Na Saleh Ally
NAONA halitakuwa jambo baya inapofikia wakati tukawa tunakumbusha mambo kadhaa kwa nia njema na kuwaonyesha wale ambao wanaamini kukosolewa ni uadui wawe wanajifunza.
Kawaida nimekuwa nikiandika mambo kwa nia njema kabisa, ninakosoa bila ya ubaguzi wa kupendelea upande na bila ya kumhofia yeyote kwa kuwa tu ninaamini nia yangu ni nzuri kwa mpira wa Tanzania ambao unatoa ajira kubwa kwa vijana na wengine.
Kuna watu kazi yao imekuwa ni kukatisha wengine tamaa na hasa watu kama mimi ambao hukemea mambo yanayoonekana kuwaangusha au kuuangusha mpira wa Tanzania.
Leo nakumbusha kuhusiana na Juma Mahadhi, ambaye alijiunga na Yanga akitokea Coastal Union. Hakika ni kijana mwenye kila kitu kama utazungumzia kipaji na hata umbo bora linalomuwezesha kucheza mpira vizuri.
Lakini tangu ametua Yanga, Mahadhi ameshindwa kuonyesha cheche na badala yake ikawa ni benchi kila mara na alipopewa nafasi ya kucheza akashindwa kuonyesha kama anastahili.
Niliandika makala ya kwanza kueleza namna anavyofeli na namna anavyoshindwa kujikwamua. Makala ya pili nilieleza kwamba nitaendelea kuandika hadi hapo nitakapopata jibu amefanikiwa au amefeli. Nilieleza namna ninavyomuona na ninavyoamini kwamba anastahili kufanikiwa ingawa amekuwa haitumii nafasi hiyo vizuri.
Ajabu kuna watu wengi walinishambulia sana kwamba nilikuwa ninamsakama hasa baada ya kuzungumza kuwa amejikita kwenye starehe ambazo si ndoto yake na wanaoshiriki nao starehe ni watu ambao kama ataanguka hawatakuwa naye tena na watahamia kwa mwingine na yeye wataendelea kumzungumzia vibaya.
Leo Mahadhi, amebadilika na kuomba radhi, nilichoeleza kwamba anachofanya si sahihi naye amekubali hilo na amewaomba radhi Wanayanga akiahidi kujirekebisha, jambo ambalo ni zuri sana na ameonyesha kweli ameng’amua anachokosea.
Ameonyesha amejua kosa lake ambayo ni hatua kubwa ya mtu kwenda katika mabadiliko na hili litakuwa pigo kwa wale waliojifanya rafiki zake na wakaona kumtetea asielezwe ukweli ndiyo kumsaidia, kumbe walitaka kuendelea kumdidimiza na mwisho wangemmaliza kabisa.
Kama mnakumbuka niliwaambia kwamba mnaweza kuwa mna mawazo ya Yanga pekee, lakini Mahadhi ni faida ya taifa zima la Tanzania kama atabadilika na kujua anachotakiwa kufanya ikiwa ni pamoja na kujituma akicheza kwa juhudi kuu tena kwa dhati.
Vizuri sana ameweza kuinuka na kugundua kuwa amejificha katika rundo la watu wasiomtakia mema, vizuri amejua anawatendea si haki wanaoipenda klabu yake ambayo inamlipa mshahara na kumpa heshima ya kuvaa jezi yake ambayo watu wanalilia angalau siku moja wafanye hivyo lakini hawajaipata bahati hiyo au hawakuwahi kupata.
Tayari Mahadhi amezungumza kwa maneno, lakini tayari ameanza kuonyesha kwa vitendo baada ya kufunga mabao mawili wakati Yanga ikiitwanga Mlandege katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi linaloendelea Zanzibar.
Tunapaswa kumpongeza, kwamba ameanza kwa maneno na ameonyesha kwa vitendo. Kuonyesha amebadilika, kwa mechi moja au mbili, bado haitakuwa sawasawa, badala yake anatakiwa kuendelea kufanya vizuri zaidi akijituma na kujitutumua kuhakikisha anafanya vema zaidi na zaidi.
Mafanikio hayapatikani kwa mechi moja au mbili, kwa siku moja au mbili na badala yake anatakiwa kufanya tena na tena ili kufanikisha kilicho sahihi.
Hakika Mahadhi bado ana safari ndefu na wale ambao wanamzunguka wana kazi kubwa. Wazazi na ndugu zake wanaweza wakawa na uchungu, basi wanapaswa kumuelezwa ukweli unaouma kwa njia nzuri na kumshauri abadilike.
Kwa kuwa sasa anaonyesha anakwenda kubadilika, basi waungane naye kumtia moyo na kumhimiza kwamba mambo yanaweza kubadilika ili aendelea kubadilika na mwisho afanye vizuri.
Urafiki au undugu mzuri pia ni kuelezana ukweli na si kufichiana mambo au kuzuia ukweli. Mahadhi unaweza kuendelea kubadilika, hadi ulipofikia ni pazuri lakini hapajatosha.
0 COMMENTS:
Post a Comment