February 28, 2018



Benchi la ufundi la Klabu ya Azam chini ya kocha wake mkuu, Aristica Cioaba, raia wa Romania, limeweka bayana kwamba litataka kuutumia mchezo wao dhidi ya Singida United kwa ajili ya kupata pointi tatu ambazo zitawarudisha katika mstari wa kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu.

Azam inayoshika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, wikiendi hii watawakaribisha Singida United iliyo mikononi mwa kocha Hans van Der Pluijm raia wa Uholanzi, katika mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar.

Kocha Msaidizi wa Azam, Nassor Idd Cheche, amesema kwamba licha ya kutambua watakumbana na ugumu wa hali ya juu kutoka kwa wapinzani wao, wao wanajipanga kupata matokeo mazuri baada ya kushindwa kupata matokeo ya kuridhisha kwenye michezo yao mitatu iliyopita.

“Bado hatujakata tamaa kwamba ndiyo tumeukosa ubingwa wa ligi kuu, tunaamini kwamba lolote linaweza kutoka kwa wapinzani wetu, baada ya kutokuwa na matokeo ya kuridhisha ndani ya michezo yetu mitatu iliyopita malengo yetu ni kupata ushindi mbele ya Singida United ya Singida.

“Tunajua kwamba utakuwa mchezo mgumu kwetu kwa sababu wapinzani wetu wako vizuri na wanaonyesha uwezo wa hali ya juu lakini hilo halitutishi, tunataka kuutumia mchezo huu iwe daraja kwetu ya kuturudisha katika reli baada ya kushindwa kupata matokeo katika michezo yetu mitatu ya nyuma,” alisema Cheche.


Katika mchezo wa kwanza timu hizi zilipokutana zilitoka sare ya kufungana bao 1-1 kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic