January 8, 2018




NA SALEH ALLY
TUMEZUNGUMZA suala la wachezaji kuangalia wafanye nini baada ya maisha yao ya mpira. Haliwezi kuwa tena jambo geni kwao au kwetu sisi, lakini kila kukicha lina nafasi nyingine ya kuzungumzwa.

Nasema nafasi ya kuzungumzwa kwa kuwa inawezekana kimetokea kitu fulani ambacho kinatoa nafasi ya kuanzisha mjadala mwingine kuhusiana na jambo hilo.

Nimeona nyota wa zamani wa Arsenal, Lukas Podolski akiwa amefungua duka la kuuza vyakula aina ya kababu, chakula maarufu kinachotengenezwa katika nchi za Kiarabu na hasa Uturuki au zile za Kihindi za India na Pakistani na nyinginezo.

Podolski amefungua duka hilo kwenye mji aliozaliwa na kukulia wa Koln huko Ujerumani. Mashabiki zaidi ya 1,000 walijitokeza kumuunga mkono.

Kumbuka, Podolski ambaye amecheza soka Ujerumani, England na Uturuki si masikini na bado anaendelea kujiingizia kipato kupitia mpira lakini hajaacha kujitengenezea maisha ya baadaye baada ya mpira.



Nikiwa jijini Koln nilipata nafasi ya kutembelea duka lake la kuuza vifaa vya michezo lakini nikapelekwa katika mgahawa mwingine maarufu wa kuuza ice cream ambao pia ni mali ya Podolski.

Sote tunajua Cristiano Ronaldo ana hoteli kubwa kwao Madeira, Ureno na pia katika Jiji la Lisbon ambako alikulia akiichezea Sporting Lisbon.

Wayne Rooney ana majumba ya kupangisha nchini Marekani na kadhalika. Kwa kifupi wachezaji wengi wa Ulaya na hata Afrika ambao wameinua vichwa vyao wakijua kuna kesho au kuna maisha baada ya soka, wamekuwa wakijiandaa.

Kawaida, mchezaji ana muda wa miaka 10 kamili kucheza soka la ushindani, akiwa juu au maarufu lakini mingine ni huwa anapambana ili ajulikane kama amepita katika mfumo wa soka la vijana.

Akiingia katika miaka hiyo 10, fanya ana miaka 20 au 22, maana yake atajulikana hadi atakapokuwa na miaka 30 au 32. Hapo ndipo anaanza kuteremka mlima kwa miaka mingine mitano, atakuwa amefunga 15 ikiwa 10 ni ushindani na iliyobaki ni kumalizia.

Miaka hiyo 15, baada ya hapo mchezaji anafanya nini? Jiulize alijiandaa kuhakikisha anakuwa vizuri kabisa katika kiwango cha maisha ya ushindani?

Kumbuka kwa wachezaji pia kunakuwa na ugumu kwa kuwa waliishi kama nyota. Watu maarufu lazima maisha yanakuwa na tofauti.

Wachezaji wetu wanaliona hili na wanalifanyia kazi? Au ndiyo wanaona kama wao haliwahusu na badala yake linawahusu wachezaji wa Ulaya pekee?

Maisha ni maisha, Ulaya na Afrika na kila upande wana yao lakini suala la maandalizi ya maisha ya baadaye halina eneo kwa kuwa kote watu wanaishi.

Wachezaji wanaweza kulalamikia mishahara lakini tunajua wako wengi wanaopata fedha nyingi wakati wa usajili na hata mishahara yao mikubwa kuliko wafanyakazi wa benki, wanasheria, madaktari, walimu na kadhalika. Je, wanajiandaa?

Wachezaji pamoja na mishahara, wana posho za mazoezi, posho za safari, fedha kama wakishinda, sare au kufungwa. Kwa kifupi wana marupurupu kibao. Je, wanakuwa wamejiandaa na maisha ya baadaye?

Kama Podolski kafungua mgahawa wa mamilioni, hapa nchii mchezaji anaweza kufungua kwa kiwango cha Tanzania na ukawa mzuri, akatumia jina lake kusaidia biashara yake na watu wakaenda kama wanavyomuunga mkono Podolski.
Kama unaona unaweza kufungua biashara hata mkoani kwenu ni vizuri zaidi na ikaendelea kukua wakati ukimalizia mpira wako.

Msitafute visingizio, wachezaji mna nafasi ya kufungua biashara zenu wakati mkicheza soka na baadaye mkajiendeleza baada ya kustaafu ili kuondoa lile kundi la wachezaji ambao kazi yao ni kulaumu walisahauliwa au maisha ni magumu wakati wao walizisaidia klabu au timu ya taifa wakati wanajua wakati wanacheza walikuwa wanalipwa na fedha zao wakazichezea pia.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic