January 29, 2018



NA SALEH ALLY
KAMA kuna kitu unaweza kukishangaa kabisa ni pale utakapowasikia wachezaji wa Kitanzania wakifanyiwa mahojiano mara baada ya mchezo.

Huenda hata wanaowafanyia mahojiano pia wamekuwa na upungufu mwingi sana ambao pia wanapaswa waufanyie kazi.

Lakini binafsi leo ninalenga moja kwa moja kile ambacho wamekuwa wakijibu wachezaji au hata makocha wakati mwingine wanapokuwa wakihojiwa.

Mazungumzo yao yamekuwa yanashangaza na yanajenga picha ambayo kama kweli kuna suala la kuboresha basi lifanyike mara moja ili kuwa na wachezaji walio katika mwendo unaoeleweka.

Mchezaji anaulizwa: “Kipindi cha kwanza mlipoteza nafasi nyingi za wazi, tatizo lilikuwa nini?”
Anajibu: “Yaani ni mambo ya mpira tu, unajua mpira ndivyo ulivyo, lakini tumejitahidi tumepata sare tunashukuru kwa kweli.”

Mchezaji anaulizwa: “Mlikuwa mkimlalamikia mwamuzi sana, labda kipi alichokosea.”

Mchezaji anajibu: “Unajua aliwapendelea sana, hakuna uamuzi wa vile duniani, yaani imetushangaza sana.”

Wachezaji si kucheza pekee na timu nyingi ambako mpira umeendelea zinafanya utaratibu wa mafunzo “In house training” kuwasaidia wachezaji wao pale wanapokwenda kufanya mahojiano au wanapokuwa wanazungumza katika hadhira ya watu.

Tukubali kuwa mchezaji ni kioo cha jamii, si kwamba kazi yake itakuwa ni kucheza mpira pekee. Kuna wakati anatakiwa kwenda kuzungumza na watu kwa ajili ya kuwahamisha au mambo mengine muhimu ya kimaisha. Wakati mwingine anatakiwa kukutana na watoto ambao wanahitaji ujuzi mkubwa kuzungumza nao na kuwafaidisha.
Katika mpira wa Kikapu Marekani yaani NBA, wachezaji wanaanza kufundishwa vyuoni lakini wanapoingia katika timu za NBA, wanapata wataalamu ambao wanawafundisha kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji na namna ya kuendesha biashara zao.

Hawa wa kwetu hawabahatiki kuipata nafasi hiyo kwa kuwa uongozi au wao wenyewe hawawezi kuliona kuwa hilo lina umuhimu zaidi ya kucheza na kushinda pekee kwa kuwa hajui kama umri unakwenda na unataka akiba mbele.

Kwa kuwa hilo la biashara ni gumu, suala la mchezaji kuzungumza kwa uhakika katika jamii hasa anapokuwa anaonekana katika runinga au kusikilizwa katika redio, ni jambo ambalo linatakiwa kupewa nafasi na kutiliwa mkazo.

Mchezaji anapozungumza kama unamsikia kwa mara ya kwanza inakushitua, unakuwa huamini kama ni yeye kwa kuwa unamchukulia tofauti kutokana na utendaji wake mzuri uwanjani.


Niliwahi kuzungumza na mchezaji mmoja, nikamueleza kwamba hilo ni muhimu sana. Yeye akasema kazi yake ni kucheza mpira na si kuzungumza. Sikushangaa kwa kuwa najua wachezaji wengi wa Tanzania wanaamini hivyo.

Hawajui michezo ya sasa si zamani tena kwa kuwa wachezaji wanatumika kama nyenzo ya uhamasishaji katika maisha ya kawaida na hasa kwa vijana wanaochipukia.

Mchezaji anaweza kukaribishwa hata katika semina ya uhamasishaji ili awaeleza watu namna alivyopata mafanikio kutokana na alipo kwa wakati huo na alipokuwa kabla. Ni rahisi watu kumuelewa au kuelewa anachoelezea kwa kuwa ni mtu wanayempenda, wanamuamini na kumfuatilia.

Lakini kinachoniumiza kichwa, hata wachezaji wa nchi jirani tu kama Uganda, Kenya na hata Rwanda ambayo naiona ni nchi ndogo kwetu, wanapozungumza kunakuwa na tofauti kubwa sana na wachezaji wetu wa hapa nyumbani wanapohojiwa au hata mbele ya kadamnasi.

Mpira wa sasa si ule wa enzi ya kina Gibson Sembuli, mambo yamebadilika sana. Ndiyo maana unawaona akina Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na wengi wanashiriki katika mambo mengi sana hasa ya jamii kwa niaba ya klabu zao au wao.

Hivyo ni lazima na wachezaji wetu walichukulie hili kama sehemu ya kazi yao, wajifunze na kuwa imara wanapotokea mbele ya wanaowaamini kwa kucheza mpira wanaotarajia kusikia ya uhakika kutoka kwao. 



1 COMMENTS:

  1. lakini kanuni nyingine inasema kwamba unapozungumza na media ni sana na usiku wa kiza (media is like a galax which you can not control) wakati mwingine pia ukumbuke mchezaji anaongea baada ya mechi huku network yake ikitegemeana na matokeo husika kwani kichwa kinakua kimechaji barabara baada ya pilika za uwanjani na mzunguko wa damu unakua haujatulia sawa sawa .........hapa nitoe mfano wa Himid Mao, uzungumjai wake mara nyingi hutawaiwa na matokeo ya mchezo, timu ikishind ni muongeaji mzuri wa kutulia lkn tazama jazba yake juzi baada ya timu kufungwa na maneno aliyoongea huenda ni zaidi ya nukuuu za hapo juu

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic