hadi mwisho na kuutwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Utamaduni huo ndani ya Yanga umekuwa ni wa kuambukizana, unaendelea kuchukua hatua moja hadi nyingine na sasa unaweza kusema unaendelea kuibeba Yanga. Kwa sasa Yanga namna ilivyo, hali ya kifedha inaonekana si nzuri.

Mwezi mmoja uliopita tulisikia wachezaji wanadai hadi miezi mitatu, viongozi walijitutumua na mwisho kufikia kulipa angalau mwezi mmoja au miwili. Baada ya hapo wachezaji wameendelea kupambana na deni linaongezeka.

Kawaida, kuna hofu na wachezaji hawawezi kulalamika hadharani. Lakini utaona matendo kwa baadhi na hasa wageni ambao wangependa mambo yaende kwa mpangilio sahihi hasa kwa wao kwa kuwa wanajua ni wachezaji wa kigeni.

Taarifa za kugoma kwa mshambuliaji Obrey Chirwa zimesikika, uongozi wa Yanga una nafasi zaidi ya kujua kusema kwamba yuko sahihi au la. Lakini kikubwa ambacho Yanga wanapaswa kujipanga kama wanataka wakae vizuri ni kuweka mikakati sahihi na mbinu ambazo zinaweza kuiingizia Yanga fedha.

Tunajua wana udhamini wa Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa ambao wanatoa mishahara. Lakini Yanga inahitaji fedha za uendeshaji, usajili na kadhalika ambazo kwa klabu kubwa kama hiyo haziwezi kuwa kidogo.

Inawezekana hata sasa Yanga inasota na mishahara kwa kuwa ilikopa ikatanguliziwa na wadhamini. Kama si hivyo basi kuna sehemu kuna tatizo na lazima lifanyiwe kazi.

Wachezaji wa Yanga, wanapaswa kupongezwa kutokana na juhudi zao bila ya kuwa na mishahara na wakaendelea kufanya vizuri hata kuwashinda wengine ambao wanalipwa vizuri.

Kuulaumu uongozi wa Yanga kwa sasa hasa kwa mashabiki wao itakuwa ni kupoteza muda, lakini uongozi nao kugoma kushauriwa au kuona kama unaonewa kila unaposhauri, pia ni kupoteza muda na kupoteza bahati ya kusikiliza na kujifunza.

Yanga inahitaji kuingiza fedha zaidi ya zile kutoka katika runinga, kutoka kwa wadhamini wao wakuu au zile nauli za Vodacom ambao ni wadhamini wa Ligi Kuu Bara.

Yanga inahitaji wadhamini wa uhakika wanaoingiza fedha za kutosha kutokana na ukubwa wa klabu na haitakuwa sahihi kujichukulia mdhamini ambaye anatoa ili mradi kwa kuwa anaamini ni ndogo.

Lazima kuwe na kitengo bora cha masoko ambacho kitaundwa na watu wanaoujua mpira na faida zake na wale waliosomea masuala ya masoko na wanalijua soko na soka la Tanzania ili waisaidie.

Viongozi wajikite katika mipango endelevu la sivyo kwa mwendo wanaokwenda, hali haitakuwa nzuri kuanzia katikati kwenda mwishoni na mwisho kabisa matokeo hayatakuwa mazuri na watapoteza kila walichonacho. 


1 COMMENTS:

  1. NAFUU NAWE UMELIONA....:::
    Hivi ndio vitu vya kuzungumza. Yanga inazidiwa na REHA FC kwa kuwa na wadhamini. Yanga inazidiwa na Mbao FC, Ndanda FC, Singida United ambao wameona Sportpesa wanaweza kuwaweka Nyuma alafu YARA Tanzania wakae kifuani. Hii ndio ubunifu. Tunahitaji watu wa masoko kwenye hivi vilabu vyetu.

    Yanga inashiriki Club Bingwa..sidani kama watakosa mdhamini wa kufanya mambo mazuri. Twende tumwambie mdhamini aweke nembo kwenye basi letu. Tunashindwa kumwambia hata Bin Slum, Serengeti Bia, NMB,CRDB, Kampuni ya Cement ya Dangote, Tanga cememnt, Twiga, na makampuni mengine. Kwanini timu hizi hazina watu wenye uweredi katika utafutaji wa wadhamini???

    Embu tukaribishe wadhamini...tufanye mchakato wa kuliweka hilo jambo Kisayansi. Mimi hilijambo nililisema tangu mwanzo mwa mwaka. Tunaenda mwisho mwa mwaka. Hakuna hata timu moja yenye kujiangaisha kwenye hilo. Inawezekana kwa kuwa hata baba yao TFF pale Ofisi sidhani kama wana mtu sahihi wa masoko.

    Embu tuwe wabunifu...hasa Yanga....wachezaji watakimbia na wengine wataendelea kujifanya wagonjwa. Na hawa wanaojifanya wagonjwa maisha yakitengemaa tutawaacha bila kuangalia ulifanya nini. Rafiki mzuri ni yule mnaejaliana hata kwenye matatizo

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic