January 26, 2018





NA SALEH ALLY
HATIMAYE lile suala la subira ya kocha mpya wa Simba sasa limepata jibu kwa kuwa Kocha Pierre Lechantre ameanza kazi yake rasmi juzi kukinoa kikosi chake baada ya kukamilisha kila kitu.

Lechantre raia wa Ufaransa, anasaidiwa na makocha wengine wawili ambao ni Masoud Djuma raia wa Burundi pamoja na Mohamed Habibi kutoka Tunisia ambaye amejiunga na Simba akiwa pamoja na Lechantre.

Kocha huyo Mfaransa alitaka kujiunga na Simba akiwa na mtu kama Habibi ambaye anajua nini ampe cha kufanya na amekuwa akifanya naye kazi katika sehemu mbalimbali. Uongozi wa Simba umekubali ombi lake lakini umebaki na Djuma ambaye ameonyesha ni kocha anayeiweza kazi yake.

Kuanza kazi kwa Lechantre na wasaizidi wake, maana yake Simba imekamilisha jambo moja inawezekana kabisa ni wakati mwafaka kuhamia katika jambo jingine kwa ajili ya muendelezo wa sahihi kinachotakiwa.

Unapokuwa na jambo fulani linalokusumbua, kawaida ukifanikiwa lazima kuna jingine linakuja mbele. Simba hawawezi kuwa na shida ya kocha pekee. Badala yake kuna mengine ya maendeleo yanafuatia na lazima wayatekeleze.

Kwa kuwa kama uongozi wametekeleza hilo moja, kunakuwa na majukumu mengine wanaendelea nayo kama kumuunga kocha huyo mkono katika masuala kadhaa kama atataka vifaa husika, uwanja wa mazoezi, kambi nzuri na kadhalika.

Simba wasitegemee kuona matunda bora kutoka kwa Lechantre na wasaidizi wake wakati wao hawatakuwa na ushirikiano na kocha huyo au kupuuzia mambo ambayo atawaambia anahitaji kwa muda fulani ambao atawaeleza.

Kumekuwa na tabia, kocha anaingia kwa mbwembwe na viongozi watamuona kama lulu. Wakimzoea, basi anakuwa wa kawaida na mambo yanakwenda kama zamani.

Huo ni upande wa viongozi, kwa mashabiki wa Simba kwa kuwa wamekubali mabadiliko na walionekana wangependa kupata kocha mpya atakayeendana na ukubwa wa Simba, sasa, Lechantre huyo hapo.

Wakati mwingine kama ni kwa kuangalia pekee, unaweza ukawa unaona kocha huyo Mfaransa huenda ni mkubwa kuliko Simba.

Huenda zaidi hadhi yake itaonekana kwa ubora wa kazi yake na kizuri ambacho mashabiki na wanachama wa Simba wanapaswa kukubali ubora wa kocha hauwezi kuanza kuonekana kwa siku moja au mbili, lazima muda unahitajika.

Angalia mjumuiko wa benchi la ufundi, makocha watatu, mmoja wa Afrika ya Mashariki, mmoja Afrika Kaskazini na mwingine Ulaya. Hawa ni watu ambao wanatakiwa kuunganisha “Chemistri” yao ili kufanya kazi kwa umoja.

Muunganiko huo unatakiwa pia kuunganisha hiyo “Chemistri” ili kufanya kazi na wachezaji vizuri, waelewane na kufanya kitu kwa pamoja na umoja.

Zingatia kuna suala la lugha ambalo Simba wamepata kama bahati ni kwamba, makocha wote watatu wanazungumza Kifaransa kwa Ufasaha kwa kuwa nchi zote tatu zinatumia lugha hiyo moja, yaani Ufaransa wenyewe, Tunisia na Burundi.

Lazima kuwe na subira katika mabadiliko huwa kuna matatizo. Tuliona muda mchache wa mabadiliko ya Kocha Djuma, wako tayari walianza kulalama na kusema anawachanganya afukuzwe.

Baada ya mambo kukaa sawa na kuanza kuzinyanyasa timu nyingine, walewale wakageuka na kuanza kumpongeza. Kweli hii ni tabia ya mashabiki wengi lakini kujitambua zaidi ya hapo, ni jambo zuri zaidi.

Kama mashabiki wataanza papara mapema hasa kama katika ubadilishaji wa mambo Lechantre atakuwa amekosea jambo, basi ujue watamchanganya zaidi na mwisho ataonekana hana lolote na kuondoka mapema.


Kikubwa ni kocha huyo kuhakikisha naye anakuwa makini katika mabadiliko yake ili kuhakikisha Simba inakwenda kwa mwendo wake ilionao kwa sasa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic