March 24, 2018






NA SALEH ALLY
KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana Machi 14, mwaka huu ilifikia uamuzi wa kumfungia maisha kujihusisha na soka Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo, Michael Wambura.


Wambura amefungiwa maisha baada ya kubainika ana makosa kupitia vipengele vitatu baada ya kamati hiyo kuweka makosa yake mezani naye akatoa utetezi wake kupitia wakili wake, Emmanuel Muga.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, inaeleza Muga alimtetea Wambura baada ya kujaribu kuomba muda wa kuandaa utetezi, kamati ikakaa kulijadili na kuona kwamba halikuwa geni kwa Wambura, hivyo alipaswa kuwa amejiandaa kutoa utetezi baada ya kupewa nafasi tatu, ajitetee kwa maandishi, atume mwakilishi au kwenda mwenyewe.

Baada ya hapo, Muga aliandaa utetezi na kuanza kujibu mashitaka hayo kupitia tuhuma tatu tofauti ambazo ni 1. Kupokea/kuchukua fedha za shirikisho (TFF) za malipo ambayo  hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.

2. Kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya Kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo siyo halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.

3. Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015).

Baada ya utetezi wa Muga akiwa mwakilishi wa Wambura, kamati hiyo ya maadili ilitoa uamuzi wake kwa kutangaza imemfungia Wambura maisha.

Kufungiwa maisha kwa Wambura kumeishitua jamii ya mchezo wa soka nchini, mimi ni kati ya tulioshitushwa kuona mdau kama Wambura anafungiwa kwa kipindi hicho. Kama ingekuwa ni maoni binafsi naweza kusema si sawa.

Lakini kila mmoja wetu anajua, kama kuna kanuni au sheria katika jambo fulani lazima zizingatiwe badala ya kupeleka au kuitanguliza huruma ya moyo.

Kitu kilichonivuta kuandika makala hii ni baada ya kuona mijadala mingi imekuwa ni ya kishabiki sana badala ya kuangalia hali halisi na kulijadili hili jambo kwa faida ya mpira wa Tanzania badala ya kuangalia upuuzi wa timu (Wallace) Karia au timu Wambura.

Vizuri kwa wadau wakaangalia mpira wa Tanzania ambao utaendelea baada ya Karia na Wambura ambao miaka miwili, hakuna hata mmoja alikuwa katika nafasi aliyokuwa nayo leo hadi lilipoibuka leo.

Ukweli, uwe wazi. Wambura kama alipata nafasi ya utetezi, halafu akaadhibiwa na kama kamati imetenda hadi yake ni jambo sahihi na anapaswa kuadhibiwa. Kusiwe na propaganda ya kutaka kumtetea kwa kuwa wako wenye mapenzi naye binafsi au wana maslahi yao. Maslahi namba moja yawe ni mpira wa Tanzania.

Tayari Wambura amekata rufaa, achana na zile propaganda kwamba alikwenda ofisini Jumamosi, akijua wafanyakazi siku hiyo wako mapumziko. Wambura ni makamu wa rais wa TFF, vipi hakujua hilo? Sasa linaweza lisiwe ishu kwa kuwa rufaa yake ilipokelewa.

Sasa kama imepokelewa, kamati inayofuatia kusikiliza ni ile ya rufaa. Inapaswa kuwa kamati huru kweli na ifanye kazi yake kwa weledi sahihi bila ya shinikizo na kama itaonekana Wambura hana hatia basi arejeshwe. Kama ataonekana kweli alikuwa ana hatia, basi aadhibiwe.

Kikubwa kinachotakiwa ni uwazi wa mambo na namna jambo linavyofanyika. Ili Watanzania wajue kilichotokea hadi kufikia uamuzi wa jambo.

Baada ya uamuzi, ikatokea Wambura ameshinda rufaa yake, litakuwa ni jambo zuri kuamini uamuzi wa kamati na kuuheshimu badala ya kuanza kutengeneza propaganda kwamba amependelewa au kuna jambo ambalo si sahihi.

Vivyo hivyo, kama itatokea kamati ya rufaa nayo bado imeona Wambura ana hatia, basi kuna kila sababu ya wadau kuheshimu mawazo na kuachana na kuingiza propaganda zisizokuwa na maana hata kidogo.

Nimeona kwa sasa waandishi wengi wameshindwa kuandika suala la Wambura kujadili na kusema ukweli bila ya woga kwa kuwa tayari kuna wahariri wamesukumiwa kashfa ya kwamba walihongwa ili kumkandamiza Wambura.

Propaganda ya kuwafunga midomo wahariri kuhusiana na jambo hilo inaonekana kufanikiwa. Ukweli ni kwamba lazima wasimame imara bila ya kuwa na upande na kuueleza umma kilicho sahihi na kisicho sahihi.

Kwa upande wa Wambura, pia wanapaswa kutulia na kufuata utaratibu badala ya zile hoja za kufuja fedha au kueleza walioajiriwa ndani ya TFF si sahihi, wakati mwezi uliopita Wambura alikuwa makamu wa Rais TFF na hatukuwahi kusikia akikemea hilo au hayo anayoyasema.

Kama yeye ndiye mwenyekiti wa kamati ya fedha, vipi alikuwa kimya na matumizi hayo na hakusema kitu, vipi anasema leo? Tuamini ni muoga au alihusika na anasema sasa hivi kwa ajili ya kukomoa au kuonekana ameonewa?

Ndiyo maana nasisitiza, huu si wakati mwafaka wa malumbano yanayoweza kutukimbiza nje ya hoja. Badala yake tuache mlolongo ufuatwe kupitia njia sahihi na mwisho badala ya hoja nje ya hoja, tuwe na hoja sahihi kuhusiana na kilicho mbele yetu.

Msisitizo wangu ni huu, kama Wambura amekosea, basi achukuliwe hatua na kamati iwe wazi. Kama hana hatia na kamati itabaini hivyo, basi imuache awe huru na kuendeleza mapambano ya maendeleo ya mpira nchini.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic