Na Saleh Ally
WEWE ni shabiki wa soka, na unaipenda sana klabu yako na klabu yako ni mabingwa watetezi wa Tanzania Bara, basi leo acha tuzungumze.
Kokote uendako duniani, hakutakuwa na shabiki wa soka anayekubali kuishabikia timu ambayo haifanyi vizuri, lakini kuna mashabiki wengi wapo katika klabu hazifanyi vizuri.
Huenda hili linaweza kuwa swali la kwanza kujiuliza, kama kweli klabu, timu yake haifanyi vizuri, vipi huyu shabiki anaendelea kubaki na kuishangilia?
Kunaweza kuwa na majibu mengi sana, lakini jibu sahihi ni hivi; hakuna timu haijawahi kupoteza na hakuna timu haijawahi kufanya vibaya. Kuna vipindi vya kupanda na kushuka katika kila timu unayoijua duniani.
Kwamba kuna wakati ipo juu na wakati ipo chini. Inapopanda kunakuwa na raha ya kupita kiasi kwa mashabiki wao lakini kuna kipindi itashuka na ndicho kipindi cha kero kwa mashabiki wake.
Wanaobaki ni wenye mapenzi ya dhati, wale watu unaoweza kusema wana mioyo ya chuma kwa kuwa mapenzi yao kwa timu husika ni yale ya dhati.
Kila mmoja anajijua ilikuwaje akaanza kushangilia au kushabikia timu fulani. Huenda ni sababu ya baba au wazazi wake, huenda sababu ya mchezaji fulani, rangi fulani na kadhalika.
Kila shabiki amewahi kuonja uchungu wa kutokuwa na furaha au utamu wa furaha mambo yanapokuwa ni mazuri au magumu.
Kipindi hiki, lazima kitakuwa kigumu kwako wewe shabiki wa Yanga ambaye huenda hujawahi kuambiwa kwa kuwa kila anayekuambia anahisi atakuwa anakusaliti au utamchukia kwa kusema kwake ukweli.
Kwa sasa Yanga iko katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu. Tofauti yake na kinara Simba ni pointi saba. Hili si geni, kumbuka msimu uliopita, Simba walifikisha hadi tofauti ya pointi nane. Sasa, nani anaweza kuongoza Yanga yenye uimara wa kufanya hivyo?
Sitaki kuingia katika kundi la waoga wanaotaka kupendwa tu hata kama wanaona ukweli wao unaweza kuwa msaada, hivyo wanachagua kuwa kimya. Kipindi hiki kinaweza kisiwe kizuri sana kwa mashabiki wa Yanga kama ilivyozoeleka lakini pia lazima tukubali, haiwezi Yanga ikawa na kero kila siku.
Mfano, wakati Azam FC inaonekana ni tishio, inaweza kukwama kwa Yanga na furaha ikawa kwa Wanajangwani kesho Jumamosi. Kama watapoteza na hali ilivyo, wakiyachukulia matokeo hayo kama tatizo lisilobadilika, machungu yao yataendelea.
Yanga imebadili mfumo, kitu kibaya wengi hawataki kukubali kwa kuwa wanazungumza au kufanya mambo kishabiki bila ya kuangalia uhalisia wa mambo.
Chini ya Mwenyekiti Yusuf Manji, Yanga ilikuwa na mfumo wa aina yake. Mfanyabiashara huyo alitengeneza mfumo wenye heshima, usikivu na ubora wa mambo katika matumizi na usiku mkubwa kutoka kwa kile alichoamini sahihi.
Heshima ya Manji, leo haiwezi kuwa ya Clement Sanga kwa kuwa kama kuna fedha ilikosekana, mara moja Manji alitoa kama msaada au mkopo na Yanga ikaendelea kufanya mambo yake inavyotaka.
Hakuna fedha kwa ajili ya usafiri, Manji anatoa, hakuna fedha sababu ya usajili, Manji anatoa. Kumbuka, wakati hayo yakifanyika, furaha ya Mwanayanga ilizidi kusonga mbele na kuwa ya leo, kesho, keshokutwa na zaidi.
Kwa sasa mambo ni tofauti, umeona fedha za usajili zikiwemo za Donald Ngoma, Yanga ililazimika kwenda kukopa kwa wadhamini na baadaye ikawa tatizo kubwa katika kusubiri ipate fedha nyingine.
Hii ililazimisha kuchelewa kwa mishahara na rundo la figisu. Kukiwa na taarifa hizi, lakini viongozi wa Yanga nao kwa kuwa ni kazi yao kuitetea klabu yao, wakawa wanapambana kuziba mashimo.
Katibu Mkuu Charles Boniface Mkwasa anaweza kuwa mhanga wa mambo mengi, lakini mwisho watakuwa wanamuonea kwa kuwa hiki ni kipindi kigumu kuongoza Yanga kuliko kingine.
Fedha za mishahara bado ziko juu na wakati akiwepo Manji ingekuwa rahisi kusukuma mambo kwa kuwa kiongozi mkuu anaweza kujifichia aibu yake ya kuepuka kuwa na deni la mshahara miezi mitatu. Angalau kuchelewa mwezi mmoja.
Kwa sasa Mkwasa atatoa wapi fedha zote hizo ili kuziba mapengo? Nakukumbusha kama Manji bado angekuwa Yanga, leo huenda uamuzi wa kuachana na wachezaji wasio na faida kwa Yanga ungepita. Leo haiwezekani kwa kuwa wakiachwa, stahiki zao zitalipwaje? Kuhusiana na usajili mpya nani atatoa fedha?
Yanga haiwezi kumtegemea Manji milele. Hiki ndiyo kipindi cha mpito kubadili mfumo kutoka ule wa Manji na kuanzisha mwingine ambao utasonga mbele bila ya Manji.
Lazima mkubali, hii inahitaji muda na inahitaji mabadiliko hata kama ni taratibu. Nani asiyejua kuwa kipindi chochote cha mabadiliko huwa na maumivu yake?
Ndicho wanachopitia Yanga.
Viongozi wanaweza kupambana kupunguza maumivu na ikiwezekana kufanya jambo kubwa zaidi, hili linawezekana. Hili pia liko kwa wachezaji kama wakiamua.
La sivyo, maumivu yatakuwa ya milele na hakutakuwa na nafuu kwa kipindi kirefu. Hivyo kwa shabiki wa Yanga, lazima kujiandaa na kuweka akiba ya mambo ingawa, Yanga haiwezi kuwa matesoni milele.
SIAMINI KWA STEVE YANGA ILA NAAMINI KWA ALLY YANGA...:
ReplyDeleteKwa mtu kama Steve Yanga (Marehemu) angekuwepo angesema..maumivu ya mashabiki ni makubwa kuliko wachezaji. Sikuwahi kufata mkumbo kuishabikia Yanga..ila ndio timu iliyonitoa kutoa Ubungo hadi Jangwani kwa miguu kwenda kuangalia mazoezi wakati Simba SC walikuwa jirani kabisa pale Viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. wakati Athman China analetwa kwenye mazoezi ya Timu ya Taifa pale Chuo kikuu na Marehemu Gulamali. Hii yote ni mapenzi ya kweli kwa timu. Kwetu hakuna shabiki wa mpira ni mimi hasa. Siogopi kutetea mbele ya watu na kukubali madhaifu yaliyopo kwa sasa. Hakuna shabiki wa kweli kama wa Arsenal. Huu ndio mpira.
Wewe ni Shabiki wa Madrid...je wewe ni shabiki wa Chelsea???ukijua hizi timu zinapopitia ndio utajua mpira maana yake nini. Chelsea ina bosi lakini inapita kugumu...Madrid ina bosi lakini inapita kugumu. Haya ni mapito na mpira ndio ulivyo. Unakuwa na fedha lakini wachezaji wabovu au wamechoka.