Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, jana alishindwa kuhudhuria mahakamani katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili kwa mara ya pili mfululizo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa figo akiwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar.
Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu' wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha kiasi cha dola 300,000 za Kimarekani.
Katika kesi hiyo ambayo iliitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Makahama ya Kisutu, Victoria Nongwa, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Leonard Swai ambaye alikuwa akisaidiwa na wakili wa serikali, Peter Vitalis, aliiambia mahakama hiyo kuwa mshitakiwa namba moja, Evens Aveva ameshindwa kufikishwa tena mahakamani hapo kwa kuwa bado ni mgonjwa.
Baada ya Swai kudai Aveva bado anaumwa, hakimu Nongwa alimuuliza anaumwa kitu gani hadi wameshindwa kumfikisha makahamani, Swai alijibu kuwa mtuhumiwa anasumbuliwa na matatizo ya figo na amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Swai aliendelea kusema kuwa pamoja na hivyo, wamekashamilisha upelelezi kwa mshitakiwa namba mbili (Kaburu) baada ya kuomba kwenda kumchukua na kumhoji kwa mara ya pili, hivyo wanasubiria Aveva atoke hospitali ili waweze kuomba kumhoji tena ili kuweza kukamilisha upelelezi.
Kufuatia kauli ya Swai, hakimu Nongwa alilazimika kumuuliza Kaburu kama alihojiwa katika hali ya usalama na taasisi hiyo kwa kuwa hawakumpitisha kwake kuweza kumuona, Kaburu alijibu mahojiano yalikuwa ya amani na mazuri kwani aliweza kufurahia na kuongeza kuwa walimpa hadi chakula cha mchana, hali iliyosababisha watu kuangua kicheko.
Upande wa wakili wa utetezi ambao uliwakilishwa na Peter Warioba aliomba mahakama iruhusu kuendelea na kesi hiyo kutokana na shahadi wa pili kukamilisha upelelezi lakini halikuweza kukubaliwa na badala yake kesi hiyo imesogezwa mbele hadi Februari 8, mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment