January 29, 2018




Na Saleh Ally
INAWEZEKANA hii ikawa ndiyo Ligi Daraja la Kwanza bora zaidi kuliko nyingine zilizopita licha ya kwamba kumekuwa na taarifa nyingi za uonevu.

Wikiendi ijayo itakuwa ndiyo hitimisho la ligi hiyo kufikia mwisho wa maneno yote na wakati zinatakiwa timu sita kupanda, ni moja tu ambayo imejulikana.

Ligi hiyo ipo katika makundi matatu yaliyogawanywa katika A, B na C na timu moja tu ya kundi A, ndiyo imeshajulikana kuwa imepanda daraja. Hiyo ni JKT Ruvu ambayo hadi baada ya mechi 13, imejikusanyia pointi 34.
Zinatakiwa timu nyingine tano kupata sita zitakazopanda Ligi Kuu Bara lakini hakuna hata moja yenye uhakika na safari yake hiyo hadi wikiendi ijayo mambo yatakapokamilika.
Ile hofu ya timu fulani itapendelewa kwa kuwa Rais Wallace Karia ni shabiki wake kama tulivyosikia kwenye Coastal Union au Biashara Mara kwa kuwa inatokea mkoa wa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura naona sasa inafutika.

Sote tunakubaliana kwamba kama kweli ingekuwa hizi timu zinapendelewa, basi leo zingekuwa zimejihakikishia kupanda na leo tungekuwa tunasubiri timu nyingine tatu tu.

Lakini hadi sasa, hazina uhakika wa kupanda na lazima zifanye vema katika mechi za mwisho za makundi. Bado unaona, timu iliyopanda ya JKT Ruvu, haina kiongozi wa juu wa TFF ambaye ni shabiki wake, badala yake imepanda kutokana na ubora.

Inawezekana katika sehemu baadhi kulikuwa na uonevu na inaonekana timu zilizofanya vurugu sana ni zile ambazo zinamilikiwa na majeshi na hasa polisi.

Zimelalamikiwa sana kutokana na kuonyesha ubabe au askari kuwasumbua mashabiki wa timu nyingine bila sababu jambo ambalo pia si zuri lakini mwisho inaonekana wazi kwamba ubora wa soka ndiyo jibu la nani atafanya vizuri.

Kikubwa sasa ni kwa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF kuhakikisha linafanya kilicho sahihi katika mechi za mwisho za ligi hiyo.

Raha zaidi kila kundi litakuwa na nafasi ya kumaliza mambo yake kwa wakati wake na zitakuwa mechi zote zikichezwa kwa wakati mmoja.

Hii itaisaidia TFF kufanya kile ambacho ni sahihi kwa wakati mwafaka hasa kuhusiana na usimamizi wa uhakika na baada ya hapo watakwenda kusimamia mechi za kundi jingine kwa uhakika zaidi.

Mechi zote za makundi zitachezwa siku moja lakini kwa kila kundi. Mfano Februari 2, ni kundi B, Februari 4 ni Kundi C na Kundi A linamalizia Februari 5.

KUNDI A:
Katika Kundi A, tayari JKT Ruvu inayoongozwa na Kocha Bakari Shime imeshapanda tena kwa zaidi ya uhakika.

Bado inaonekana timu mbili zina nafasi ya kukwea Ligi Kuu Bara ambazo ni African Lyon na Friends Rangers ya Elly Mzozo. Kila mmoja inategemea atacheza vipi karata zake.

Lyon wako nafasi ya pili wakiwa na pointi 24, wanatakiwa kushinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Kiluvya ambayo haina presha ya kupanda wale kushuka na Rangers wanakutana na Mvuvumwa ambayo tayari imeteremka, nao wanatakiwa kushinda. Kama wote wakishinda, Lyon anasonga ila asiposhinda, Friends akashinda, anapanda.

Februari 5
Kiluvya United vs African Lyon
Friends Rangers vs Mvuvumwa
JKT Ruvu vs Mshikamano
Ashanti United vs JKT Mgambo

KUNDI B:
Hadi sasa hakuna timu yenye uhakika, JKT Mlale na KMC ziko nafasi ya kwanza na ya pili na zote zina pointi 25, lakini Coastal Union iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 23. Hizi zote zina nafasi ya kupanda.

Ugumu upo kwa Mlale na KMC, hawa wanakutana wote, atakayeshindwa hapa, halafu Coastal akashinda basi atapanda Coastal na aliyeshinda.

Coastal ambaye anacheza na Mawenzi akipoteza, wao hata wasicheze, Mlale na KMC watakuwa wamepanda na mechi ya mwisho Mlale wanaoongozwa na Danny Mrwanda katika ushambulizi watakuwa nyumbani.

Coastal walikosea hesabu katika mechi iliyopita baada ya kupata sare nyumbani, sasa wana kazi dhidi ya Mawenzi ambayo ina uhakika wa kubaki Ligi Daraja la Kwanza kwa asilimia 90 kutokana na mabao ya kufunga na kufungwa hata kama itapoteza.

Februari 2
Mawenzi Market vs Coastal Union
Mufindi United vs Polisi Tanzania
Mbeya Kwanza vs Polisi Dar
JKT Mlale vs KMC

KUNDI C:
Hapa napo uhakika ni wa shida kidogo, Biashara Mara wanaongoza wakiwa na pointi 27, wanafuatiwa na Alliance Schools wenye pointi 25, sawa na Dodoma FC.

Huenda huku ni kugumu zaidi kwa kuwa Biashara anakutana na Transit Camp ambao hawana presha ya kushuka wala kupanda. Lakini timu mbili zenye pointi 25 zina presha zaidi kwa kuwa Alliance atakutana na Oljoro wasio na presha lakini watataka heshima huku Dodoma FC wakikutana na Toto African ambao wanataka kushinda ili wabaki dhidi ya ndugu zao Pamba ya Mwanza.

Hivyo utaona utamu ulivyo unaotokana na ushindani na kama kweli kulikuwa na fitina, TFF na Bodi ya Ligi lazima watupe jicho na masikio katika siku tatu za mwisho za ligi hiyo ili imalizike kwa uhakika bila ya uonevu au fitina za upendeleo.

Februari 4
Alliance Schools vs JKT Oljoro
Biashara United vs Transit Camp
Rhino Rangers vs Pamba SC
Dodoma FC vs Toto Africans.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic