Kocha wa Yanga, George Lwandamina ni mjanja sana kwani ametengeneza kikosi ambacho sasa hakimtegemei mchezaji mmoja katika kupata mafanikio.
Maana yake ni kwamba, sasa Yanga inaweza kumtumia mchezaji yeyote ambaye amesajiliwa na anafanya mazoezi na timu hiyo ili kuweza kupata matokeo mazuri katika mchezo wowote ule.
Kwa mujibu wa nahodha msaidizi na beki wa Yanga, Kelvin Yondani ametamba kuwa, timu yao sasa inaweza kupambana na kikosi chochote kile bila ya kumtegemea mchezaji mmoja au wawili kama zamani.
Yondani alisema bila ya kiungo mkabaji, Papy Tshishimbi na mshambuliaji, Obrey Chirwa wana uwezo wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga imepangwa kucheza na Wolayta Dicha ya Ethiopia katika mechi ya kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho na katika mechi ya kwanza itawakosa Tshishimbi, Chirwa na Said Makapu wenye kadi mbili za njano.
Yondani alisema anampongeza Lwandamina kwani amekitengeneza kikosi kipana ambacho hakimtegemei mchezaji mmoja kupata ushindi.
“Ukiiangalia Yanga hii ni tofauti kabisa na misimu mingine iliyopita ambayo ilikuwa ikimtegemea mchezaji mmoja pekee au wawili ambao kama wakikosekana kunakuwa hakuna mbadala wao.
“Lakini Yanga ya hivi sasa kila mtu ameiona, iliandamwa na wachezaji wengi majeruhi wanafika hata kumi, lakini kocha alijitahidi kuwatengeneza wengine na kuchukua nafasi zao.
“Mfano alikosekana Tambwe (Amissi), Chirwa (Obrey) na Ngoma (Amissi) ambao ndiyo namba tisa wetu, lakini Buswita (Pius) ambaye ni kiungo alichezeshwa nafasi hiyo na kufanya vizuri huku akifunga mabao.
“Hivyo, basi kukosekana kwa Chirwa na Tshishimbi katika mechi yetu ijayo ya Kombe la Shirikisho Afrika hakuwezi kuwa sababu ya kutofanya vizuri kwetu,” alisema Yondani.
Yanga inatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza na Wolayta kati ya Aprili 6-8 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana Aprili 16-17 nchini Ethiopia.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment