January 1, 2018



KAMA kutakuwa na mtu mwingine naye amekuwa akipiga kelele sana za kuwashawishi wadhamini kujitokeza na kusaidia mchezo wa soka, basi kwanza nianze kumpongeza.

Binafsi nimepiga kelele kwa zaidi ya miaka kumi nikieleza namna ambavyo wadhamini wanaweza kuubadilisha mpira wa Tanzania kama watajitokeza.

Lakini nimekuwa nikipiga kelele za ushawishi kwa wadhamini hao pia kuwaeleza namna wanavyoweza kuzitangaza bidhaa zao kupitia mchezo wa soka na michezo mingine.

Nimetumia mifano mingi ya Ulaya na kwingine ambako mpira umeendelea kwa kuwa sikuwa na ujanja zaidi ya kufanya hivyo kwa kuwa ndiyo sehemu sahihi ya kuwaonyesha wafanyabiashara wa Tanzania.

Kuanzia mwaka juzi kumekuwa na muamko mkubwa wa wadhamini kujitokeza na kudhamini hasa katika mchezo wa soka.

Kampuni ya kuuza matairi ya Bin Slum Tyres Ltd, nimekuwa nikiipongeza kwa kuwa ndiyo iliweka rekodi ambayo haijafutwa hadi leo kwa kuzidhamini timu tatu za Ligi Kuu Bara na zote zikiwa si Simba au Yanga, yaani timu kubwa.

Bin Slum waliidhamini Mbeya City, Stand United na pia Ndanda FC, jambo ambalo lilikuwa ni faraja kubwa katika kusaidia maendeleo ya mpira wa Tanzania na hii ilisaidia timu hizo kuendelea kubaki katika Ligi Kuu Bara hadi leo. Lakini tumeona baadaye makampuni mengi yamejitokeza kama SportPesa ambayo pia inadhamini timu tatu kubwa za Yanga, Simba na Singida United.

Lakini kuna Cowbell wanaodhamini Mbao FC, Ruvu Shooting na kadhalika na utaona ni jambo jema kuona timu ambayo inaonekana ni ya jeshi nayo inapata mdhamini, wakati awali lingekuwa jambo gumu sana.

Kampuni ya kuuza mafuta ya Puma, nayo ipo inaidhamini Singida United. Kampuni ya masuala ya kilimo ambao ni Yara nao wameidhamini klabu hiyo. Mkataba wao ni wa mwaka mmoja.

Katika hali ya kiufundi kibiashara utaona kuna wadhamini wengi wamedhamini kwa mwaka mmoja mmoja wakionyesha wanataka kujifunza jambo.

SportPesa pekee kwa kuwa wanajua nguvu ya Simba na Yanga, wao wameshikilia kwa muda mrefu zaidi wakijua wanawahitaji.

Lakini karibu kila kampuni iliyodhamini klabu nyingine, utaona wanajaribu kuangalia upepo na kutaka kupata uhakika wa namna hali inavyotakiwa kuwa. Kama kweli watafaidika au la au baadaye itakuwa ni hasara kwao ili waondoke na kuendelea na hamsini zao.
Kwa klabu huu ni mtihani mkubwa na wanatakiwa kujifunza kwa kusoma alama za nyakati kwamba kilichopo mbele yao ni chakula bora na msaada lakini bado hakina uhakika wa kuendelea kukaa mikononi mwao kwa kuwa wanaowapa bado hawajapata uhakika.
Umuhimu wa wanachotoa ndiyo msaada wa maisha ya klabu hizo kwa kuwa hazina vyanzo vya uhakika kuingiza fedha. Sasa je, nini wafanye kuendelea kuwabakiza?

Kwa kuwa wadhamini wameanza kujitokeza, jambo la kwanza muhimu kabisa ni kuwalinda kwa kuwaridhisha waliopo na hii ni kuhakikisha yaliyo katika mkataba yanatimizwa.

Yatatimizwa vipi? Kwa kuhakikisha kila mlichokubaliana kinafanyika kwa usahihi wa asilimia 100 ili mdhamini aone kuwa anafikia kile alichokitaka na faida ya kutoa fedha zake. Kumbuka, anachozungumza mfanyabiashara mwishoni, huwa ni faida.

Faida ya kuwalinda waliopo ni kuutangaza zaidi mchezo wa soka kwa kuwa itasaidia kuwavuta wengine ambao walikuwa kando na hawaamini kuwa wanaweza kupata faida katika mpira. Lakini ukiwaachia waliopo waondoke, maana yake ni kuwaambia wengine huku hakufai.

Hii maana yake ni hivi; viongozi wa mpira wasifurahie kupokea fedha za wadhamini halafu wakaishi kama hawajadhaminiwa. Au wasichukue fedha za wadhamini halafu wakaona kama ni haki yao kupewa, mtarudi mwaka 1947 halafu muanze kulialia tena.




1 COMMENTS:

  1. Samahani saleh hivi inaweza kunisaidia jinsi ya kupata watu wakuwatangazia kwenye blog blog yangu ni www.skuliblog.blogspot.com

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic