NA SALEH ALLY
SIKU moja tu baada ya Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino kuondoka nchini, nilisikia jambo ambalo liliendelea kunikumbusha kwamba katika soka bado kuna mambo mengi tunapaswa kuyafanya kwa ajili ya kuboresha mambo.
Ujio wa Infantino na wajumbe wengine waliofanya mkutano wa Fifa hapa nchini kama Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Ahmad Ahmad lilikuwa jambo zuri na hakika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanapaswa kupongezwa kwa hilo.
Ujio wao umekuwa na faida kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kukutana na serikali na kujadili mambo kadhaa kama ujenzi wa viwanja na kadhalika.
Infantino na Hamad walikutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kujadili mambo ambayo yatakuwa na faida kubwa kwa Tanzania.
Wamekubaliana kufanya ujenzi wa viwanja kadhaa kwa maana ya sehemu nzuri ya kuchezea.
Hili ni jambo jema na hata serikali kuzungumzia michezo na hasa soka ni jambo zuri kwa kuwa mara nyingi nimeandika kuzungumzia kwamba serikali imekuwa haiingii moja kwa moja katika michezo na kuiacha iwe kama sehemu ya akiba au ziada tu.
Wale ambao wamekuwa wakiingia katika michezo zaidi ni wanasiasa ambao hutaka kuitumia kwa ajili ya kujipigia kampeni na baada ya hapo wanaendelea na maisha yao mengine michezo ikiendelea kudorora.
Wakati Infantino ameondoka siku moja tu, nilisoma katika gazeti hili yale malalamiko ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga kuhusiana na kasoro zilizo kwenye Uwanja wa Kambarage.
Uwanja huo uko katika eneo la Majengo katikati ya mji huo, ni mmoja wa viwanja vikongwe na kikubwa kilichokuwa kikilalamikwa ni vyoo kutokuwa katika hali nzuri tena ni vya shimo.
Jambo hili lilinirudisha nyuma sana kimawazo, nikakumbuka namna ambavyo tuliomba Fifa kutusaidia lakini nikajiuliza hili suala la vyoo nalo tunasubiri Fifa watupe msaada?
Kwangu naona hii ni aibu na kweli kuna sehemu ambazo serikali sasa inapaswa kutoa agizo na mambo yafanyiwe kazi kwa kuwa wahusika ambao wameaminika kusimamia nyanja kadhaa wamekuwa ni wazembe na wasiotaka kubadilika.
Kambarage ni mali ya Chama cha Mapinduzi, lakini lazima tukubali hiyo ni mali ya Watanzania kwa kuwa hata CCM ni ya Watanzania. Sasa wale ambao wamepewa dhamana ya kusimamia wawe wabunifu ambao wanaweza kuleta mabadiliko badala ya kusubiri kila kitu wafundishwe au kuelezwa wafanyeje.
Vyoo vya shimo kwa Tanzania sasa ni aibu kubwa, na hili suala hata la kujadiliwa hasa kama wahusika wangekuwa ni watu wanaojitambua na kuachana kuamini kwa kuwa uwanja uko mkoani basi shida au kuwa na miundombinu duni ni sahihi.
Iko haja ya TFF na bodi ya ligi kuvifungia viwanja vyenye viwango duni na iko sababu ya CCM kushirikiana na serikali yake kuweka msisitizo viwango vya vyoo viwe vya kiwango sahihi kulingana na hadhi inayotakiwa.
Wako watu wanashindwa kwenda uwanjani kuangalia mpira kwa kuwa hali ya viwanja hivyo, uchafu, uduni wa sehemu kama hizo yaani vyoo. Hapohapo tunapiga kelele watu ni wachache viwanjani huku tukilalamikia mambo mengine kabisa.
Kambarage ni kongwe, imeingiza fedha nyingi sana kupitia ligi kuu na ligi nyingine na kama viongozi wangekuwa wabunifu wangeishajenga vyoo bora kabisa, vyumba bora kabisa ya kubadilishia nguo wachezaji na ingewezekana kabisa kuwa na mabafu.
Tuachane na kufikiri kama zamani, hii ni sasa na wakati huu mambo yamebadilika kabisa. Lazima tukubali, suala la kuboresha viwanja haliwezi kuwa la sehemu ya kuchezea pekee, kukaa pekee badala yake mazingira bora ya viwanja kwa wachezaji na watazamaji pia huku viongozi wanaosimamia viwanja au wamiliki wajichukulie kama wafanyabiashara wanaotakiwa kutoa huduma bora.
Brother Saleh hapo umezungumza maneno haswa. Lakini sio vyoo tu bali kuna mambo mengi ya aibu yaliyojikita katika miundo mbinu ya michezo hasa viwanja ambayo ukiayaangalia si suala la kutokuwa na uwezo bali ni uzembe uliojijenga katika tabia za kivivu na kuishi kwa mazoea ya fikra potofu yakwamba usafi ni anasa au uzungu na mwaafrica mazingira yake ni machafu. Mfano utaona baadhi ya viwanja vyetu vya ligi au hata baadhi ya viwanja wanavyofanyia mazoezi timu ambazo tunaziita timu kubwa yaani Simba na Yanga mazingira yake ni mabovu kwani ukiachilia mbali sehemu inayofanyiwa mazoezi maeneo mengine inayoizunguka sehemu hiyo huwa ya hatari kabisa ni msitu hasa. Na kaama mpira utadondokea huko kazi ya kwenda kuutafuta ni shughuli nyengine. Kwa wenzetu maeneo ya wazi ikiwemo viwanja vya michezo ni mapambo na siku zote huwa ni sehemu zinazokuwa chini ya uangalizi bora wa kimazingira hata kama hakuna shughuli yeyote inayofanyika pale lakini kwetu sisi ni majalala au madamps na la kushangaza zidi maeneo yetu huwa na shughuli maulumu zinazokusanya watu maalumu kabisa karibu kila siku lakini katika mazingira mabovu, sasa kama si mambo ya aibu kitu gani? Watanzania lazima tubadilike kwani kuna baadhi ya mambo sio suala uwezo bali ni tabia mbaya. Mimi nitoe rai tu kwa mamlaka zetu husika kukadhania katika kuwatoza watu ada au ticket kwa wale watakaoshindwa kuweka mazingira yao safi. Na yule atakaeshindwa kulipa ada basi kuwepo na sheria ya kwenda kutumikia kifungo jela. Kweli chungu lakini hizo ndio sheria za nchi za wenzetu tunazozihusudu kuwa zipo safi. Watu wake wanadabu katika kutunza mazingira yao lakini adabu hizo hazikuja bure bure bali wameadabishwa na sasa imekuwa ni way of life. Watanzania bado hatuna adabu katika masuala ya kuyaweka mazingira yetu katika hali ya usafi. Sina hakika kama sheria hizo zipo Tz na kama zipo pengine zipo kimzaha mzaha sio serious na endelevu. Kwa wenzetu ukikutikana unamwaga mkojo wako katika mazingira ya wazi hata kama porini unaweza kuingia matatani na kunauwezokano mkubwa kufikishwa mbele ya vyombo sheria kujieleza kwanini usiazibiwe kwa uchafuzi wa mazingira. Sasa kwa kwetu sehemu za halaiki ya watu utakuta zinanuka uvundo na bado mamlaka husika wanaona ni vitu vya kawaida tu kwa kweli kuna tatizo. Zitozwe ada za adhabu bila muhali kwa wanaotekeleza au kuyaacha mazingira yao katika hali ya uchafu na katika usimamizi wenye uadilifu wa tozo hizo ugharamie usafi wa mazingira hayo au hata hilo la usafi asubiriwe Maghufili kulikemea?
ReplyDelete