January 9, 2018




NA JOSEPH MSAMI, NEW YORK
Simba msipotulia , mtalikoroga
Ni kawaida kwa timu za Simba na Yanga na kwa ujumla timu nyingi kuchukua hatua pale mambo yanapoenda mrama mathalani vipigo mfululizo, kukosa kombe kwa muda mrefu, kufungwa na timu yenye uwezo mdogo na kwa ujumla matokeo mabaya na yasiyotarajiwa.

Kwa bahati mbaya sana Simba na Yanga za Tanzania zinakabiliwa na shinikizo kubwa la mashabiki na wanachama jambo linaloweza kuzifanya kuamua mara nyingine hata kumfukuza kocha kwa vile tu kelele zimezidi. Uamuzi kama huo waweza kuwa namatokeo chanya u hasi kwa timu husika.

Juma hili limekuwa baya kwa Simba kufuatia kufungashwa virago kwenye kombe la Mapinduzi baada ya URA ya Uganda  kuifunga kwa bao 1-0. Awali Simba ilipokea kipigo cha bao hilohilo moja kutoka kwa Azam ya Tanzania.

Vipigo hivyo vimeleta tafrani na kwa yeyeote anayefahamu soka la Bongo,si ajabu ukasikia Simba wanasaka mchawi, yaani kuwachnguza nani wametufungisha na hata kuanza kujadili uwezo wa kocha na ikibidi kumfukuza. 

Wachezaji waweza kuathirika
Katika hatua kama hizi, mara kahdaa wachezaji wamekuwa watuhimiwa namba moja. Huonekana wasaliti au wahujumu kwa namna moja au nyingine .Sisemi kwamba hakuna wachezaji wanaohujumu timu. 

Lakini swali la kujiuliza ni kwamba hivi kwanini timu hizi au soka letu kila unapofanya vibaya kuna mchawi? Siku moja nikiwa nimesononeka sana baada ya timu ninayoishabikia huko Ulaya kufungwa, nilimpigia simu rafiki yangu akaniambai maneno ambayo hata leo nayakumbuka. Alisema, “No King rules forever” Akimaanisha hakuna mfalme anayetawala au kudumu milele. 

Huwa najiuliza hivi vilabu vikubwa duniani kama vile Real Madrid ambayo hivi karibuni ikicheza na hasimu wake mkubwa Barcelona ilichapwa kipigo cha aibu ikiwa nyumbani cha 3-1, wao hawapigiwi kelele tulizozoea kuzisikia kwetu? Mbona hawafanyi haraka kufukuza na kusaka wachawi? 

Ikiwa timu hizo zisingejenga utamaduni wa uelewa kuwa mpira hudunda na kwamba kuna matokeo ya suluhu, sare, kufungwa na kufunga, nadhani kungekuwa na mtiti ndani ya timu na labda mchezaji ambaye ni tumaini kama Christian Ronaldo ambaye siku ile hakufanya alichotarajiwa, angeonekana kafanya figisu.

Wakati fulani wachezaji kama vile beki wa Yanga Kelvin Yondani,  (aliyewahi kuchezea Simba) na hata kiungo Nurdin Bakari aliyekuwa Simba kabla waliwahi kutuhumiwa kuzihujumu timu kwa kile kilichoitwa wana mapenzi na timu pinzani.

Miongoni mwa waathirika wakubwa ni Henry Joseph wa Mtibwa, mchezaji aliyewahi kuwa tegemeo la timu ya Taifa na kapteni wa timu hiyo. Wakati akiwa Simba alilazimika kucheza kufa na kupona kuzishinda sauti na kejeli za mahaba yake na Yanga. Kila ilipofika wakati wa mchezo kati ya watani wa jadi Henry alijikuta ana wakati mgumu kwani kosa la kawaida  lilimgharimu vilivyo.

Nimeeleza kwa urefu hayo kwakuwa nataka kusisitiza kuwa yawezekana kabisa kuna wachezaji wasaliti, lakini ikiwa hisia zitatokana na shinikizo la mashabiki, matokeo yake huharibu timu na kupoteza mwelekeo.

Simba yaweza kuboronga isipomakinika.
Baada ya kutolewa kwenye kombe la Mapinduzi, ikiwa benchi la ufundi la wekundu wa msimbazi halitatambua wajibu wa tathimini ya kitaalamu na kuchukua hatua kurekebisha mapungufu, na kuruhusu fitna, wataenda nazo ligi kuu, na huo huenda ukawa mwanzo wa timu kufanya vibaya na kulikosa kombe ambalo kwao kwa sasa ni A must win season

Yaani ni msimu ambao kwa namna walivyowekeza kununua wachezaji na kuanza kwa kasi, wameshajiongezea deni la kubeba ubingwa .

Mitandao ya kijamii, wanachama na mashabiki.
Naelewa vyema kwamba timu hizi yaani Simba na Yanga na nyinginzeo zina wanachama kwa mujibu wa katiba na sheria. Sitaeleza leo kwa kirefu, faida na hasara ya kuwa na wanachama, sina maana ni jambo baya la msingi ni nguvu waliyo nayo na mipaka yao.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba pamoja na wanachama na mashabiki kupiga kelele nyingi kupitia mitandao ya kijamii na njia nyinginezo, benchi la ufundi na uongozi wa Simba una wajibu wa kujali mustakabali wa timu kwa kuzingatia na kusoma alama za nyakati. 

Kweli, wanachama hawapaswi kupuuzwa kwa kuwa ni wanahisa, wakati huo huo ukiamua kwa shinikizo waweza kufanya uamuzi mbaya. Kwa mfano maoni kwamba chanzo cha kuboronga kwa Simba ni kufukuzwa kwa aliyekuwa kocha Joseph Omog yaweza kuwa sahihi au siyo sahihi, lakini kuamua kumrudisha yaweza kuleta mgawanyiko mkubwa na kuongeza sintofahamu zaidi ndani ya klabu.

Kocha Irambona Masoud Djuma
Nimesoma lawama za mashabiki na pengine wanachama kwa kocha msaidizi Irambona Masoud Djuma ambaye ndiye kashikilia benchi la ufundi kwa sasa, kwamba mfumo wake haueleweki na si imara katika ulinzi na pengine wakashinikiza kuwa afukuzwe. 

Hili ni kosa ambalo ikiwa Simba watajaribu kulifanya nabashiri watapotea na kama usemvayo usemi wa Kiswahili vita vya panzi furaha ya kunguru, mahasimu wao Yanga watajinufaisha na mgogoro huo na kuwaondoa kwenye muelekeo wa ushindi na pengine hata kushinda. Timu nyingi hasa za nchi zilizoendelea kisoka hufanya uamuzi huo pale inapobidi na hakuna namna nyingine, kwani huelewa madhara yake katika mfumo wa uchezaji na wachezaji wenyewe.

Kwa maoni yangu kufungwa mara mbili mfululizo yaani dhidi ya Azam na URA kwenye kombe la Mapinduzi kuwe chachu kwa Simba kuimarisha uwezo wake kuelekea ligi kuu ambayo inaongoza, badala ya kutumia muda mwingi kusaka mchawi eti kwa kuwa Yanga wamefanya vyema badi kuna mkono wa mtu. 





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic