Na Saleh Ally
INAWEZEKANA kabisa viongozi wa Simba au Yanga wasingependa kuambiwa mambo kadhaa kuhusiana na klabu zao kwa kuwa wanaamini kufanyiwa hivyo ni kusakamwa bila sababu za msingi.
Wengi wa viongozi hao wamekuwa wakiona kuelezwa ni kusalitiwa au kuzisakama klabu hizo kwa lengo la kuziangusha.
Wanachokuwa wanajisahau ni kwamba klabu hizo wao wamepewa dhamana tu, si mali zao ni mali za wanachama na wanazozifanya ziwe kubwa au maarufu ni mashabiki na asilimia 99 ni Watanzania. Nataka kusisitiza, Yanga na Simba ni mali ya Watanzania na viongozi wamepewa dhamana tu.
Binafsi nimekuwa nikikerwa sana na mwenendo wa wachezaji wengi wa kigeni na inawezekana kabisa kuna mambo mawili, wao ni tatizo au tatizo kubwa ni viongozi wetu.
Nasema hivyo, kupitia mambo kadhaa ambayo yameanza kujitokeza kuanzia katikati ya mwaka jana ikiwa ni siku chache baada ya kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu Bara 2017-18.
Tangu msimu umeanza, wachezaji wa kigeni hasa walio Yanga na Simba ndiyo wanaoongoza kwa kukaa nje ya uwanja wakiwa na sababu nyingi, chache za msingi na nyingi si za msingi.
Lazima tukubali kwamba wachezaji wa nje ya Tanzania wanalipwa fedha nyingi sana ukilinganisha na wachezaji wazalendo. Ajabu, wengi wao wamekuwa hawairudishi ile fedha kwa kuwa hawana faida na klabu.
Muda mwingi badala ya kucheza, wanakuwa wamesafiri kurejea kwao, iwe Zambia, Zimbabwe, Rwanda, Uganda na kadhalika, lakini kutakuwa na sababu ya kuwafanya wasafiri na kukaa muda mrefu bila ya uongozi kusema lolote.
Suala la majeruhi limekuwa juu zaidi kwa wachezaji wa kigeni, wengi wameendelea kuwa nje kwa muda mrefu na hapa ndipo nilisema huenda viongozi wanakosea kusajili wachezaji wakongwe wengi kutoka nje ya Tanzania.
Wachezaji hao, wanapata “pancha” kila mara kutokana na umri wao, jambo ambalo viongozi wa Yanga na Simba wanapaswa kuliweka wanapokuwa wanafanya usajili kwa kuwa, kuwa na mchezaji mwenye miaka zaidi ya 35 halafu ukawa unamlipa mshahara mkubwa huku akiendelea kubaki jukwaani kwa muda mrefu, ni kuwavunja nguvu wengine, jambo ambalo ni baya sana.
Mshambuliaji Donald Ngoma hajatulia katika kikosi kwa muda mrefu. Tokea msimu umeanza, hajafikisha hata mechi saba za mashindano akiitumikia Yanga, kumbuka alimaliza msimu namna hiyo. Sasa anaendelea kubaki nje baada ya kurejea nchini akitokea kwao.
Atarudi lini na faida yake ni ipi? Ajabu siku akicheleweshewa mshahara kwa mwezi mmoja, utasikia amegoma? Sasa Yanga nayo imgomee? Obrey Chirwa naye amegoma, yuko kwao Zambia na Yanga wanahaha kumbembeleza arejee. Swali langu, akilipwa naye atailipa Yanga mechi ambazo hakuitumikia wakati amesusa? Je, mshahara wa kipindi ambacho alisusa ataudai? Kwa nini viongozi wa klabu wanakuwa waoga kuchukua hatua sahihi?
Angalia upande wa Simba, ingawa wanataka kufunika kombe, timu yao wakati inatolewa ilikuwa inahitaji msaada mkubwa wa akina Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi ambao tunaelezwa ni majeruhi lakini hakuna rekodi za kutosha kwamba kuumia kwao kunawalazimu kukaa nje kati ya wiki tatu hadi takribani miezi miwili sasa.
Simba iliwanunua wachezaji hawa wa nini, wote karibia wamekuwa na safari za kurejea nyumbani mara kwa mara na wakati mwingine unaona walistahili kusubiri kipindi cha mapumziko kufanya hivyo.
Viongozi watakuwa wakilaumu chinichini, wakisikia wachezaji wamesemwa, watalazimika kuwatetea hata ambapo kuna makosa na hii ni hofu ya kuepuka kuonekana wao ni watu wabaya mbele ya mashabiki. Maisha ya Yanga na Simba kwa viongozi ni kuridhisha au kuwafurahisha tu mashabiki!
Hakika kuna mambo mengi yanaonekana kufanywa na wachezaji wa kigeni, wakiwa na uhakika hawatafanywa kitu huenda kwa kuwa wamewateka mashabiki na wao ndiyo vipenzi vyao au kwa kuwa wanajua Tanzania ni sehemu ambayo wageni wanapapatikiwa sana, hivyo wanaweza kufanya lolote bila ya bugudha.
Kikubwa kwa viongozi lazima watengeneze mikataba bora, maana wakati mwingine suala la mchezaji kujitunza ni lake na si la uongozi. Mchezaji anatakiwa kuitumikia timu kwa zaidi ya asilimia 90 ili kupata anachotakiwa kulipwa.
Tusikubali fedha nyingi kwenda kwa wageni ambao wanatoa mchango mdogo ndani ya timu. Tunawapenda na kuwahitaji, lakini lazima nao wafanye kazi na si hadithi nyingi ambazo tunaona kabisa zingeweza kuwa tofauti na faida kwa klabu hizi za Watanzania.
Tuwe wakweli, wanayofanya wachezaji wa kigeni ndani yake yanaonyesha hawako ‘siriaz’. Kama angekuwa anafanya mchezaji mzawa, naamini hatua zingeshachukuliwa na tayari angeshatangazwa ni msaliti au anaivuruga timu.
Viongozi lazima wawe imara, au kwa mikataba bora, kuwa wachunguzi kabla ya kusajili, kujadili suala la umri wakati wa malipo au kusajili lakini pia lazima kama nidhamu ya timu, basi iwe kwa wachezaji wote.
Kuendelea kuwakweza wachezaji wa kigeni haitakuwa inasaidia mpira wetu. Kama kuna mashabiki watalalamika wakati mmefanya sahihi, itakuwa ni sahihi zaidi kusimamia kilicho sahihi.
0 COMMENTS:
Post a Comment