January 12, 2018



Na Saleh Ally
MZAMBIA Obrey Chirwa amekaa nje ya kikosi cha Yanga kwa zaidi ya wiki mbili kwa kuwa alikuwa na mgomo akitaka kulipwa fedha zake za usajili ambazo Klabu ya Yanga ilishindwa kutimiza kwa wakati kama walivyokubaliana.


Baada ya kurejea kwao Zambia akiwa ameomba ruhusa, siku za kurejea zilipowadia, Chirwa aligoma kurudi akishinikiza alipwe fedha zake la sivyo asingerudi.


Pamoja na kwamba uongozi wa Yanga ulifanya juhudi kubwa kutaka kulifukia suala hilo, baadaye ukweli ulijulikana kwamba Chirwa ameamua kubaki Zambia akijihusisha na kilimo hadi hapo atakapolipwa.


Kurejea kwake, ingawa imekuwa siri, inaonyesha atakuwa amelipwa angalau kiasi fulani. Nakukumbusha, lazima kuna wachezaji ndani ya Yanga ambao watakuwa wanadai lakini waliendelea kubaki na kuitumikia timu hiyo.


Chirwa ana haki ya kudai na lazima tukubali hili. Tukirudi kwenye msingi wa msimamo wake, lazima tutakuwa na maswali ambayo nimewahi kuuliza na leo nitaongeza kadhaa ili kupata majibu.


Kwamba, kama aligoma kwa wiki mbili na ushee, Yanga ilikuwa na majukumu kadhaa kama yale ya Kombe la Shirikisho, ligi na Kombe la Mapinduzi. Akishalipwa fedha alizokuwa anadai, mwisho wa mwezi atachukua mshahara wakati hakuwa akiitumikia Yanga?


Pili; Wakati kuna wengine wanadai na walibaki wakaendelea kuipigania Yanga, kurejea kwake na siku moja tu akapelekwa Zanzibar na kujiunga na timu, viongozi hawaoni wameonyesha udhaifu kwa kuwa wanawavunja nguvu wengine waliobaki?


Sasa nakuja katika hili, amerudi wenzake wakiwa nusu fainali, wanapigania kwenda fainali. Moja kwa moja kapata nafasi ya kukaa benchi na mwisho amepiga penalti ya mwisho ambayo inaiondoa Yanga. Tunaweza kusema ni mambo ya mpira lakini nani mwisho amekosea na kuitoa timu?

Jibu ni Chirwa na kama atasamehewa hiyo ndiyo maana ya mchezo na kujenga kukubali masuala ya kiuanadamu kwamba kila mmoja wetu anakosea na ukitaka kuishi na watu vizuri, basi lazima ukubali makosa yao pia. Au nifupishe, uvumilivu unaweza kuwa dawa zaidi ya muarobaini.

Juhudi za wenzake wote zimeishia mguuni mwake. Waliziba pengo lake na kumpigania lakini amerejea ameonyesha si mtu makini. Na kama utasema kukosa penalti ni jambo la kawaida na Yanga wanapaswa kuelewa na kumvumilia, mimi nitakuuliza vipi yeye alishindwa kuwavumilia?

Unakumbuka Portsmouth ya England, wachezaji wake waliipigania timu bila mishahara tena hiyo ni England, walifanya hivyo hadi mwisho wao. Leo Chirwa anaonyesha jeuri na mwisho anarejea na kupewa nafasi haraka, halafu mwisho anakosea na kosa lake linaitoa timu mashindanoni!



Viongozi Yanga, wanapaswa kuwa makini na kuangalia mambo yanayohusisha saikolojia ya wachezaji wao. Wanapaswa kupima mambo kabla ya kufanya na lazima wajue kama viongozi hawapaswi kuwa waoga na wao ndiyo wanaopaswa kusimamia nidhamu na kuwaonyesha wachezaji kama Chirwa na wengine wanaojiona ni wakubwa kuliko klabu kuwa lazima washikilie nidhamu, ambaye atakuwa hataki, abebe mabegi yake aende na Yanga itatumikiwa na wengine na itafanikiwa. Ndiyo maana ilifika nusu fainali bila ya Chirwa, Donald Ngoma na wengine. 

Viongozi, acheni uoga, acheni kupapatikia wachezaji wageni au wale wanaoonekana walifanya vizuri kwa kuwa hilo ndiyo jukumu lao, hawaisaidii Yanga.

2 COMMENTS:

  1. NIMEKUELEWA LAKINI SIJAKUELEWA.....::::
    Ukimuuliza Chirwa kwanini alipiga penati au kwanini alicheza ile mechi utakuwa unamuonea. Hii sidhani kama ni kwa Chirwa imetokea hata huko mbele kwa watu wanaojua mpira ni nini yamewakuta. Kukosa penati ni kitu kingine na fitness ni kitu kingine. Swali kwanini alicheza na kupiga penati tuwaulize benchi la ufundi. Yeye majukumu yake ni kuambiwa afanye alilotakiwa kulifanya. Jiulize "Je angepiga na kupata kungekuwa na cha kuongea???"...mpira ndivyo ulivyo...hata penati zingepigwa siku...wiki hata mwezi mzima ila mwisho wa siku mshindi angepatikana. Na mshindi huyo ni URA ya Uganda basi.Sidhani kama tunatakiwa kumtafuta mchawi ndio maana Afisa Habari wa Yanga Mr. Dismas Ten Kasema "mechi imeisha na lazima kukubali matokeo"...hakuna haja ya kuendelea na stori. Mbona sisikii kuondolewa kwa MLANDEGE, JAMHURI, MWENGE,JKU, TAIFA JANG'OMBE au hata ZIMAMOTO???"kwa kuwa si habari ile???.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Jamani kiukweli kabla ya kutoa comments kwa hoja iliyotolewa ni vyema tukaisoma mara kadhaa hiyo na tukaelewa vizuri mlengo wa mtoa hoja. Tukiaza kujibu hoja kwa mtazamo wa kishabiki na hasira za kufungwa hatutapata mabadiliko ya uzembe wanaofanya viongozi wetu. Nafikili Saleh Jembe yuko sahihi kuwa viongozi wetu wanao udhaifu mkubwa sana katika management ya hizi timu zetu hasa Simba na Yanga. Nakumbuka awali palitolewa taarifa kuwa Chirwa alipewa ruhusa maalumu na angerudi mapema kuja kuendelea na majukumu yake,baada ya kutokea msiba wa mtoto wa RWANDAMINA viongozi walitoa taarifa kuwa anasubili ahudhurie mazishi ya huyo mtoto wa boss wa bench la Ufundi.Baada ya mazishi Chirwa anaonekana Instagram amepost picha yuko shamba anapalilia shamba lake well and good kwa kujiongezea kipato.Na taarifa zaidi zikaendelea kusambaa kumbe amegoma kurudi hadi alipwe pesa yake ya usajili iliyobaki. Siku mbili baadaye Katibu mkuu wetu Charles Mkwasa akajibu hoja honestly nanukuu "Nikweli Chirwa anaidai Yanga kiasi cha Pesa ya usajili kama walivyo wachezaji engine Mwisho wa Kunukuu. Kama mnakumbukumbu nzuri ndugu zangu wakati anasaini palitolewa taarifa kuwa alilipwa yake yote ya usajili na pesa hiyo ilitolewa na Yusuf Manji akiwa Mwenyemiti. Swali langu ni kwamba alipwa pesa ipi kama sio ya usajili? Kama Yusuf Manji alitoa mkwaja wote katika usajili ule pesa nyingine ilienda wapi? Viongozi tupeni majibu. Nikirudi kwenye hoja kucheza ile, kiukweli hakupaswa kucheza kwasababu hakuwa na timu kwa zaidi ya wiki mbili, pili hakuwa physically sambasamba na wenzake,tatu Psychologically hakuwa tayari kwasababu ametoka kwenye msuguano na viongozi halikadhalika alikuwa shamba jua na yeye mvua na yeye utimamu wa mwili kimchezo lazima upotee, kumbuka amefanya hayo wakati anajua waliobaki kufa na timu nao hajalipwa hiyo kibinadamu lazima imsute. Kwaujumla anayepaswa kulaumiwa kwa mtokeo yale sio wachezaji bali viongozi wetu.Ni mtazamo wangu kama mchambuzi wa michezo

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic