Kipa namba mbili wa Simba, Said Mohammed 'Nduda', amesema kuwa leo Jumatatu anatarajia kuanza mazoezi rasmi ya pamoja na timu hiyo huku akitamka kuwa anarejea kwa kazi moja pekee ya kudaka katika kikosi cha kwanza nafasi inayochezwa na Aishi Manula.
Nduda alikuwa nje ya uwanja kwa muda wa zaidi ya miezi mitano akiuguza majeraha ya goti ambalo alifanyiwa operesheni tangu Oktoba, mwaka jana nchini India alikopelekwa kwa ajili ya matibabu.
Kipa huyo, alipata majeraha hayo akiwa kambini Unguja, Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Nduda alisema alitakiwa aanze mazoezi ya pamoja tangu wiki iliyopita, lakini aliuomba uongozi wa timu hiyo aanze mazoezi leo kwa ajili ya kumalizia programu ya mazoezi ya gym na ufukweni.
Nduda alisema, anarejea uwanjani akiwa yupo fiti na tayari kwa ajili ya kuitumikia timu yake hiyo inayojiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika ambao wenyewe wataanza kucheza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Gendermerie Tnale ya Djibouti.
“Ninajisikia furaha nikirejea uwanjani kuitumikia timu yangu ya Simba ambayo tangu nimejiunga nayo msimu huu sikuwa nayo pamoja.
“Ninaamini kurejea kwangu kutaimarisha kikosi chetu kinachojiandaa na michuano ya kimataifa na ligi kuu inayoendelea na kikubwa nitarejea uwanjani kwa lengo moja la kudaka katika kikosi cha kwanza, hivyo nimejiandaa na ushindani wote nitakaokutana nao,” alisema Nduda.
0 COMMENTS:
Post a Comment